Friday, April 24, 2015

SOMA HAPA KUMFAHAMU VEMA MBUNGE SUGU

Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu).

Alizaliwa Mei Mosi, 1972 katika Hospitali ya Ligula, Mtwara, akiwa ni mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wanne upande wa mama yake,  Desderia Lungu.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1981 katika Shule ya Msingi Sanawari, Arusha kabla ya baadaye, mwaka 1982 kuhamia Shule ya Msingi Ligula, Mtwara. Mwaka 1984 akiwa darasa la nne, alihama tena kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam alikojiunga na Shule ya Msingi Sokoine, Temeke.
Katika kitabu chake cha Muziki na Maisha, Sugu anaeleza kwamba sababu kubwa ya kuhamahama, ilikuwa ni kuhamishwa kikazi kwa baba yake aliyekuwa akifanya kazi Idara ya Forodha. Baadaye alihamia tena Shule ya Msingi Sisimba, mkoani Mbeya alikohitimu darasa la saba.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Mbeya (Mbeya Day) alikosoma mpaka kidato cha tatu, akahamia Shule ya Sekondari Sabasaba, Mtwara alikohitimu kidato cha nne.
Matokeo ya kidato cha nne hayakuwa mazuri sana kwake, akaamua kujiunga na Chuo cha Equator Training College jijini Dar es Salaam alikosomea Clearing and Forwarding kwa ngazi ya cheti. Hata hivyo, hakumaliza kozi hiyo baada ya baba yake kufariki, akarejea Mbeya.
Baada ya kuona maisha yamekuwa magumu, alijaribu kuzamia Sauzi (Afrika Kusini) mwaka 1994 lakini ikashindikana, baadaye akarejea Dar es Salaam alikopata ajira ya ulinzi kwenye Kampuni ya Mafuta ya BP, Kurasini.
Tangu akiwa shuleni, Sugu pia alikuwa akijihusisha na muziki, alipopata ajira BP akaingia studio kwa mara ya kwanza na kurekodi Wimbo wa Siku Yangu, akitumia jina la 2 Proud na baadaye kukamilisha albamu yake ya kwanza iitwayo Ni Mimi iliyomtambulisha vyema kwenye muziki.
Baadaye alisimamishwa kazi BP, akazamia Ulaya nchini Uingereza kwenye mji mdogo wa Slough, nje kidogo ya London alikopata kibarua kwenye kiwanda cha kutengeneza dawa za meno. Alikaa kwa miaka kadhaa kabla ya kurejea Bongo kuendelea na harakati za muziki.
Mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye siasa baada ya kuchukua kadi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kugombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, akashinda na kufanikiwa kuingia bungeni. Mpaka sasa Sugu ni Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

No comments:

Post a Comment