Dar es Salaam. Tanzania jana iliadhimisha miaka 51 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar huku viongozi wa upinzani wakisusia sherehe
hizo za mwisho katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambazo, makomandoo
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walitia fora.
Rais Kikwete alikagua gwaride hilo katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali pamoja na maelfu ya wananchi
ambao baadhi walilazimika kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa kufuatilia
shughuli hizo.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na, Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Sharrif Hamad. Wengine ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Rais
mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wapinzani wasusia
Viongozi wakuu wa vyama vya upinzani hawakushiriki
maadhimisho hayo baadhi wakiwa mikoani katika shughuli za kuimarisha
vyama vyao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe yuko mkoani Kagera na Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye yuko mkoani Mtwara.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe hawakuhudhuria na
sababu za kutokuwapo kwao hazikuelezwa.
Wakuu waliokosekana
Pia, baadhi ya viongozi wa kitaifa hawakuonekana
katika sherehe hizo akiwamo Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan
Mwinyi, Mawaziri wakuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba, John
Malecela, Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya, Edward Lowassa.
Kikwete uwanjani
Kama ilivyo kawaida, msafara wa Rais Kikwete
aliyekuwa na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange katika gari maalumu la
jeshi lililozungukwa na magari mengine saba na pikipiki 15, ulizunguka
uwanja huku kiongozi huyo akipunga mkono na kushangiliwa kwa nguvu.
Hatua hiyo ilifuatiwa na wimbo wa Taifa sambamba na mizinga 21
na kisha Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alikagua gwaride la
vikosi vya ulinzi na usalama.
Hata hivyo, wakati akikagua gwaride hilo, Rais
Kikwete alipofika kwenye Kikosi cha Bendera, alisahau kupokea heshima
hali iliyomfanya arudi nyuma kufanya hivyo kisha kuendelea kukagua
vikosi vingine.
Baada ya hapo, ndege za kivita zilipita juu ya
uwanja zikitokea Kaskazini kulekea Kusini mwa uwanja. Tukio hilo
liliwafanya wananchi waliofurika katika uwanja huo kushangilia hasa kwa
jinsi ndege hizo kivita zilivyokuwa zikifanya madoido angani.
Ndege hizo zilifuatiwa na gwaride la nje
lililokuwa na vikosi 13 vikiongozwa na bendera ya Rais na ile ya JWTZ
zilizokuwa sambamba na bendera saba, sita zikiwa ni za vikosi vya
majeshi ya ulinzi na usalama pamoja na ya kikundi cha usindikizaji.
Vilipita mbele ya Rais kwa mwendo wa haraka. Baadaye Vilifuata vikosi
viwili; Kikosi Maalumu cha Wanamaji (Marine Special Force) na makomandoo
vikiwa katika mwendo wa mchakamchaka.
Baada ya makomandoo kupita, alifuata askari polisi
mmoja wa jeshi (MP) aliyepita peke yake kwa mwendo wa ‘digidigi’ na
kushangiliwa kwa nguvu.
Makomandoo
Sherehe hizo zilikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na manjonjo ya makomandoo hao walipokuwa wakipita mbele ya Rais Kikwete.
Kikosi cha makomandoo hao kikiwa katika mavazi ya
kivita, bunduki, mabegi mgongoni hukuwa wakiwa wamepaka rangi nyuso zao,
waliingia huku wakikimbia mchakamchaka na kushangiliwa kwa nguvu.
Halaiki
Sambamba na makomandoo, halaiki ya watoto
iliyoonyesha mafunzo katika meli ya kivita nayo iliwanyanyua wananchi
katika viti vyao kushangilia huku waliokaa jukwaa kuu wakiinua bendera
na kuzipepea.
Halaiki hiyo iliyoingia uwanjani saa 5.10 ilianza
kwa kutoa ujumbe wa sherehe hizo kwa mwaka huu ambao ni “Miaka 51 ya
Muungano, Tudumishe Amani na Umoja, Ipigie Kura ya Ndiyo Katiba
Inayopendekezwa na Kushiriki Uchaguzi Mkuu.” Kisha kuhamasisha kilimo
wakisisitiza matumizi ya zana za kisasa. Pia, watoto hao wa halaiki
walitoa ujumbe kupinga ujangili katika mbuga za wanyama ili kulinda
maliasili hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kadhalika, walihamasisha
ujasiriamali wa kutumia kazi za mikono.
