Mchungaji wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of God City Centre jijini hapa, Michael Kulola.
MH! Mchungaji wa Kanisa la Evangelist Assemblies Of God
City Centre jijini Mwanza, Michael Kulola ametiwa mbaroni kisha
kufikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza kisa
wizi wa fedha za rambirambi za Askofu Moses Kulola kiasi cha Sh. milioni
33.
Picha ya marehemu Askofu Moses Kulola enzi za uhai wake.
Habari zilidai kuwa baada ya kuwekwa nyuma ya nondo, mchungaji huyo
alifikishwa mahakamani hapo mwishoni mwa wiki iliyopita na kusomewa
shitaka la wizi wa fedha hizo, mali ya mke wa marehemu Kulola, Elizabeth
Kulola ambapo wakili wa serikali, Castuce Ndamugoba, mbele ya Hakimu
Mfawidhi, Angelo Rumisha alimsomea shitaka lake.
Ndamugoba aliiambia mahakama kuwa mchungaji Michael anashitakiwa kwa
kosa la wizi wa fedha hizo chini ya vifungu vya 258 (i) na 265 vya
sheria ya kanuni ya makosa ya adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Alisema, huku akifahamu ni kosa na kinyume cha sheria, mshitakiwa
alidaiwa kutenda kosa hilo kutoka kwenye akaunti namba 0061016209 mali
ya Elizabeth Kulola katika Benki ya FMBE iliyopo Barabara ya Station.
Wakili huyo alidai mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Septemba
20, mwaka jana na Januari 21, mwaka huu.Baada ya kusomewa mashitaka,
mchungaji huyo alikana ambapo wakili wake, Deocless Rutahindurwa wa
kampuni ya uwakili ya Rwelu aliiomba mahakama impe mteja wake dhamana
ambayo aliambiwa ipo wazi.
Hata hivyo, Rumisha alisema kutokana na wingi wa fedha hizo,
mshitakiwa atatakiwa kuweka dhamana kwa ya Sh. milioni 16.5 au wadhamini
wawili wanaofahamika na wenye mali isiyohamishika.
Wadhamini hao walitimiza masharti kwa kuweka hati za nyumba, wanasubiri kesi kutajwa tena.
No comments:
Post a Comment