Dodoma. Vita kati ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),
David Kafulila imeingia katika sura mpya baada ya mbunge huyo, kuwaeleza
wapigakura wake kuwa endapo litatokea jambo lolote baya kwake, mhusika
namba moja ni mwanasheria huyo.
Wakati Kafulila akisema hayo, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amemtaka mbunge huyo
kuonyesha uanaume wake kwa kuzungumza tuhuma zake akiwa nje ya Bunge.
Maswi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam
kwenye semina ya wizara hiyo na waandishi wa habari huku akisisitiza
kwamba yeye ni msafi na yupo tayari kuchunguzwa na yeyote. “Nina usongo
naye,” aliongeza Maswi.
“Mimi sichukui rushwa, sasa mtu anaokota
vikaratasi vya kufungia vitumbua, anakwenda kutoa tuhuma
zake…Alipomaliza kutoa tuhuma zake ndani ya Bunge nilimpigia simu
nikamwambia kama yeye ni mwanaume, azungumze akiwa nje ya Bunge na siyo
kutegemea kinga ya Bunge.
“Na akisema nje ya Bunge nampeleka mahakamani
akathibitishe madai yake…Kwanza yuko mkononi, mwenzake (jina
linahifadhiwa) hachangii tena hoja kwenye Wizara ya Nishati, nina tuhuma
zake za kuhongwa,” alisema Maswi.
Maswi alikuwa akizungumzia tuhuma zilizoibuliwa
bungeni na Kafulila akiwahusisha mawaziri wawili na Sh200 bilioni
zilizochotwa kwenye akaunti ya Escrow, iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja
kati ya Tanesco na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.
Akiomba mwongozo wa Spika bungeni jana, alisema
wakati akichangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini, Spika Anne Makinda alielekeza kuwa apeleleke ushahidi wa ufisadi
huo mezani kwake ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Alisema waliwasilisha ushahidi huo yeye na Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, mezani kwa Spika lakini hadi leo
hawajui aliupeleka wapi zaidi ya kuambiwa kwamba Waziri (hakumtaja)
anautumia kukosoa.
“Mwenendo wa jambo hili tangu ulipoanza na wakati
wa hotuba ya Waziri Mkuu na baadaye Wizara ya Nishati na Madini linaleta
shaka kuhusu dhamira ya kiti kulishughulikia na limekuwa likihatarisha
maisha yangu na wengine,” alisema.
Alisema juzi akiwa bungeni Werema alionyesha kusudio la kutaka kumpiga na baadaye nje ya Bunge alitangaza kukitoa kichwa chake.
“Nasimama hapa kuwaeleza wananchi wa jimbo langu,
kitakapotokea kitu chochote kwangu muhusika wa kwanza atakuwa yeye
kwasababu ya kauli hiyo ya kusema kuwa atachukua kichwa changu,”
alisema.
Kafulila alitaka kufahamu Spika Makinda analitolea uamuzi gani ili kusudi liweze kufikia mwisho.
Akijibu Spika Makinda, alisema alimwandikia barua lakini kabla
ya kuiona, akalisikia jambo hilo katika vyombo vya habari, “Hizo ni
adabu hizo? Siyo adabu.”
Alisema suala hilo limeshatolewa uamuzi kamili
kwasababu limeshapelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ma-document (nyaraka zako zote zinakwenda huko,
ulitegemea sisi tufanye hukumu hapa? Ndivyo tunavyofanya? Hata ulipoleta
(suala hilo) juzi mimi nilikushangaa sana,” alisema.
Alisema Kafulia wapo naye katika Umoja wa Mabunge
Duniani (IPU) na kumsifia kuwa ni mmoja wa vijana hodari lakini kwa
jambo hilo ameona (Spika) hajalishughulikia vyema.
“Sasa tunaanza kupata mashaka ni suala la kawaida
ama siyo la kawaida? Nataka kukwambia kuwa suala hili liko kwa CAG na
Takukuru sasa hivi,” alisema na kumtaka kuendelea kupeleka nyaraka za
ushahidi hukohuko.
Kuhusu usalama, Makinda alisema: “Wewe umemchokoza
na yeye akachokozeka, mnapotumia lugha mbaya mjue kuwa kila mtu ni
binadamu. Tulieni suala la IPTL lina utaratibu wake.”
Alisema hakuna namna nyingine zaidi ya kupeleka nyaraka hizo kwa CAG na Takukuru.
“Sasa mnakaa mnatusambazia makaratasi haya sisi
tufanye nini. Jambo ambalo mtu anajua lina tatizo anakuwa na utulivu.
Kama unajiamini unakuwa na utulivu. Kama hujiamini unakuwa hauna
utulivu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Maswi, Kafulila
alisema ameshazungumza jambo hilo nje ya bunge na kwamba hana hofu
yoyote kwa kuwa anauhakika taarifa anazozisema ni sahihi.
Kuhusu yeye kutumiwa na Mbunge wa Musoma Vijijini
kuwatuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na
Katibu Mkuu wake Maswi, alisema hakuna jambo hilo siyo la kweli.
“Juzi tulikutana na waandishi na nilitaka akaunti
ya Kampuni ya Uwakili ya Mkono (Mkono & Co. Advocates) ichunguzwe.
Itakuwaje mtu huyo huyo anipe documents (nyaraka)?” alihoji Kafulila.
Alisema kinafanyika sasa ni dalili zinazoonyesha
kuwa viongozi hao wameanza kutapataka kwa kuwa wanafahamu malipo hayo
hayakufanywa kwa njia halali.
“Huko ni kutapatapa hoja hapa ni Sh200 bilioni zilizochukuliwa. Naamini watachukuliwa hatua,” aliongeza.
“Huko ni kutapatapa hoja hapa ni Sh200 bilioni zilizochukuliwa. Naamini watachukuliwa hatua,” aliongeza.
Katika tuhuma zake Kafulila, alimuunganisha pia
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini na vigogo wengine, wakiwamo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na
Serikali, wote akiwataja tu kwa vyeo bila majina.
Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na
Madini, Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco). Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni
Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara
hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Kafulila alitoa tuhuma hizo bungeni alipokuwa
akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri
Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2014/15.
No comments:
Post a Comment