Tuesday, June 3, 2014

MSIBA WA TYSON WAMALIZA BIFU LA WEMA NA KAJALA

AMA kweli kufa kufaana! Lile bifu zito lililokuwa likitokota kati ya wapendwa wawili, Miss Tanzania 2006/07, Wema Isaac Sepetu na mwigizaji mwenzake wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja limekwisha kufuatia kukalishwa katika kikao cha siri  kilichofanyika kwenye msiba wa aliyekuwa mwogoza filamu mahiri nchini, marehemu George Otieno ‘Tyson’, Risasi Mchanganyiko limeinasa.

 Wema Isaac Sepetu na mwigizaji mwenzake wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja wakiwa pamoja katika hali ya kupatana.

Kwa mujibu wa chanzo makini, upatanishi huo ulitokea baada ya wote wawili kufika kila mmoja kwa wakati wake kwenye msiba huo nyumbani kwa marehemu, Makonde, Mbezi-Baech jijini Dar.
Kabla ya kikao hicho, ‘maadui’ hao kila mmoja alionesha kuwa kivyake huku wapambe wakiwaongoza kwenye ‘kambi’ mbalimbali ili wasikutane.
Ilidaiwa kwamba kufuatia hali hiyo, ndipo baadhi ya mastaa waliamua kujikusanya na kujadili namna ya kuwapatanisha wawili hao huku wakiona kwenye msiba huo ndiyo mahali mwafaka kwa vile wote wapo.
MUDA WA KIKAO
Chanzo kilidai kwamba, kikao cha kuwapatanisha Wema na Kajala kilichukua muda wa saa mbili, kwa maana ya dakika 120 huku kikifanywa kuwa siri nzito ambayo haikutakiwa kufika kwenye vyombo vya habari.

 Kajala Masanja

 WAJUMBE WA UPATANISHI
Kwa mujibu wa chanzo hicho, wajumbe wasiopungua nane walishiriki kuwaweka chini maadui hao na kusikiliza hoja zao kabla ya kupatanishwa.
“Kikao kilikuwa kizito kidogo, kilianza usiku mwingi, lakini kiliisha salama.
“Kajala alionesha ugumu wa kukubali kupatana kuliko mwenzake (Wema) lakini wajumbe walikuwa ngangari.
“Wajumbe waliokuwepo ambao wote ni watu wa filamu ni Single Mtambalike ‘Richie’, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Hartmann Mbilinyi, Vincent Kigosi ‘Ray’, John Lista na mwingine alliyetambulika kwa jina moja la Lamatha,” kilisema chanzo chetu kwa kujiamini.
BAADA YA USULUHISHI
Chanzo kilisema kuwa baada ya kumaliza upatanishi huo, wawili hao walibaki wenyewe ambapo waliongea mambo mbalimbali kuhusu maisha kwa sasa.
“Kusema ule ukweli hawa watu wamepatana kweli, wala si sinema. Hata baada ya usuluhishi, waliachwa wenyewe ambapo walizungumza mambo yao,” kilisema chanzo hicho.


 Wema Isaac Sepetu katika pozi.


HISTORIA YA BIFU
Machi 25, 2013, Kajala alihukumiwa kwenda jela miaka mitano kufuatia kesi yake ya kuuza nyumba iliyowekewa zuio halali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).
Kesi hiyo ilihukumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar ambapo Wema alimlipia Kajala faini ya shilingi milioni 13 na kumfanya mshitakiwa huyo kuwa huru.
Baada ya hapo, wawili hao wakawa marafiki wakubwa huku Kajala akifanya kazi ya ukatibu kwenye ofisi ya Wema ya Endless Fame Production, Mwananyamala jijini Dar (kabla haijafungwa).
BIFU
Haikujulikana mara moja nini kilitokea, lakini ghafla wawili hao wakawa maadui. Madai ya chanzo yalisema bifu lao lilitokana na kitendo cha Kajala kumchukua ‘bwana’ wa mwenzake anayejulikana kwa jina la CK au kigogo wa ikulu.
Huyo kigogo wa ikulu, awali alikuwa mpenzi wa Wema na Kajala kuwa shemeji yake ‘automatiki’.
Chanzo kingine kilisema bifu lao lilitokana na kitendo cha Wema kuhamishia ushoga kwa staa mwingine wa filamu, Aunt Ezekiel hivyo kumfanya Kajala kuwa ‘wazamani’.
UKWELI WA BIFU
Hata hivyo, ukweli wa kuwepo kwa bifu lao ulijitokeza siku moja Kinondoni jijini Dar ambapo Wema alikuwa saluni, Kajala naye akafika, Wema alitoka ili kumkumbatia lakini Kajala akamkwepa na kumwambia atamchafua.
Inadaiwa Wema alikasirika na kumtukana Kajala hali iliyokoleza bifu lao ambalo awali lilikuwa chini kwa chini. Ilidaiwa siku hiyo Wema aliamua kutumia nafasi hiyo ya kukumbatiana ili kuondoa minong’ono ya siku nyingi kwamba wana bifu.
Hata hivyo, katika mahojiano maalum na mwandishi wetu, Wema alikiri kuhusu Kajala kumkwepa lakini akaongeza kuwa, bifu lao liliungwa mchuzi kufuatia kitendo cha Kajala kumsema vibaya kuhusu fedha zake.
Wema alisema kuna wakati walikwenda Arusha kwenye shoo iliyoandaliwa na kampuni yake, yeye akawa na uhutaji wa fedha ambapo alimuomba Kajala.
Alisema licha ya kumkopesha ikiwa imepungua kidogo, lakini Kajala alimwita mdogo wake mmoja na kumpa fedha nyingine akimwelekeza akaziweke benki kwa vile anahisi Wema atazimaliza.
SHUTUMA HADHARANI
Kuanzia hapo, Wema na Kajala walikuwa wakiropokeana kwenye vyombo vya habari. Kuna siku Wema alidiriki kutoa tamko kwamba, kwa hali ilivyo anajuta hata kumtolea zile shilingi milioni 13. Akasema angejua angemwacha akafungwe jela.
Habari hiyo iliandikwa na Gazeti la Ijumaa la Aprili 25, mwaka huu ikiwa na habari yenye kichwa; NAJUTA KUMLIPIA KAJALA MIL. 13!
WADAU WASHUKURU
Tukirudi kwenye chanzo, kilisema wadau waliosikia kupatana kwa wawili hao ndani ya msiba wa Tyson walishukuru wakiwaombea kwa Mungu awape uzima.
KUHUSU MWILI WA TYSON
Kwa upande mwingine, mwili wa George Tyson uliagwa jana kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar na kusafirishwa kwa ndege kwenda nchini Kenya kwa mazishi.

No comments:

Post a Comment