Wednesday, July 2, 2014

DIAMOND AWADATISHA MASTAA WA MAJUU

Next level! Staa wa Bongo Fleva ambaye kwa sasa anafanya kweli kimataifa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameandika historia kwenye Tuzo za Black Entertainment Television (BET) 2014 huku akiwatia kiwewe mastaa wakubwa kama Cornell Iral Haynes ‘Nelly’, Christopher Maurice ‘Chris Brown’ na wengine kibao.

 Diamond akisalimiana na Nelly.

Tukio hilo lilijiri usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii kwenye Ukumbi wa Nokia Theatre jijini Los Angeles, Marekani ambapo Diamond alikuwa ameteuliwa kuwania Kipengele cha Mwanamuziki Bora kutoka Afrika akiwa sambamba na mwanamuziki Davido (Nigeria), Mafikizolo (Afrika Kusini), Tiwa Savage (Nigeria), Toofan (Togo) na Sarkodie (Ghana).
TUZO YAENDA KWA DAVIDO
Tuzo hiyo haikuwa bahati kwa Diamond kwani ilikwenda kwa Davido.
Licha ya kukosa tuzo hiyo, yapo mengi ambayo Diamond ameweka historia au rekodi katika ‘event’ huku kuunganishwa na mastaa hao ikiwa topiki muhimu.
MCHUMBA WA CHRISS BROWN AMSHOBOKEA
Katika hali ya kushangaza, mwanamitindo maarufu Marekani ambaye ni mchumba wa Chris Brown, Karrueche Tran alionekana kumshobokea Diamond mara alipokutana naye uso kwa uso.
Karrueche alijikuta hajiwezi alipokuwa  akimhoji Diamond ambapo moja kwa moja alimvutia kipaza sauti na kuanza kumpiga maswali huku akionesha kuvutiwa naye kwa muonekano aliokuwa nao.

 ...akihojiwa na demu wa Chris Brown.

Karrueche alikuwa akijichekeshachekesha huku akimhoji kuhusiana na mwanamuziki ambaye Diamond anamkubali ambapo alijibu ni Chris Brown, wote wakajikuta wakiangua kicheko.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Karrueche muda wote aliendelea kumshangaa na mwisho wa siku wakabadilishana namba za simu.
MASTAA MACHO JUU
Ulipofika wakati wa utoaji tuzo katika kategori ya Mwanamuziki Bora kutoka Afrika, lilipotajwa tu jina la Diamond kutoka Tanzania na wimbo wake wa Number One RMX, mastaa kibao walionesha kushangaa na ndipo macho yote yakahamia eneo aliokuwa amekaa.
Wengi walionekana kutoa maneno ya chinichini sambamba na kumuoneshea vidole wakionesha kumkubali kwa kutinga mjengoni hapo.
NELLY, CHRIS BROWN WAINGIWA KIWEWE
Wakati Diamond anaingia ukumbini, mastaa mbalimbali duniani walionekana kumshangaa na kati yao alikuwa ni Nelly ambaye aliushikilia mkono wa Diamond kwa sekunde kadhaa akitaka waendelee kupiga stori.

 Diamond akiwa kwenye pozi

Wakiwa katika zulia maalum jekundu, Nelly aliyewahi kutamba na wimbo wake maarufu wa Dilemma alionekana na kutaka kumfahamu zaidi Diamond.
Kila sehemu aliyokuwa akienda, Nelly hakutaka kumuacha na alionekana kuambatana naye kwa kumng’ang’ania mkono kila kona akipiga naye picha na kuzunguka eneo lote wakiwa pamoja.
Naye Chris Brown ambaye aliangusha bonge la shoo alionekana kumshangaa Diamond huku akitamani kuendelea kukaa naye.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu ukumbini humo, maswali mengi yaliibuka kuwa iweje, kwa Mtanzania kama yule kukanyaga katika mjengo mmoja na mstaa wa dunia.
TYSON, MAYWEATHER WADUWAA
Mabondia maarufu duniani akiwemo Floyd Mayweather na Mike Tyson walijikuta wakiduwaa kwa kumshangaa kwa kila hatua aliyokuwa anapiga. Macho yao hayakuwa mbali naye na hata katika zulia jekundu, Maywearher, baada ya kumaliza kupiga picha akiwa na mkewe alimfuata Diamond na kuongea naye mawili-matatu kuonesha kukumkubali.
MASTAA KIBAO WAGOMBEA NAMBA
Wakati shoo hiyo ikiendelea baadhi ya msataa waliokuwa pembeni na  Diamond walionekana kumfagilia na hata wengine kuomba namba za simu kwa malengo tofauti ikiwa ni pamoja na kutaka kufanya naye kolabo katika siku za usoni.


