Monday, June 23, 2014

BABU SEYA NA MWANAWE PAPII KOCHA WATIMIZA MIAKA KUMI GEREZANI

MASKINI! Wakati wakitimiza miaka 10 gerezani tangu walipohukumiwa Juni 25, 2004, mwanamuziki nguli wa dansi Bongo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wametoa watu machozi kwa mara nyingine.

 Kwa pamoja wanamuziki nguli wa dansi Bongo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wakitumbuiza.

 Wakitumbuiza na kukumbushia enzi zao mwishoni wiki iliyopita kwenye sherehe ya siku ya magereza nchini iliyofanyika katika Chuo cha Maofisa Magereza, Ukonga, Dar, wanamuziki hao walitoa burudani ya kihistoria mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, kamishna wa magereza nchini, John Minja na mkuu wa magereza wa Namibia, Raphael Tuhafeni Hamunyela.

 Mwanamuziki nguli wa dansi Bongo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ akilirindimisha gitaa la solo.

 BABU SEYA, PAPII WAHUZUNISHA
Wanamuziki hao ambao wanatumikia kifugo cha maisha, waliimba wimbo ambao uliwahuzunisha wengi kutokana na ujumbe uliomo katika mashairi hayo.
Sehemu ya mashairi hayo ilisema: ’’Magereza si sehemu ya mateso bali ni sehemu ya kujifunza na kurekebishwa, JK tusamehe, tumejirekebisha, mgeni rasmi (Chikawe) tuombee kwa rais atupe uhuru wafungwa wote tumejifunza, hata Petro alimkana Yesu mara tatu lakini alisamehewa sembuse sisi kwani ni kipi tulichokosa sisi?’’

 ...Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ naye akifanya yake.

 MIAKA 10 GEREZANI
Juni 25, 2004 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, iliwatia hatiani Babu Seya na wanaye Papii, Nguza Mbangu na Francis Nguza kwa kupatikana na hatia ya ubakaji na unajisi wa watoto.
Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya ambaye aliwatia hatiani kwa makosa yote waliyokuwa wameshitakiwa nayo.

 Mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe aliyehudhuria maadhimisho ya siku ya magereza.

 Jaji Mstaafu, Mihayo, Septemba 15, 2011 aliwahi kunukuliwa akikanusha  uvumi ulioenea kuwa, kiongozi mmoja mkubwa wa serikali aliwashinikiza majaji ili watoe hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na wanaye.
“Hakika si kweli…Niliupitia mwenendo wa kesi hiyo na kubaini kwamba kilichokuwa kinasemwa mitaani kilikuwa ni uvumi usiokuwa na chembe ya ukweli,” alisema Jaji Mihayo alipokuwa akizindua rasmi Ripoti ya Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari vya Magazeti (Julai 2010-Juni 2011) ya Baraza la Habari la Tanzania (MCT) jijini Dar.

 ...Askari wakipiga gwaride kama sehemu ya maadhimisho hayo.

 Alisema aliusoma kwa kina mwenendo wa kesi ya kulawiti dhidi ya Babu Seya na wanawe kama ulivyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kabla ya kutoa hukumu ya mwisho.
Alisema kwa kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kuamua kuhusiana na shauri hilo, ilipokea ukweli wa mwanzo wa shauri hilo na ikauwasilisha Mahakama Kuu.
Alisema wakati akizisoma nyaraka na mwenendo wa kesi kutoka katika mahakama hiyo ya chini (Mahakama ya Kisutu), aligundua kwamba kilichokuwa kikisemwa na watu mitaani ulikuwa ni uvumi tu.
Jaji Mihayo alisema alitenga muda wa kuongea na watoto waliodaiwa kubakwa na Babu Seya na wanaye na akagundua kwamba watoto hao walikuwa wamelawitiwa na kwamba tendo hilo lilikuwa limefanywa kwa kipindi cha miezi kadhaa.
Alisema aliwasikiliza watoto hao na akapata picha kamili ya kilichoendelea katika matukio hayo na pia aligundua kwamba wazazi wa watoto hao hawakuwa wanajua mwenendo wa watoto wao.
Alifafanua kwamba baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikitoa ripoti isiyo sahihi ya kesi hiyo na akasema kwamba kama waandishi wangefanya uandishi wa kiuchunguzi, wangeweza kupata ukweli wa tukio hilo.
Hata hivyo, baada ya kesi yao kusimamiwa na  wakili Mabere Marando, jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa lililokuwa na majaji Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Massati katika hukumu yao iliyotolewa Februari 2010, mahakama hiyo iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na mwanaye, Papii huku ikiwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya, Mbangu, na Francis.
Oktoba 30, mwaka jana, Mahakama ya Rufaa iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati walisikiliza hoja za pande zote kuhusu ombi la kufanyika marejeo ya uamuzi wa awali wa mahakama hiyo.
Mahakama hiyo baada ya kufanya mapitio iliendelea kuwaona warufani hao wawili kuwa na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu yao.
Juu ya vilio vya wanamuziki hao kuomba rais kuwaachia huru, Marando alisema rais ni mtu mkubwa hivyo anaweza kusikiliza vilio vyao.
Ilidaiwa kuwa watoto hao walifanyiwa vitendo hivyo kati ya Aprili na Oktoba 2003 maeneo ya Sinza Kwaremmy, Dar.

No comments:

Post a Comment