Saturday, April 25, 2015

Chadema yaifanyia umafia CCM

Ukerewe. Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimeweka mkakati utakaowafanya makada wake wavamie majimbo yanayoshikiliwa mapema na CCM, huku wakichelea kuingia kwenye majimbo yaliyo chini ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mongella mjini hapa, mkutano ambao ulifurika maelfu ya watu.
Mbowe alitangaza kupiga marufuku wanachama wa Chadema kuanza kutangaza nia kwenye majimbo ambayo wenzao wanayashikilia hadi hapo Bunge la Jamhuri ya Muungano litakapovunjwa.
Lakini alisema wanachama wa Chadema wanaruhusiwa kuanza purukushani kwenye majimbo ambayo yanashikilia na vyama vingine hasa chama tawala cha CCM ambacho kinashikilia majimbo mengi.
“Naomba ifahamike Chadema ni zaidi ya ubunge, tunahitaji amani na siyo kuharibu chama. Chadema itasimamisha watu makini kwenye maeneo yote katika uchaguzi huu,” alisema mwenyekiti huyo ambaye yuko kwenye ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mbowe ambaye hakugusia suala la Ukawa katika mkutano huo, alisema kuwa utaratibu utaandaliwa wa kupata wagombea na kwamba hata waliokuwa wabunge, wasijihakikishie kuwa watapitishwa tena kwenye maeneo yao wanayoyaongoza sasa.
“Tutakuja na utaratibu mwingine. Hata wabunge wa Chadema waliokuwa katika maeneo hayo, wasidhani kwamba watabakia hapo. Tutasimamisha mtu anayekubalika na watu wote, na utaratibu ukiwekwa, hata aliyekuwa mbunge anaweza kuondolewa,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa Chadema inaamini kuwa katika kila eneo kuna mtu wake ambaye ni makini na ni wazi atashinda.
Vyama vinne vya upinzani, Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kwenye uchaguzi wa madiwani hadi rais. Vyama hivyo, vilivyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimekubaliana kuwa kila chama kipate mgombea wake na baadaye vitachambua anayekubalika na wengi.
Ainanga Nec
Akizungumzia mwenendo wa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, Mbowe alisema Taifa kwa sasa liko kwenye giza nene kutokana na maandalizi mabovu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec).
Mbowe alisema kucheleweshwa kwa kazi ya uandikishaji wapigakura ni sehemu ya njama za CCM kupitia Serikali yake inayotamani kutumia nafasi hiyo ili kuendelea na hujuma katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

No comments:

Post a Comment