Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendegu,
Hakika cheo ni dhamana, hivyo ni muhimu kwa wenye dhamana hiyo
kujitambua na kuonyesha wanavyoweza kubeba dhamana hiyo kwa jamii
husika.
Halima Dendegu, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya
Tanga, mkoani Tanga anaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kuonyesha
alivyobeba dhamana hiyo ya kuiongoza wilaya kutokana na kugeukia kundi
la vijana wilayani kwake akidhamiria kuwakomboa.
Dendegu aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Mei
mwaka 2012 kuwa mkuu wa wilaya hiyo anaeleza kuwa baada ya kuingia
wilayani humo alifanya utafiti na kubaini kundi kubwa la vijana
likijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu mbalimbali.
“Nilianza kubaini vijiwe vingi vya vijana na
hawana ajira, nilipofuatilia zaidi niligundua wengi wametumbukia katika
matumizi ya dawa za kulevya,”anasema Dendegu na kuongeza:
“Nilibaini vijana 867 wavulana na wasichana, walioathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya.”
Anabainisha kuwa baada ya kuwahoji vijana hao
walitoa sababu mbalimbali za kujiingiza kwenye dawa za kulevya ikiwamo
kukosa ajira, makundi na kukata tama.
“Wengine walisema walishawishiwa, wapo waliosema
kiingiacho mjini siyo haramu, waliokuwa wakiuza dawa hizo, hata
walioshindwa kutimiza malengo yao maishani,” anasema Dendegu.
Anaongeza: “Kwa sababu hiyo, nimeanzisha kituo ili
kuwatibu, kimeanza na vijana 150 na 78 kati yao wameanza matibabu
wakiwamo wasichana 28.”
Anabainisha kwamba kwa kuwa lengo lake ni
kuwaepusha wasirudi kwenye dawa za kulevya katika kituo hicho ameanzisha
pia utoaji elimu ya ujasiriamali.
“Tayari tumebabini wenye vipaji mbalimbali, wapo
wapenda mpira wa miguu, watengenezaji sabuni hata wasanii wa muziki wa
kizazi kipya.”
Anasema kuwa ili kuwajenga zaidi kiafya na
kuanikiza vipaji vyao, kila Jumamosi huandaliwa bonanza linaloendana na
michezo mbalimbali.
“Pia nimeanzisha michuano ya mpira ‘Dendegu Cup’
litazinduliwa Juni mwaka huu ili kuibua vipaji zaidi, naamini tutatoa
vijana wa kucheza timu kubwa,”anasema akidokeza kuwa hata yeye anapenda
na kucheza mpira wa pete, volleyball, pia kuimba.
Anasema kuwa katika tamasha hilo la uzinduzi vijana
watafundishwa stadi za maisha na kupewa fursa za mikopo ili kuwainua
kiuchumi.
Anabainisha kuwa baadhi ya vijana hao tayari
wameunda kikundi cha muziki wa kizazi kipya, ambalo lilitoa burudani
wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete Machi 27, pamoja na sherehe za
miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, jijini Dar es
Salaam.
“Lengo langu ni kuwawezesha hawa vijana wawe na
maisha kama wengine, wakipata fursa za kurekodi studio, wengine timu za
kucheza mpira watafika mbali na kuliletea sifa taifa kutokana na vipaji
vyao,”anasema.
Anaongeza: “Tunahitaji wafadhili wa kuwezesha yote
hayo, Watanzania na wote wenye mapenzi mema tafadhalini wasaidieni
vijana hawa warejee kwenye ujenzi wa taifa. Mimi nimeanza, nitakufa nao
vijana hawa mpaka nikitoka Tanga, lakini tukumbuke kuwa vijana
wasipokuwa na mwelekeo nchi haitatawalika.”
Anaweka wazi kuwa anafanya yote hayo kwa kutumia
fedha zake za mshahara, ingawa pia wapo wachache wanaomsaidia, akidokeza
kuwa katika juhudi zake pia amewezesha vijana 200 wilayani humo kupata
ajira.
Anawashukuru wasanii, Mzee yusuph aliyewachukua
kijana mmoja, Tundaman watatu na Linex vijana watano kwa lengo la
kusaidia kuwakuza katika sanaa ya muziki.
Dendegu ni mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro na kwa
maneno yake, anaeleza kwamba ametokea kwenye familia ya kawaida ya
mkulima(Mzee Dendegu), aliyekuwa pia mwanasiasa.
Alipata yake ya msingi mkoani humo na baadaye
Kilakala sekondari, Msalato na kumalizia Forest alipolazimika kurejea
kufuatia kifo cha mama yake, aliyemwachia kazi ya kulea wadogo zake
saba. Hata hivyo wawili kati yao sasa ni marehemu.
Dendegu ambaye ni mama wa watoto wawili mmoja wa
kike, mwingine wa kiume alipata shahada yake katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam,(UDSM) kabla ya kuajiriwa na ‘Foundation fo Civil Society
mwaka 2003, ambapo alipata fursa ya kuzunguka mikoa yote nchini na kuwa
karibu na jamii kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya mwaka 2012.
Akizungumzia ndoto zake kimaisha ni kusonga mbele
zaidi kwa kujituma na kuweka utaifa mbele, huku akisema kuwa bado hajawa
na ndoto ya kuwa mbunge kwani wajibu alionao sasa ni utumishi wa watu
pia.
No comments:
Post a Comment