Saturday, May 2, 2015

KIVUMBI CHA POLISI NA MWENDESHA BODABODA MLIMANI CITY

BODABODA mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja, mwanzoni mwa wiki hii alionja joto ya jiwe baada ya kuhenyeshwa na polisi kufuatia kitendo chake cha kukataa kutii sheria bila shuruti, alipotaka kusababisha ajali Barabara ya Chuo Kikuu, eneo la Mlimani City, jijini Dar.
 Dereva bodaboda akidhibitiwa na polisi.

Shuhuda wa sakata hilo aliliambia gazeti hili kuwa, mwendesha bodaboda huyo aliyekuwa akitokea Mwenge kuelekea Chuo Kikuu, alisimama barabarani ili kuzungumza na abiria aliyemsimamisha ndipo askari wa Jeshi la Polisi wanaotembea na pikipiki, walimfuata na kuzungumza naye.
 Dereva bodaboda akipambana na polisi.

 “Polisi walimuuliza kwa nini amesimama barabarani kwani kitendo hicho kingeweza kusababisha ajali, walimtaka awape funguo kwa kile walichosema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria, lakini bodaboda alikuja juu na kuanza kutaka kupambana na polisi,” alisema shuhuda huyo.
Inadaiwa kuwa baada ya polisi hao waliokuwa na silaha zao za moto, kuzozana kwa muda bila mafanikio na bodaboda huyo, walinzi wanaolinda lango la kuingilia Mlimani City waliungana na polisi kumtaka mwendesha pikipiki huyo kukubali kufuata sheria.

 Wakimtia nguvuni.

 “Baada ya kuona askari wa pikipiki na walinzi wamemzunguka mwenzao, bodaboda mwingine naye alisogea na pikipiki yake pale ili aweze kumsaidia, lakini naye akajikuta akiibwaga pasipo kufanikiwa kumnasua dereva huyo ambaye alikuwa jeuri,” alisema shuhuda mwingine.Askari hao walifanikiwa kumtaiti mwendesha bodaboda huyo na kwenda naye kituoni kwa maelezo zaidi.

No comments:

Post a Comment