Dar/Mikoani. Katika kile kinachoonekana kuendelea kujiimarisha
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vimegawana maeneo mbalimbali nchini vikifanya mikutano
ya hadhara na mafunzo kwa viongozi wake ikiwa ni utekelezaji wa mkakati
wa ushindi.
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Chadema kilianza ziara zake mikoani wiki
zilizopita baada ya kuzindua mkakati wake uitwao ‘Hakuna kulala, Hakuna
kula, Mpaka Kieleweke’ nchi nzima wakati timu ya NCCR-Mageuzi ikiweka
kambi mkoani Kigoma kwa kile ilichokiita kuimarisha majimbo ya
kimkakati.
Sanjari na vyama hivyo, CUF tangu juzi kiliingia
katika moja ya ngome zake, mkoani Mtwara pamoja na mipango mengine ya
kiushindi, kinahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura.
Jitihada za Ukawa kuzunguka mikoani zinakuja ikiwa
ni majuma kadhaa tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Katibu
Mkuu wake Abdulrahman Kinana kilipomaliza ziara ya kujiimarisha na
kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Pia, ziara hizo ziligongana na zile za Chama cha ACT - Wazalendo zilizosababisha Chadema na chama hicho kipya kugongana Butiama.
ACT - Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe
kilihitimisha ziara yake ya kimkakati katika mikoa tisa inayoonekana
kuwa ngome ya CCM, wiki iliyopita wilayani Bariadi, Shinyanga na kuvuna
wanachama zaidi 6,000 katika mikoa hiyo.
NCCR-Mageuzi ipo Kigoma
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema jana kuwa Ukawa ina mikakati inayofanana ndani ya vyama vyao ya
kuhakikisha inajiimarisha kisiasa nchi nzima ili ishinde Uchaguzi Mkuu.
Alisema siku 10 zilizopita, timu ya NCCR
ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti - Zanzibar, Haji Hamis Hamad ilianza
ziara Kigoma kuhakikisha majimbo ya mkoa huo yanaendelea kuwa ngome
yake.
“Kigoma nzima ina majimbo yetu ya kimkakati na
Ukawa wameshatukabidhi sasa kilichobaki ni kufanya ‘political
management’ (usimamizi wa kisiasa) katika kiwango kinachotakiwa.
“Katika kikosi hicho, pia wamo Katibu Mwenezi,
David Kafulila, Katibu Mkuu Mstaafu, Samuel Ruhuza na Kamishna wa
Kagera, Peterson Mshenyela na wengineo,” alisema Nyambabe.
Alisema baada ya kumalizika ziara katika mkoa huo viongozi hao
wataelekea Kagera kwa kuanzia majimbo ya Ngara na Nkenge, maeneo ambayo
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anaendelea kumwaga ‘cheche’.
Kinachoendelea katika ziara hizo ni kama
mashambulizi ya ‘bandika bandua’ na kuzuia mparaganyiko ndani ya vyama
hivyo ambao unaweza kutokea baada ya kuanza kwa mchakato wa kugawana
nafasi za udiwani na ubunge.
Chadema kila kona
Chadema, inayoendelea na utoaji wa mafunzo ya
uongozi bora kwa viongozi wa ngazi zote na makada waliotia nia ya
kugombea na mikakati mingine ya ushindi, viongozi wake wa juu
wametawanyika maeneo tafauti katika kanda zake 10 za kiutendaji.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa aliyekuwa
Morogoro alieleza kuwa Tanzania kwa sasa inasifika nje ya nchi kwa
uvunjifu wa haki za binadamu.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara kwenye
Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro juzi,
Dk Slaa alisema katika kipindi cha miaka mitano, utawala wa Rais Jakaya
Kikwete umekuwa na matukio mengi ya uvunjaji wa haki za binadamu.
Alisema hivi karibuni alikuwa Marekani kwa ziara
maalumu na huko alihojiwa na waandishi wa habari katika kituo kimoja cha
redio juu ya masuala ya utawala bora nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum
Mwalimu akiwa mkoani Rukwa alisema CCM imepoteza baraka za Mungu kiasi
cha kushindwa kujua mgombea wake wa urais mpaka sasa, jambo ambalo
halijawahi kutokea katika historia ya chama hicho.
Mwalimu aliyekuwa akizungumza kwenye Ukumbi wa
Libori Mjini Sumbawanga, alisema viongozi wanaotokana na Chadema wapaswa
kuwa tayari kusimamia haki kwa gharama zozote, kukataa rushwa na
kupunguza kero kwa wananchi na kuwaonya wasije wakaufanya utawala wa
Chadema kuwa kama wa CCM ambayo inayumba.
“Tuna miezi mitatu imesalia tuanze kampeni, lakini
mpaka sasa CCM haijamjua mgombea wake, lini imewahi kutokea? Mungu
amewachanganya kama wajenzi wa karavati,” alisema Mwalimu ambaye baada
ya mkutano huo aliendelea na ziara yake mjini Makambako, Njombe.
Mwalimu alionyesha kushangazwa na baadhi ya
wafuasi wa Chadema kujiunga na chama cha ACT – Wazalendo na akakiita
kuwa ni chama cha msimu ambacho kitapotea baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akiendelea na ziara yake mkoani Kagera, Mbowe
alisema kusuasua kwa uandikishaji wa wapigakura ni kiashiria cha
uvunjifu wa amani inayotokana na hofu ya CCM kuangushwa Oktoba.
Akiwahutubia wakazi wa Mji wa Bukoba juzi katika Uwanja wa
Uhuru, Mbowe alisema nchi inaweza kuingia katika machafuko endapo
litakuwapo jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kama upigaji kura
wa Katiba Inayopendekezwa ulivyoahirishwa.
Alisema uchaguzi siyo suala la dharura na kila
hatua inatakiwa kuwekwa wazi ili kuondoa hofu iliyoanza kujengeka
kutokana na kubakia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Profesa Lipumba, Mtwara
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema
kuwa endapo Wapinzani wataingia madarakani, kazi ya kwanza
itakayofanyika ni kufumua mikataba yote iliyoingiwa bila kufuata
taratibu.
Alisema asilimia kubwa ya mikataba iliyoingiwa na
Serikali, haiwanufaishi Watanzania walio wengi na zaidi ya hapo haina
tija kwa Taifa.
“Haiwezekani Watanzania wakaishi katika hali ya
umaskini wakati wana rasilimali nzuri, zinazowafanya wafaidi matunda ya
nchi yao, lakini kuna wajanja wachache wanaingia mikataba isiyo na tija,
sasa tukiingia madarakani, tutaifumua,” alisema Profesa Lipumba ambaye
leo atakuwa Kijiji cha Msimbati.
Juzi, akiwa katika Mji wa Mikindani mkoani Mtwara
aliionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuacha kushughulikia suala la
Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na badala yake ijikite kuandaa
mazingira ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu ili kulinusuru Taifa kuingia
katika mgogoro usio wa lazima.
Profesa Lipumba alisema NEC isipoteze rasilimali za Taifa na muda kwa jambo lisilo na tija kwa wakati huu.
“Jaji Lubuva (Damian, Mwenyekiti wa NEC)
asiliingize Taifa katika mgogoro, ana haraka gani na Katiba
Inayopendekezwa wakati hili la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura hajalimaliza...? Ashughulikie hili la daftari ndiyo kazi yake
kwa sasa, siyo Katiba,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na
wananchi.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment