Sunday, June 1, 2014

NI UJUHA KUSHANGILIA USHINDI WA MUTHARIKA WA MALAWI..... SIO RAFIKI WA TANZANIA

Rais mpya wa Malawi, Prof. Arthur Peter Mutharika

Watu wengi wanampongeza rais mpya wa Malawi Prof. Arthur Peter Mutharika kwa kutangazwa rasmi na tume ya uchaguzi ya Malawi baada ya vuta nikuvute ya siku kadhaa. Mutharika anaingia kushikilia nafasi inayoachwa na rais Joyce Banda baada ya kutumikia kwa miaka miwili kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa rais wa tatu wa nchi hiyo Dr. bingu wa Mutharika, mwezi April 2012.
Wapo wanaoshangilia ushindi wa Prof. Mutharika kwa imani kwamba ni ushindi wa wapinzani wa Malawi hivyo ni tochi ya kwa vyama vya upinzani vinavyopambana kuviondoa vyama tawala vya Afika. Ukweli ni kwamba, Chama cha Mutharika kiliondoka madarakani miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha kiongozi wao. Mfumo mzima wa utawala ulikuwa chini influence ya chama cha kina Mutharika ambao kama ilivyo kawaida ya vyama vya Afika vilivyo madarakani kujiwekea mizizi ili isiwe rahisi kung'oka madarakani kwa njia yoyote.
Kipindi ambacho marehemu Bingu wa Mutharika akiwa madarakani aliweka mipango ya kumrithisha kiti cha urais mdogo wake ambaye ndiye rais anayeingia madarakani sasa, mpango huo ulipingwa vibaya na baadhi ya wanachama na viongozi wa juu wa chama hicho akiwemo makamu wake wa rais Joyce Banda. Kitendo hicho kilipelekea rais Bingu kuwatimua uanachama baadhi ya wanachama waliokaidi mapendekezo yake, baada ya kutimuliwa uanachama Joyce Banda hakuwa na uhusiano mzuri na Bingu hivyo kukosa baraka za kikazi hali iliyomfanya kuhamishia ofisi katika makazi yake binafsi na hatimaye kuanzisha chama chake cha PP akiwa pamoja na baadhi ya wale ambao walitimuliwa kutoka katika serikali ya Bingu.
Joyce Banda aliendelea kushikilia wadhifa wa makamu wa rais kwa kuwa ni wadhifa wa kikatiba hivyo Bingu hakuwa na mamlaka kikatiba kumtimua katika nafasi hiyo, hivyo aliendelea kuwa makamu wa rais asiyekuwa na mawasiliano na rais wala watendaji wengine serikalini, alibaki mpweke licha ya kuwa na ulinzi na kupata kila kinachomstahili kwa mujibu wa sheria.


Baada ya kifo cha ghafla cha Bingu, ukawekwa mpango wa kumchinjia baharini Joyce Banda asiwe rais kwa mujibu wa katiba badala yake Peter Mutharika akawa anapanga na wasaidizi wake wamuapishe kimya kimya kuwa rais wa Malawi kitendo ambacho kilipingwa vibaya na mkuu wa majeshi wa Malawi na hatimaye spika wa Bunge alitangaza rasmi kwa mujibu wa katiba rais ni Joyce Banda na siku iliyofuata aliapishwa rasmi kuwa rais wa Malawi kumalizia kipindi cha marehemu Bingu wa Mutharika.
Hapa ni lazima tutambue kwamba chama kilichokuwa madarakani wakati huo kilikuwa kimekamata mfumo mzima wa utawala kuanzia usalama wa taifa mpaka watendaji serikalini hivyo kilichofanyika ndani ya miaka miwili hii ni kujipanga tu na kusubiri wakati. Pia cham cha PP cha Joyce Banda kilikuwa kidogo nah hakina nguvu hivyo ilikuwa ni rahisi sana kukiyumbisha na kukitengenezea kashfa nyingi kikiwa madarakani na hivyo kukichafua.
Kwa maana hiyo ushindi waMutharika umetokana na mikakati ya kimtandao na kijasusi hivyo hatuwezi kuita ni ushindi wa upinzani dhidi ya chama tawala.

No comments:

Post a Comment