KWELI kifo hakina huruma! Msemo huu umetimia juzi kufuatia kifo cha
ghafla cha mwigizaji na mwongozaji wa filamu za Kibongo, Adam Philip
Kuambiana (38) kilichotokea akiwa njiani kukimbizwa kwenye Hospitali ya
Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kuugua.
Mwili wa Adam Kuambiana ukipelekwa Hospitali ya Muhimbili.
Kuambiana aliugua ghafla kwenye kambi ya kurekodi filamu na wasanii
wenzake iliyopo katika Nyumba ya Kulala Wageni ya Silvarado iliyopo
Sinza ya Kwaremmy, Dar.
NINI CHANZO CHA KIFO?
Akizungumza na Ijumaa
Wikienda Jumamosi iliyopita nje ya Hospitali ya Mama Ngoma, msanii wa
Bongo Fleva, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ alisema muda mchache kabla ya
kufikwa na mauti, Kuambiana alimlalamikia maumivu ya tumbo ambapo
Ijumaa iliyopita alisema hali yake si nzuri kwani alikuwa akiendesha
damu tupu.
Mmoja wa wasanii aliyekuwa katika harakati za kushuti video na Adam Kuambiana akilia kwa uchungu.
Q-Chillah alisema: “Jana (Ijumaa) jioni Kuambiana na wasanii wenzake
walikuwa baa wakinywa pombe hadi usiku mnene lakini bado aliendelea
kulalamikia maumivu ya tumbo.
“Wenzake walimuuliza ni kwa nini alikuwa akiendelea kunywa pombe kama anaumwa? Akawaambia wamuache!
“Baada ya kumaliza kunywa kila mmoja alikwenda kulala chumbani kwake
huku tukiahidiana kwamba itakapofika saa 3:00 asubuhi tuwe tayari kwa
ajili ya kwenda ‘location’.
“Lakini ulipofika muda huo sisi tukiwa tayari kwa safari tulikwenda kugonga mlango wa chumba chake bila mafanikio.
Yobunesh Batuli akiwa na simanzi nzito.
“Cha kushangaza, alisikika sauti yake kwa mbali. Kwa bahati nzuri mlango
ulikuwa wazi, mmoja akaingia ndani na kumkuta ameanguka chooni na
hajiwezi. Neno lake la mwisho alisema kwamba anajisikia kuishiwa nguvu
na anaharisha damu.
“Kutokana na hali yake hiyo mbaya tulimbeba na
kumlaza kitandani kisha tukatafuta gari na kumkimbiza Hospitali ya Mama
Ngoma ambapo daktari alisema kwamba alishafariki dunia muda mrefu.”
Rais wa Bongo Muvi, Steve Nyerere (katikati) na Mtitu wakiwa katika hali ya majonzi.
VIDONDA VYA TUMBO VYATAJWA
Kwa mujibu wa watu wa
karibu, Kuambiana kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa
vidonda vya tumbo (ulcers). Lakini pia inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na
kisukari (diabetes).
DAKTARI AELEZEA
Ijumaa Wikienda lilimtafuta
daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (aliomba jina kuhifadhiwa)
ili azungumzie kuhusu vidonda vya tumbo, alisema:
“Kwa kawaida, mtu
kuharisha damu kwa sababu ya vidonda vya tumbo inawezekana kabisa, hiyo
kitaalam inaitwa heamatemesis. Inatokana na perforation ya tumbo yaani
kidonda kuwa kikubwa.
“Kwa mtumiaji wa pombe ni kipindi anatakiwa kusimama au kuacha moja
kwa moja. Kama hatajali afya yake anaweza kufa ghafla kwani uwezekano wa
utumbo kukatika ghafla ni mkubwa.”
Ni simanzi na majonzi.
ALIJUA KIFO CHAKE
Q-Chilla ambaye ni miongoni wa
wasanii wanaocheza filamu hiyo, aliendelea kusema kuwa siku chache kabla
ya kifo, Kuambiana alimwambia filamu yake hiyo inayoitwa Jojo ndiyo ya
mwisho, hatajishughulisha tena na sanaa na alikuwa na mpango wa kwenda
China kupumzika kwa muda mrefu.
Msanii Sandra akilia kwa uchungu.
“Nimeumia sana kwani hii filamu ndiyo ilikuwa apate fedha nyingi sana
kwa sababu ni ya kwake mwenyewe na ni kali mno, amecheza vizuri
akinishirikisha mimi.
“Lakini ndiyo hivyo tena imeishia katikati,
sijui ni nani atakayeiendeleza maana mwenyewe katuachia majonzi
yasiyoelezeka,”alisema Q-Chillah.
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ na msanii aliyekuwa akishuti video pamoja na Kuambiana muda mfupi kabla ya kifo wakiwa katika majonzi.
AMEMFUATA MDOGO WAKE
Habari zaidi zinasema
kwamba, Kuambiana ameaga dunia hata arobaini ya mdogo wake wa damu,
Patrick haijafika. Patrick alifariki dunia mwezi mmoja uliopita.
AKUTANA NA MHARIRI WA GLOBAL
Ijumaa saa 10:00
jioni maeneo ya Sinza Kwaremmy jirani na Silvarado, Kuambiana alikutana
na Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global Publishers, Oscar
Ndauka.
Mhariri huyo alimuuliza ni kwa nini hawaonani siku hizi, Kuambiana akajibu:
“Nipo Mr Ndauka, nipo bwana. Tutaonana lakini sina hakika sana.”
Kuambiana alionekana mwenye afya njema na alimtania mhariri huyo kwa
kumwambia: “Naona siku hizi Ndauka unazidi kunenepa tu, mi maisha
yananipiga.”
STEVE NYERERE, BATULI WALIA SANA
Baada ya
taarifa kuenea, wasanii mbalimbali wa filamu walikusanyika katika
Hospitali ya Mama Ngoma ambapo Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven
Mengere ‘Steve Nyerere’ na Yobnesh Yusuf ‘Batuli’ walivunja rekodi ya
kulia kufuatia kifo hicho.
WADAU WAZUNGUMZIA MTU KUANGUKA CHOONI
Wadau na
mashabiki wa filamu waliokuwa eneo hilo walisikika wakisema kwamba
wasanii wengi hawana tabia za kucheki afya zao, jambo ambalo
linawagharimu kiasi cha kupoteza maisha.
Wengine walisikika wakisema kwamba watu wanaoanguka chooni mara nyingi huwa hawaponi, wakipona huwa wanapooza miili.
“Unajua watu wengi wanakosea, pale mtu anapodondoka chooni
wanamkimbiza hospitali badala ya kumtibu kienyeji, mtu akianguka chooni
tu anatakiwa kupewa ndizi mbivu lakini akipelekwa hospitali lazima
afe,” walisikika watu.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Marehemu Kuambiana alizaliwa mwaka 1976, Ifunda mkoani Iringa. Kabila ni Mmakua wa mkoani Mtwara.
Marehemu Kuambiana anatarajiwa kuzikwa kesho kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar.
Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.
Credits to Global Publishers
No comments:
Post a Comment