Sunday, June 1, 2014

Magereza 12 hayafai kwa matumizi ya binadamu



Dar es Salaam. Wakati mamilioni ya fedha za Watanzania yakipotea kila mwaka kutokana na ufisadi na misamaha ya kodi, imebainika kuwa baadhi ya magereza nchini hayafai kutumiwa na wafungwa kutokana na kukosa sifa ukiwemo uchakavu wa majengo.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwenye magereza na vituo vya polisi 102 katika mikoa 12, inaeleza kuwa magereza 12 hayafai kutumiwa na binadamu.
Hali hiyo inaamanisha kwamba magereza hayo siyo tu ni hatari kwa wafungwa na mahabusu, bali pia kiwa watumishi wa Idara ya Magereza. Ripoti hiyo inaweka bayana kuwa magereza hayo yana hali mbaya kutokana na majengo yake kujengwa miaka mingi iliyopita, huku mengine yakikabiliwa na ukosefu wa mwanga wa kutosha.
Magereza yaliyotajwa kukosa sifa za kutumiwa na binadamu ni Rombo, Nzega, Geita, Ngudu, Kasungamile, Ukerewe, Mugumu, Musoma, Bunda, Ushora, Mang’ola na Bariadi.
“Hali kwenye haya magereza ni kinyume na Kanuni namba 10 ya Umoja wa Mataifa, inayozungumzia namna ya kuwahifadhi wafungwa ambayo inataka sehemu za kulala zikidhi vigezo vya kiafya, hali ya hewa, nafasi ya kutosha, joto na mwanga wa kutosha,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Utafiti huo uliokuwa ukiangalia hali za watoto magerezani kwa mwaka 2012/2013 unaeleza kuwa maboresho ya majengo ya magereza yaliyochakaa ni jambo ninalohitaji kupewa kipaumbele katika mpango endelevu wa kuboresha magereza nchini.
Hata hivyo, taarifa hiyo imeyamwagia sifa magereza ya Igunga, Kahama, Arusha, Karanga, Handeni, Singida, Kiomboi, Shinyanga, Uyui na Butimba kuwa yanapitisha mwanga na hewa ya kutosha kwa wafungwa na mahabusu. Imebainisha namna wafungwa watoto walivyokuwa wakipigwa, kutishwa na kuzuiwa kutembelewa na ndugu zao kama sehemu ya adhabu.
Asilimia 55 ya watoto waliohojiwa walisema walipewa adhabu mbalimbali, ambapo magereza yaliyoyajwa kutekeleza vitendo hivyo ni Mugumu, Sengerema, Butimba, Lushoto, Tanga, Karanga, Tukuyu, Ngudu na Rombo. Kuhusu utolewaji wa elimu ndani ya magereza, ripoti hiyo inabainisha kuwa asilimia 51.6 ya watumishi wa magereza waliohojiwa walisema hakuna programu yoyote ya elimu.
“Kanuni namba 38 ya Umoja wa Mataifa inayohusu ulinzi wa watoto inasema kuwa, kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anatakiwa kuwa kwenye darasa la umri wake,” inasema.
Mchambuzi wa Sera wa Shirika la Haki Elimu, Boniventura Godfrey akizungumzia ripoti hiyo alisema Katiba inatoa haki ya elimu kwa mtoto kuwa ni lazima na siyo hiari.
“Mtoto anatakiwa apate elimu, hata akiwa gerezani kwa sababu kosa alilolifanya halina uhusiano na kupata elimu,” alisema.
Mkazi wa Mtoni Kijichi, wilayani Temeke, Rehema Kyaruzi alipohojiwa kuhusu ripoti hiyo, alisema Serikali inapaswa kuwaruhusu watoto wanaofanya makosa madogo kutumikia adhabu zao nyumbani. Alisema anaamini iwapo watoto hawatapewa nafasi ya kushiriki kwenye masomo au michezo wanaweza kuathirika kisaikolojia na kiafya.
“Hakuna mzazi hata mmoja anaweza kutamani mtoto wake apelekwe gerezani.Hilo jambo linaumiza sana, lakini ikitokea, hakuna namna zaidi ya kulipokea bila kulikubali,” alisema.

No comments:

Post a Comment