Cornell Iral Haynes ‘Nelly’, akiwa kwenye pozi

LUPITA, DIAMOND USO KWA USO
Staa kutoka Kenya ambaye anatingisha katika soko la filamu za Hollywood, Marekani kupitia filamu ya 12 Years A Slave, Lupita Nyng’o alikutana uso kwa uso na Diamond wakiwa wote wametokea Ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Walionekana kuwa na furaha kwa pamoja na ikumbukwe kuwa Lupita amejizolewa umaarufu mkubwa ambapo hata Jay-Z na Rihanna waliwahi kuandika kupitia kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii wakioneshwa kumkubali kwa kazi zake.
Mastaa wengine wakubwa aliokutana nao ni pamoja na Ashanti, DJ khalid, Jeniffer Hudson, French Montana, John Legend, Paris Hilton na wengine kibao
HABARI NYUMA YA PAZI
Duru za kibahari zilieleza kwamba mambo yote yanayokea kwa Diamond kuna nguvu kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye hivi karibuni alimkutanisha mtoto huyo wa Tandale na meneja wa wanamuziki wakubwa duniani, Tremaine Neverson ‘Trey Songz’ na Sean Michael Leonard Anderson ‘Big Sean’, ili kufanya nao kazi.
“Siyo jambo rahisi na bado milango itazidi kufunguka zaidi kwani JK aliahidi kumsaidia. Kwa kuunganishwa na mastaa wakubwa duniani sasa hivi utasikia amehamia Marekani kutusua mtonyo,” alisema mmoja wa wasanii wa Bongo Fleva ambaye naye anafanya vizuri.

 Christopher Maurice ‘Chris Brown’ akiwa kwenye pozi

Akizungumza na mwanahabari wetu kutoka jijini Los Angeles, Diamond alisema kuwa hakuamini jinsi alivyopokelewa na mastaa wakubwa ambao hakutarajia kukutana nao uso kwa uso.
“Sasa najua ndoto itatimia. Mastaa wakubwa lakini wamenionesha upendo wa ajabu. Naona wasanii wote duniani wanapendana sana. Jamaa hawana ubaguzi. Walinichangamkia sana utadhani tunafahamiana.
“Kuna mengi nafanya nao lakini siwezi kuwataja kwa sababu si unawajua Wabongo?
“Lakini nikidondoka tu Bongo naachia video mbili kali sana, mashabiki wangu wasikilizie.
“Kuhusu kukosa tuzo, mimi naona ni mwanzo mzuri. Inanipa hasira ya kutengeneza muziki mzuri utakaopendwa na watu wengi duniani. Tusikate tamaa, ni mwanzo mzuri. Pia asiyekubali kushindwa si mshindani,” alifunguka Diamond akimshukuru Mungu kwa yote anayomtendea kila kukicha kisha watu wanampa sapoti.

 Mike Tyson akiwa kwenye pozi

SASA LEVO ZA AKINA HASHEEM THABEET
Kwa sasa Diamond anakuwa ni staa mwingine wa Kibongo wa kimataifa akitanguliwa na staa wa NBA, Hasheem Thabeet, Modo Flaviana Matata na wengineo.






No comments:

Post a Comment