Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wizara ya
Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi amefariki dunia jana alipokuwa
amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
matibabu ya Kansa ya Ini.
Mwakapugi ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa
miaka 64, alitumikia taifa kwa miaka 30 mfululizo kabla ya kufikwa na
umauti usiku wa kuamkia jana saa 3:45 ikiwa ni wiki moja tangu
aliporejeshwa kutoka India kwa matibabu zaidi.
Hayo yalizungumzwa jana na msemaji wa familia,
Mathias Mwambona wakati wa mazungumza na waandishi wa gazeti hili
-nyumbani kwa marehemu huku akifafanua juhudi zilizofanyika bila
mafanikio tangu alipoanza kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya ini.
Mwambona alisema marehemu Mwakapugi ambaye ameacha mjane na watoto
wawili, kabla ya umauti wake alianza kusumbuliwa na ugonjwa huo miezi
sita iliyopita kupitia maumivu ya tumbo yaliyomsumbua.
“Ndugu waliamua kumpeleka hospitali mbalimbali
kupima bila matokeo yoyote, lakini baadaye alipimwa tena Muhimbili
ambako madaktari walithibitisha kuwa na ugonjwa wa kansa ya ini,”
alisema Mwambona na kuongeza:
“Mwezi huu tukaamua kumpeleka India ambako
tulielezwa tayari kansa ilikuwa imeshafikia ‘stage four’(isiyoweza
kutibika tena), alikaa huko akitumia huduma ya mionzi(Chemotherapy)
kabla ya kumrejesha Aga Khan Jumamosi iliyopita.”
Utumishi wake serikalini
Marehemu Mwakapugi aliyeacha mjane na watoto
wawili, alitumikia nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo Shirika la
Viwango nchini(NBS), Mkurugenzi wa Tume ya Mipango 1999 mpaka 2006 kabla
ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini tangu
mwaka 2006 mpaka 2010.
Baada ya kustaafu mwaka 2010, marehemu Mwakapugu
aliendelea kufanyakazi katika taasisi nyingine zinazojihusisha na
masuala ya kiuchumi kupitia Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa
Umaskini(Repoa).
Mwili kuagwa leo
Katika hatua nyingine Mwambona alieleza utaratibu
wa kuaagwa mwili wa marehemu leo nyumbani kwake eneo la Mikocheni B,
Kinondoni jijini Dar es Salaam huku ndugu, jamaa na viongozi
wakitarajiwa kushiriki katika tukio kwa ajili ya kuaga kwa mara ya
mwisho.
Baada ya tukio hilo, mwili utasafirishwa kwenda kuhifadhiwa kijijini kwao Ilundo, iliyopo Wilaya ya Tukuyu mkoani Mbeya.
“Leo jioni tutaanza na ibada na kisha kuuaga mwili
wa marehemu halafu kesho ndiyo tutausafirisha kwenda kijijini,” alisema
Mwambona ambaye ni mjomba wa marehemu.
Mwandosya amlilia
Mwandosya amlilia
Akionyesha masikitiko yake, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya alisema katika kipindi cha
miaka 30 wakati wa utumishi wake, Mwakapugi alitimiza wajibu wake huku
akionyesha mchango mkubwa zaidi hata baada ya kustaafu.
“Taifa lilianza kumtegemea tangu utawala wa hayati
Mwalimu Julius Nyerere katika mikutano ya kimataifa, na Umoja wa
Mataifa iliyohusiana na masuala ya uchumi,” alisema na kuongeza:
“Lakini hata baada ya kustaafu bado aliendelea
kujihusisha na uandishi wa vitabu vya uchumi, akafanya kazi kwenye
Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini(Repoa), lengo lake likiwa ni
kuendelea kuisaidia jamii ya Watanzania.”
Mtoto wake amlilia
Katika hatua nyingine, mtoto wa marehemu
Mwakapugi, Margareth Mwakapugi alionyesha hisia zake za majonzi huku
akieleza kumbukumbu pekee atayoendelea kuitumia kama ngao aliyomwachiwa
baba yake.
No comments:
Post a Comment