Kivutio kikubwa katika halaiki hiyo ilikuwa ni
jinsi watoto hao walivyohamasisha ulinzi ambako walitoa ujumbe kuwa
suala hilo ni jukumu la wananchi wote. Wakati wanatoa ujumbe huo
walikuwa katika mwendo wa haraka huku wakienda mbele na nyuma na kutoa
burudani nzuri kwa hadhira iliyokuwepo uwanjani hapo pamoja na
watazamaji kupitia runinga.
Wakiendelea na onyesho la ulinzi, watoto hao walipita katika
vikwazo huku wakiruka na kupita katikati ya maduara makubwa ya vyuma
yaliyokuwa yanawaka moto na kisha kukanyaga makarai yaliyokuwa na moto
pia.
Pia kulikuwa na watoto watatu waliopita juu ya
kamba kwa staili tofauti na kuwavutia wazazi waliokuwapo. Wa kwanza
alipita huku akining’inia kwa mikono yake. Alifuatiwa na aliyeshika
kamba kwa mikono pamoja na miguu; uso ukielekezwa angani. Wa mwisho
alipita juu ya kamba hiyo kwa kutambaa.
Mazoezi mengine ni yake ya mfano wa meli ya kivita
yaliyokuwa yameandaliwa kwa umakini mkubwa. Watoto hao walipanda mnara
wa meli hiyo kwa aina tofauti. Kuna aliyepanda kwa mikono pasipo miguu
yake kugusa nguzo. Mwingine alipanda huku miguu yake ikiwa imenyooka
mbele na wa mwisho alipanda kwa kuruka ruka.
Wakiwa bado ndani ya meli hiyo, mmoja alijifunga
kamba mguuni na kuwanyanyua wenzake wawili kutoka chini. Ilikuwa ni
mithili ya filamu nzuri ya kivita.
Kabla hawajaondoka, walipita katika mfumo wa
vifaru vya kivita. Kimoja kikiwa cha kupiga masafa marefu na kingine
mafupi. Watoto watatu walitengeneza matairi ya vifaru hivyo. Usingependa
kuondoka wala kutaka watoto hao wamalize kuburudisha. Kwa hakika
walivutia.
Ngoma, Kwaya
Baada ya halaiki zilifuata ngoma za makabila.
Ngoma nne zilitumbuiza, mbili kutoka visiwani na nyingine bara. Pia
kwaya kutoka Chunya, Mbeya ambayo ilifuatiwa na wimbo maalumu.
Wapongeza
Akizungumzia sherehe hizo, Spika wa zamani wa
Bunge, Pius Msekwa alisema kudumu kwa Muungano ni suala la kujivunia
kwani yapo mataifa mengine yaliyoshindwa.
“Tumepita katika mawimbi makubwa au kero za
Muungano huu. Ingawa tumefanikiwa kuyavuka lakini ukweli ni kwamba
yametuyumbisha sana. Ninaandika kitabu ambacho kinazungumzia historia ya
Muungano tangu tulipouanzisha,” alisema Msekwa.
Alitoa mfano wa mataifa yaliyojaribu kuungana na kushindwa kuwa ni Senegal na Gambia; Malaysia na Singapore.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere,
Joseph Butiku alisisitiza vijana kujitokeza kwa wingi na kushiriki
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian
Lubuva alisema: “Nakumbuka sherehe za Muungano za mwaka 1977 niliteuliwa
kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na tangu hapo nimekuwa nikiitumikia
Serikali. Ni siku ya kumbukumbu yangu muhimu katika maisha na taaluma
pia,” alisema Jaji Lubuva.
Awali
Kabla ya sherehe hizo kuanza, milango ya Uwanja wa
Uhuru ilifunguliwa saa 12.30 asubuhi na wananchi kutoka maeneo
mbalimbali ya jiji kuanza kuingia. Mpaka inatimu saa 2.00 asubuhi uwanja
huo ulikuwa umejaa na wananchi kulazimika kuingia Uwanja wa Taifa.
No comments:
Post a Comment