Wednesday, June 18, 2014

MALIMWENGU: MNGONI ALIYEPOTEA AIBUKA AKIWA MMASAI

Maajabu ya karne! Mtoto aliyezaliwa na wazazi wa kabila la Kingoni (Mngoni), Samson Matei Joseph wa Nguruka Kata ya Nguruma wilayani Uvinza mkoani Kigoma alipotea miaka miwili iliyopita lakini katika hali ya kushangaza, hivi karibuni ameibuka akiwa ni Mmasai baada ya kusakwa bila mafanikio.

 Mtoto aliyezaliwa na wazazi wa kabila la Kingoni (Mngoni), Samson Matei Joseph wa Nguruka Kata ya Nguruma wilayani Uvinza mkoani Kigoma aliyepotea miaka miwili iliyopita na kupatikana akiwa Mmasai.


Akizungumza na waandishi wetu kwa njia ya simu akiwa mkoani Kigoma, baba mzazi wa mtoto huyo, Matei Joseph alisimulia mkasa mzima na kusema kuwa yeye na mkewe walimpoteza mtoto wao huyo Desemba 16, 2012 wakati huo akiwa na umri wa miaka 11, akisoma darasa la tatu.
Alisema kuwa baada ya kupotea walimsaka kila kona ya nchi bila  mafanikio na kuamua kumuachia Mungu.
“Siku moja niliona simu yangu ya mkononi ikiita kwa namba ngeni, nilipopokea kuna bibi kajitambulisha kwa jina la Mama Vero akasema kuna mtoto anataka kuongea na mimi.
“Alimpatia simu mtoto ambaye alijitambulisha kuwa yeye ni Samson, nilifurahi na kushangaa lakini pia sikuamini kwani alikuwa akiongea Kimasai!” alisema Matei.

 Mtoto Samson Matei Joseph akiwa na baba yake mzazi, Bw. Matei Joseph.

 Matei alisema mwanaye huyo alimwambia kuwa alikuwa Chalinze mkoani Pwani akihitaji msaada, akilalamika kuteswa kwa muda mrefu na Wamasai ambao ndiyo waliomtorosha.
“Nilifunga safari hadi Chalinze na kukuta kweli ni Samson, lakini alikuwa katika muonekano wa Kimasai kwani aling’olewa meno nane kama mila zao zinavyosema,” alisema Matei.
Aliendelea kusimulia kwamba alipomhoji mwanaye alidai alichukuliwa na Mmasai aliyemtaja kwa jina moja la Samson ambaye alikuwa akiuza dawa na pipi mkoani Kigoma kabla ya kumuiba na kutimkia naye Chalinze.
“Nilishangaa kusikia alichukuliwa na Mmasai niliyekuwa namjua ambaye alikuwa akifanya biashara pale Nguruka huku Kigoma.
“Alimrubuni mwanangu kuwa anakwenda kufanya kazi dukani kwa mama Yoyoo, kumbe ni kuchunga ng’ombe na mabwawa ya maji,” alisema Matei.
Baada ya kupata habari kamili, Matei alikwenda Kituo cha Polisi cha Nguruka na kutoa taarifa ambapo alifungua jalada la kesi namba NGK/IR/2022/2014- KUTOROSHA MTOTO.
“Baada ya kuchukua RB niliambiwa nifanye juu chini nikamfuate mwanangu Chalinze kisha nimtafute Nasoro kwa ajili ya kumfungulia kesi ya kujibu.
“Kweli nilifanya hivyo, tulipomkamata Nasoro hakuwa na la kujibu, nikamchukua mwanangu nikarudi naye Kigoma,” alisema Matei.
Kwa upande wake mtoto Samson alisema kuwa alikuwa amewekwa kwenye mapori ya Milima Mitatu Chalinze Kata ya Vizimbwi ambapo alikuwa akichunga ng’ombe na mabwawa ya maji.
Alisema alifanikiwa kutoroka baada ya kuua sungura na kuwauzia Wamasai wengine ambapo alipata fedha ndipo akakutana na Mama Vero ambaye alimnunulia vocha akawapigia wazazi wake kwa kuwa alikuwa akikumbuka namba zao kichwani.

No comments:

Post a Comment