Friday, June 13, 2014

Al Shabaab yataka wanawake kuvaa Niqab

Al shabaab

Wanamgambo wa Al-shabaab nchini Somalia wamewakamata takriban wanawake mia moja na kuwaaamuru kuvalia mavazi yanayostahili kwa wanawake wa kiislamu kuambatana na sheria za dini hiyo la sivyo wapate kichapo.
Wanawake hao walikamatwa sokoni katika eneo la Buala karibia kilomita mia tatu Kusini-Magharibi mwa Mogadishu.
Mwandishi wa BBC nchini humo Mohamed Mohamed anasema ni nadra kwa Al-shabaab kuwakamata watu wengi kwa wakati mmoja kama hivyo.
Baadhi ya wanawake hujifunika gubigubi kutoka kichwani hadi miguuni
Wanawake hao walikamatwa wakiwa sokoni na kupewa onyo kabla ya kuachiliwa huru.
Hawakuadhibiwa kwa sababu lilikuwa kosa lao la kwanza lakini walionywa kuwa watachapwa hadharani ikiwa wangepatikana na kosa hilo kwa mara nyingine.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa wanawake hao walivalia mavazi mapesi na kukosa kujifunika nyuso zao kutokana na joto kali
Wanawake hao waliamrishwa kuvaa Niqab,vazi linalowafunika mwili mzima huku sehemu ndogo ya uso ikiachwa nje ili kuwawezesha kuona.
Jina al shabaab linalo maanisha "vijana" kwa kiarabu,linapigania mfumo wa kiislamu wa wahhabi saudia.
Watu ambao washawahi kupatikana na kosa la Zinaa wamepigwa mawe hadi kufa na wezi kukatwa mikono.
Serikali ya Somalia inayofadhiliwa na umoja wa mataifa,ikisaidiwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika, imefaulu kutimua Al-shabaab nje ya miji mikubwa nchini humo lakini kundi hilo bado linaendelea kutekeleza mashambulizi huko.

No comments:

Post a Comment