Friday, April 24, 2015

Makamba: Nikiukosa urais sasa,vigumu kuupata tena


Dar es Salaam. Mbunge wa Bumbuli (CCM) na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema haweki utani katika suala la kugombea urais na akikosa kiti hicho kipindi hiki itakuwa vigumu kukipata miaka ijayo.
Makamba aliliambia gazeti hili, hivi karibuni jijini hapa, kuwa kauli zinazotolewa na watu, ikiwemo ile ya yeye kutumiwa kutangaza nia ili baadaye aje kumuunga mkono mgombea mwingine wa urais kwa tiketi ya chama hicho, inamkera na ‘kumnyima usingizi’.
“Urais nautaka sasa na si kipindi kingine chochote, na niseme tu wazi kwamba, hizi kauli kuwa natumiwa na watu zinaniumiza sana. Naamini kuwa ninaweza. Kama atakayepewa sasa (urais) ataharibu, ni vigumu sana kugombea tena urais na kuupata,” alisema Makamba ambaye amewahi kuwa mwandishi wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete.
Kauli hiyo ya Makamba aliyetangaza nia ya kuwania urais mwaka jana akiwa London, Uingereza imelenga kuwajibu wanaodhani kuwa anatumika kutibua harakati za vigogo wa chama hicho wanaoutaka urais.
Julai 9, mwaka jana Rais Kikwete alizungumzia nia ya Makamba kutaka kuwania urais, akisema mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”, na kwamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka.
“Nasikia kuwa bwana mdogo January anataka mambo makubwa. Mie hajaniambia, na mie nasikia. Hata alipogombea ubunge hakuniambia nilisikia baadaye... asilazimishe, wakati ukifika atapata, na akikosa asilete nongwa,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alitolea mfano wake aliposhindwa katika uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati akiwa na miaka 45 (miaka minne zaidi ya umri wa Makamba), akisema kuwa hakukata tamaa na aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee hadi alipofanikiwa kukalia nafasi hiyo ya juu mwaka 2005.
Kauli hiyo ilikuwa ya kwanza kutolewa na Rais Kikwete kuhusu wanachama wa CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama hicho kuwaonya makada sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka nafasi hiyo kubwa.
Akifafanua zaidi nia yake hiyo, Makamba ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yussuf Makamba alisema, “Wapo wanaosema kuwa ninautaka urais kwa sababu ninatumiwa na watu. Wapo pia wanaosema kuwa ninautaka urais kwa ajili ya kujitangaza ili niweze kupata nafasi nyingine za uongozi.”
Aliongeza: “Wanasema kuwa ninautaka urais sasa kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri ya kugombea (urais) mwaka 2025. Unajua kama CCM ikiweka mgombea ambaye si mzuri, mwaka 2025 utakuwa mgumu sana.”
Makamba alisema anaamini kuwa yeye ni miongoni mwa makada wasafi wa chama hicho tawala.
“Kuhusu suala la maadili sina shaka kabisa. Moja ya changamoto kubwa iliyopo nchini kwa sasa ni mmomonyoko wa maadili. Wapo viongozi wengi wanaoomba nafasi ya urais huku kukiwa na mashaka makubwa kuhusu uadilifu wao,” alisema.
 Alisema wapo viongozi wanaotumia pesa nyingi kutafuta nafasi hiyo kwa kuzigawa nchi nzima ila anaaamni viongozi hao hawawezi kuleta mabadiliko yoyote katika nchi hii yakiwamo ya kupambana na rushwa ambayo ni kansa inayoirudisha nyuma na kuitafuna nchi.

No comments:

Post a Comment