Friday, April 24, 2015

Pengo aonya kuhusu urais, ashtushwa na wanaotumia fedha

Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mt Joseph Dar es Salaam wakimsikiliza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipokuwa akiwahutubia katika hafla ya mahafali ya 7 ya chuo hicho, jana. Picha na Said Khamis 


Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye alizua kizaazaa bada ya kutofautiana na maaskofu wenzake kuhusu Kura ya Maoni, jana alizungumzia suala la urais, akivitaka vyama vya siasa kuwaengua makada wake wanaotumia fedha kusaka urais.
Kardinali Pengo alisababisha mkanganyiko wakati alipotofautiana na tamko la Jukwaa la Wakristo lililotaka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na siku ya Kura ya Maoni, wapige kura ya hapana kukataa mabadiliko hayo ya Katiba.
Tamko hilo lililotolewa na maaskofu wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, lilieleza sababu kadhaa za kupingana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya, hasa suala la Serikali kuahidi kuingiza Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba kwa lengo la kutaka Waislamu waipitishe Katiba Inayopendekezwa.
Lakini Kardinali Pengo akakosoa tamko hilo akisema waumini hawana budi kuachiwa kufanya uamuzi wao bila ya kushurutishwa, kauli ambayo ilisababishwa akosolewa na wengi, akiwamo Askofu Josephat Gwajima ambaye amefunguliwa mashtaka ya kumdhalilisha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.
Jana, Pardinali Pengo alizungumzia masuala ya kisiasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT) ambako alionya dhidi ya matumizi ya fedha.
Akionya juu ya matumizi ya fedha katika harakati za kuingia Ikulu, Kardinali Pengo alisema kwa mujibu wa imani na kanuni za dini, uongozi ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba kamwe hauwezi kununuliwa.
“Kama wapo watu wanaotumia fedha kutaka kuingia Ikulu, ni bora wakaachwa mara moja na vyama vyao. Hata wasipitishwe na kuja kuomba kura kwetu. Ni vyema wakatambua kuwa uongozi haununuliwi,” alisema Pengo.
Alifafanua kuwa rushwa ni kitu kibaya kama itatumika kupata kiongozi katika ngazi yoyote ile na kwamba endapo mtoaji atapewa nafasi aitakayo, bila shaka gharama alizozitumia atataka zilipwe na wananchi anaowatumikia.
“Rushwa ni kitu ambacho kila kiongozi anapaswa kukiepuka ili kuwaondolea wananchi uwezekano wa kuingia katika mchakato wa kulipa deni ambalo kiongozi atataka alipwe (akiwa Ikulu) ingawa alitoa kwa hiari yake wakati wa kujinadi na kuwawishi wapigakura,” alisema. “Ni bora tumchague Rais maskini ambaye hatakuwa na madeni binafsi ya kuyalipa na kwa pamoja tuelekeze nguvu zetu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa kwa ujumla. Watoa rushwa mwisho wa siku watataka tulipe gharama walizotumia kutushawishi,” alisema kiongozi huyo wa kiroho nchini.
Pamoja na hayo yote, Askofu Pengo alisema ni lazima ushindani uwepo kuanzia ndani ya vyama kabla havijapata mwakilishi atakayesimama kuviwakilisha mbele wa wananchi ili wachague anayefaa zaidi kulitumikia Taifa.
Alisema ni vyema demokrasia ikaanzia huko kabla haijahubiriwa nje kwani hilo huonekana kabla hata vyama hivyo havijasema namna vinavyojiendesha.
Askofu huyo ametoa kauli hiyo wakati Taifa likiwa kwenye mjadala kuhusu sifa za wagombea urais, huku kukiwa na malalamiko mengi, hasa kutoka chama tawala cha CCM, dhidi ya makada wanaotuhumiwa kutumia fedha kushawishi wanachama wao wawapitishe kuwania urais.

CCM, ambayo mgombea wake ndiye amekuwa akishinda urais tangu siasa za ushindani wa vyama ziliporejeshwa mwaka 1992, imekuwa ikieleza mara kwa mara kuwa makada hao hawatavumiliwa na vikao vya uamuzi vitawaondoa katika mbio za kuwania kuteuliwa kugombea urais.
Mapema wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliwaambia viongozi wa chama hicho mkoani Dar es Salaam kuwa fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”, zitakuwa kitanzi chao kwenye Uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa wanachama hao watang’olewa.
Hata hivyo, chama hicho kimekuwa hakiripoti vitendo hivyo kwenye vyombo vilivyoundwa kwa ajili ya kuzuia na kupambana na rushwa na juzi, Takukuru ilisema chama hicho kikitoa ushirikiano, itaweza kukomesha uovu huo.
Akizungumzia demokrasia ndani ya vyama, Kardinali Pengo alitaka wagombea wengi zaidi kujitokeza ili kuwapa wananchi wigo mpana wa kuteua mtu anayefaa.
“Wajitokeze wengi zaidi ndani ya vyama vyao. Endapo vyama hivi vitadhihirisha demokrasia baina ya wanachama wao, ni dhahiri itakuwa sifa ya ziada kwa wananchi ambao ndiyo wapigakura wenye uamuzi wa mwisho,” alisema Kardinali Pengo.
Afya yake
Kwa muda wote wa sherehe hizo, Kardinali Pengo alikuwa ameketi kutokana na afya yake kutokuwa nzuri ikiwa ni muda mfupi tangu atoke India kwa matibabu ya mgongo na alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wote kuhusu hali yake.
Alisema kuwa maradhi hayo yalianza tangu mwaka 2013 na baada ya kwenda Ujerumani alibainika kuwa na tatizo hilo ambalo baadaye alishauriwa akatibiwe Hospitali ya Manipal iliyopo Bangalore, India.
“Ninaendelea vizuri. Maumivu yamepungua kwa kiasi kikubwa. Naomba wote wanaonitakia mema wasiwe na wasiwasi kwani matibabu niliyopata yalikuwa mazuri na yenye msaada mkubwa kwangu,” alisema kiongozi huyo ambaye anatembelea mkongojo.

MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment