Saturday, May 2, 2015

KIVUMBI CHA POLISI NA MWENDESHA BODABODA MLIMANI CITY

BODABODA mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, mwanzoni mwa wiki hii alionja joto ya jiwe baada ya kuhenyeshwa na polisi kufuatia kitendo chake cha kukataa kutii sheria bila shuruti, alipotaka kusababisha ajali Barabara ya Chuo Kikuu, eneo la Mlimani City, jijini Dar.
 Dereva bodaboda akidhibitiwa na polisi.

Shuhuda wa sakata hilo aliliambia gazeti hili kuwa, mwendesha bodaboda huyo aliyekuwa akitokea Mwenge kuelekea Chuo Kikuu, alisimama barabarani ili kuzungumza na abiria aliyemsimamisha ndipo askari wa Jeshi la Polisi wanaotembea na pikipiki, walimfuata na kuzungumza naye.
 Dereva bodaboda akipambana na polisi.

 “Polisi walimuuliza kwa nini amesimama barabarani kwani kitendo hicho kingeweza kusababisha ajali, walimtaka awape funguo kwa kile walichosema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria, lakini bodaboda alikuja juu na kuanza kutaka kupambana na polisi,” alisema shuhuda huyo.
Inadaiwa kuwa baada ya polisi hao waliokuwa na silaha zao za moto, kuzozana kwa muda bila mafanikio na bodaboda huyo, walinzi wanaolinda lango la kuingilia Mlimani City waliungana na polisi kumtaka mwendesha pikipiki huyo kukubali kufuata sheria.

 Wakimtia nguvuni.

 “Baada ya kuona askari wa pikipiki na walinzi wamemzunguka mwenzao, bodaboda mwingine naye alisogea na pikipiki yake pale ili aweze kumsaidia, lakini naye akajikuta akiibwaga pasipo kufanikiwa kumnasua dereva huyo ambaye alikuwa jeuri,” alisema shuhuda mwingine.Askari hao walifanikiwa kumtaiti mwendesha bodaboda huyo na kwenda naye kituoni kwa maelezo zaidi.

SHOO YA ZARI ALL WHITE PARTY YAFUNIKA JIJINI DAR

 Diamond akiwachengua mashabiki kwa wimbo wake wa Nasema Nawe aliomshirikisha Malkia wa Taarab, Khadija Kopa.
 Malkia wa Taarab nchini, Khadija Kopa akiimba sambamba na Diamond Wimbo wa Nasema Nawe.

 Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Shetta akiwarusha mashabiki waliofika katika Usiku wa Zari All White Party.
 Diamond na Nay wa Mitego wakiimba ngoma yao ya Muziki Gani.
 Mashabiki wakijiachia.

 Diamond Platnumz akizikonga nyoyo za mashabiki.
 Ray Kigosi na Mama Rolaa nao ndani.
 Diamond akicheza na mashabiki wake.
Nyomi iliyohudhuria shoo hiyo.

ALI KIBA AVAMIWA USIKU WA KUAMKIA LEO

 Msanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba

 MSANII wa Bongo Fleva, Ali Kiba usiku wa kuamkia leo akiwa nyumbani kwake Kunduchi jijini Dar es Salaam, alivamiwa na kundi la watu wapatao 20 wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.

 Ali Kiba akiwa katika pozi.
 Watu hao waliokuwa na silaha za aina tofauti yakiwemo mapanga, visu na silaha za moto walifanikiwa kuvunja kuingia ndani na kuwadhuru baadhi ya ndugu wa Ali Kiba na kuiba mali na kila kitu ambacho waliweza kubeba, walimpiga na kumtesa mlinzi wa nyumba hiyo wakimtaka awaonyeshe alipo Ali Kiba, hata hivyo hawakufanikiwa kumpata na wakaondoka muda mfupi kabla ya polisi hawajafika nyumbani kwa staa huyo baada ya kupigiwa simu na majirani.
Ikiwa utakuwa na taarifa zozote zitakazosaidia kupatikana kwa majambazi hao, unaweza kutoa taarifa katika kituo cha polisi ulicho karibu nacho.

Global

Wednesday, April 29, 2015

MUNGU MKUBWA: TAZAMA PICHA JINSI KICHANGA HIKI KILIVYOOKOLEWA KWENYE KIFUSII HUKO NEPAL

Mtoto mwenye umri wa miezi minne ameokolewa kwenye kifusi cha jengo llililoanguka kufuatia tetemeko kubwa la ardhi huko Nepal.



MIILI YA WAUZA MADAWA YA KULEVYA WALIOUAWA INDONESIA YAANZA KURUDISHWA MAKWAO.

Ndugu wa marehemu waliouawa baadaya kukutwa na hatia yakuingiza madawa ya kulevya nchini Indonesia wakiwa ndani ya gari la wagonjwa liliobeba mwili ya ndugu yao mara baada ya kuupokea toka gerezani katika kisiwa cha Nusa Kambangan.

INDONESIA YAJITETEA KWA KUUA WAUZA UNGA 8, YASEMA HIYO NI VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA.

Waustralia wawili waliouawa

 Indonesia imetetea uamuzi wake wenye utata wa kuamua kuwauwa walanguzi wanane wa dawa za kulevya wakiwemo raia saba wa kigeni, ikisema kuwa hivyo ni vita dhidi ya biashara ya mihadarati.

Kwa upande wake, Australia imemuita nyumbani balozi wake Nchini Indonesia, kama hatua ya kulalamikia kuuwawa kwa raia wake wawili waliohusika na ulanguzi huo.
Waziri mkuu Tony Abbott, anasema kuwa hata ingawa anaheshimu utawala wa Indonesia kama taifa huru, uhusiano wa mataifa hayo mawili hautaendelea kama kawaida kufuatia mauwaji ya wa-australia hao wawili.
Mkuu wa sheria Nchini Indonesia, Muhammad Prasetyo, ameelezea hatua hiyo ya Ausralia kama hasira za muda mfupi tu.
 Moja ya majeneza ya wale waliouawa


Waustralia hao wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi na kikosi maalum cha wauwaji kwa pamoja na washukiwa wengine sita wa ulanguzi wa mihadarati, watano kati yao walikuwa raia wa kigeni.
Licha ya vilio vya kuwasamehe watu hao kutoka kwa mataifa ya dunia, Indonesia iliamua kwa vyovyote kuwauwa.
Kuuwawa kwa mfungwa wa tisa, raia wa Ufilipino, Mary Jane Veloso, kumecheleweshwa na Rais Joko Widodo, baada ya mwanamke mmoja kujiwasilisha kwa polisi nchini Ufilipino, akisema kuwa ndiye aliyemhadaa mfungwa huyo mwanamke mwenzake, kupeleka dawa za kulevya hadi Indonesia.
Brazil nayo inasema kuwa kuuwawa kwa raia wa pili wa Brazil Nchini Indonesia, katika kipindi cha miezi minne, ni hatua ya kutamausha na ambayo tayari imeyumbisha vibaya uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa hayo mawili.

BBC

ESCROW YAMPAISHA KAFULILA, APATA TUZO YA UTETEZI WA HAKI.

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila akikabidhiwa Tuzo ya utetezi wa haki za binadamu ya mwaka 2014, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tom Nyanduga, Dar es Salaam jana.  Kulia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, Martina Kabisama.  


Dar es Salaam. Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi),  David Kafulila baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo. Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa mkutano wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni,  liliibuliwa na Gazeti la The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za binadamu nchini.
Wengine ni Maanda Ngoifiko wa asasi ya kiraia, inayotetea haki za binadamu ya PWC kutoka  Loliondo  wilayani Ngorongoro, na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Salma Said aliyetishiwa kuuawa baada ya kuonyesha msimamo wa kukataa shinikizo la kukubaliana na muundo wa Muungano wa serikali mbili wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka jana.
Baada ya kukabidhiwa, Kafulila alisema tuzo hiyo ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kuibua ufisadi ndani ya Serikali.
“Nimepata ujasiri na kuamini kwamba siko peke yangu katika vita hii, nashukuru kupata tuzo hii, lakini nashukuru zaidi ushirikiano nilioupata kwa mhariri wa gazeti la The Citizen, ambaye alinipatia nyaraka nne za kuanzia,” alisema Kafulila.
“Hata hivyo, ninasikitishwa kuona bado Tanesco wakiendelea kulipia Dola 4 bilioni za capacity charge kwa kampuni hiyo ya ITPL, wakati hukumu iliyotolewa na Mahakama ya ICSID ya Uingereza Februari 12, mwaka jana inasema haikuwa sahihi tozo hiyo, lakini bado kiwango hicho kinaendelea kulipiwa.”
Salma alisema pamoja na vitisho ambavyo bado ameendelea kukutana navyo mpaka sasa kutoka kwa baadhi ya wabunge wa lililokuwa Bunge la Katiba, bado msimamo wake utaendelea kuwa palepale.
Aidha, alisema vita iliyopo kwa sasa imehamia kwenye harakati za Baraza la Katiba la Zanzibar ambalo linaendesha elimu kwa Wazanzibari kuhusu Katiba Inayopendekezwa. “Mimi ni mjumbe wa Baraza hilo na kwa sasa hawapendi kuona tukielimisha ukweli wa Katiba hiyo na badala yake wanataka kueleza mazuri tu. Hilo tumesema haliwezekani.”

 Miswada ya sheria

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tom Nyanduga aliyekabidhi tuzo hizo, amewataka wadau wote wa haki za binadamu nchini kufungua kesi mahakamani kupinga miswada hiyo itakayosainiwa na Rais wakati wowote kuanzia sasa.
Nyanduga aliwataka kutoendelea kulalamika tu na badala yake wachukue hatua hiyo ili kujihakikishia haki imetenda kwani Mahakama ndiyo sehemu itakayopima uhalali wa sheria hizo kama zinawapokonya uhuru na haki zao kikatiba. Miswada hiyo ni ule wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015.
Kauli hiyo inajibu madai ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kupitia viongozi wake, ambao juzi walisema ikiwa Rais Jakaya Kikwete atasaini miswada hiyo kuwa sheria, watakwenda mahakamani kupinga hatua hiyo licha ya Ikulu kueleza msimamo ikisisitiza kusainiwa miswada hiyo.
Akizungumza jana wakati wa kusherehekea Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, jijini hapa, Nyanduga alisema: “Wasilalamike tu kuna utaratibu ambao wanaweza kufikisha madai yao mahakamani bila kujali kama rais atasaini au la kwani yeye (Rais) anayo mamlaka yake kikatiba,ila wakienda mahakamani haki itatendeka kama kuna ukandamizaji umefanyika,” alisema Nyanduga.
Mbali na utoaji wa tuzo hizo, umoja huo pia ulizindua ripoti ya taarifa ya hali ya upiganiaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2014, ambayo inaonyesha kuwa kesi tano zilifikishwa mahakamani, kesi 20 zilizoripotiwa na waandishi mbalimbali wa habari nchni, wakidai kufanyiwa vitisho huku ikielezea maombi ya uboreshaji wa sheria 29 kandamizi katika uhuru na haki za wananchi kupata taarifa.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alikuwa miongoni mwa wadau wa umoja huo ambaye alisema kundi la wanaokandamiza haki isitendeke nchini linazidi kujitokeza, huku likijenga hofu kwa watetezi wa haki.
“Kundi hilo halipendi kukosolewa na hata likiona kuna utetezi sehemu fulani, basi yule anayetetea atakuwa kwenye wakati mgumu. Mfano kuna vipingamizi vya kuzuiwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa ili tusitoe elimu juu ya Katiba inayopendekezwa katika baadhi ya wilaya nchini. Hatuwezi kukubaliana na hali hiyo lazima tuone haki ikitendeka kwa wote,” alisema Dk Hellen.

MWANANCHI