Enzi za uhai wake Marehemu Adam Kuambiana (wa pili kushoto) akiwa na JB, Profesa J na Q-Chillah.
KILA nafsi itaonja mauti! Pumzika mahali pema peponi
Adam Philip Kuambiana. Tasnia ya filamu imepoteza mtu muhimu, wewe
ulikuwa ufunguo na daraja kwa wasanii.
Kuambiana aliyezaliwa mwaka 1976 Ifunda mkoani Iringa, alikuwa na
vipaji vingi, alikuwa mwigizaji, muongozaji na pia mwandishi mzuri wa
miswada ya filamu (script).
Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Mlimani jijini Dar,
baadaye Sekondari ya Tambaza kisha akahamia jijini Nairobi kwenda kusoma
kidato cha tano na sita.
Adam Philip Kuambiana.
Alipofika jijini Dar kwa mara ya kwanza na kurekodi sinema ya kwanza
(Sauti ya Manka), uwezo wake ulianza kuonekana kwa waigizaji wengine
kutokana na ‘u-serious’ wake kwenye kazi.
Kabla ya kuanza kuongoza
filamu, mkali huyo alikwenda kusomea masuala yahusuyo filamu nchini
Afrika Kusini, ndipo moto wake ulipokuja kuonekana katika tasnia hiyo.
Kuonesha alikuwa ni jembe, Kuambiana alipenyeza cheche kwenye
uongozaji wa filamu ambapo ndani ya muda mfupi tu, alianza kupokea dili
mbalimbali za kuongoza filamu na wasanii wengi wakubwa wakaanza
kumtumia.
Miongoni mwa kazi nzuri na za heshima ambazo Kuambiana ameziacha ni
Sinema ya Sauti ya Manka ambayo ilitokana na wimbo wa Sauti ya Manka wa
msanii Gwamaka Kaihula ‘GK’.
Mwenendo wake mzuri na uwezo wake
ulidhihirika katika Filamu ya Regina ambayo ilipendwa na wengi kutokana
na umahiri mkubwa wa kuzitendea haki ‘sini’ zake, kiasi cha kushindwa
kutofautisha kama anaigiza au ndiyo hali halisi.
Kuambiana alikuwa na uelewa mzuri wa Lugha ya Kiingereza, kitu
ambacho kiliongeza ufanisi wake katika kazi, achilia mbali kozi fupifupi
za sanaa ambazo alisomea ndani na nje ya nchi.
Nikiwa kwenye
taaluma yangu ya uandishi wa habari, niligundua kuwa umaarufu wa
Kuambiana ulikuwa mkubwa zaidi kwa wasanii wenzake kuliko wafuatiliaji
au mashabiki wa kawaida wa sinema za Kibongo.
Nyota huyo alikuwa akisifiwa sana na wasanii, wengi walikuwa
wakifanya naye kazi kimyakimya pasipo ‘media’ kujua thamani yake, ndiyo
maana ilikuwa rahisi kwa watu kumjua zaidi mwigizaji kama Wema Sepetu
lakini na si yeye.
Kutokana na desturi ya Watanzania wengi kutothamini mchango wa mtu
akiwa hai, Kuambiana ambaye alikuwa akistahili tuzo za heshima kutokana
na kazi zake, hakupata tuzo nyingi mpaka anafariki.
Waandaaji wa tuzo mbalimbali walimpotezea kana kwamba hawamuoni.
Kwa wasanii wa kizazi kipya cha filamu, Kuambiana alikuwa kimbilio la
wengi kwani alikuwa si mtu wa kujiona wa gharama, amewasaidia wengi
kuandaa miswada, kuigiza na hata kuongoza.
Hadi mauti yanamkuta,
Kuambiana alikuwa akishuti muvi ya Jojo waliyoshirikiana na mwanamuziki
mkongwe na muigizaji, Stara Thomas ambaye anamzungumzia marehemu kuwa
alikuwa mhimili mkubwa sana katika kampuni yake ya kuzalisha filamu.
Miongoni mwa sinema ambazo marehemu ametia mkono wake kwa kiwango
kikubwa ni pamoja na Fake Pastor, Life of Sandra, Faith, More Fire,
Scola, Lost Sons, My Fiance, Jesica, Basilisa, No Body, Chaguo Langu na
nyingine kibao.
Kuambiana alipatwa na umauti alfajiri ya Mei 17, mwaka huu katika
Gesti ya Silvarado iliyopo maeneo ya Sinza, jijini Dar na anatarajiwa
kuagwa kesho (Jumanne) katika Viwanja vya Leaders na kuzikwa katika
Makaburi ya Kinondoni.
Credits to Global Publishers.
No comments:
Post a Comment