Dar es Salaam. Sakata la uchotwaji wa fedha
katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR- Mageuzi), David Kafulila baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua
mchango wake katika kufichua ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306
bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza
nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka
kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa mkutano
wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni, liliibuliwa na Gazeti la
The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd
na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea
haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu
zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za
binadamu nchini.
Wengine ni Maanda Ngoifiko wa asasi ya kiraia,
inayotetea haki za binadamu ya PWC kutoka Loliondo wilayani
Ngorongoro, na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Salma Said aliyetishiwa
kuuawa baada ya kuonyesha msimamo wa kukataa shinikizo la kukubaliana
na muundo wa Muungano wa serikali mbili wakati wa Bunge Maalumu la
Katiba.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo
vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na
hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa
zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za
binadamu kwa mwaka jana.
Baada ya kukabidhiwa, Kafulila alisema tuzo hiyo ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kuibua ufisadi ndani ya Serikali.
“Nimepata ujasiri na kuamini kwamba siko peke
yangu katika vita hii, nashukuru kupata tuzo hii, lakini nashukuru zaidi
ushirikiano nilioupata kwa mhariri wa gazeti la The Citizen, ambaye
alinipatia nyaraka nne za kuanzia,” alisema Kafulila.
“Hata hivyo, ninasikitishwa kuona bado Tanesco
wakiendelea kulipia Dola 4 bilioni za capacity charge kwa kampuni hiyo
ya ITPL, wakati hukumu iliyotolewa na Mahakama ya ICSID ya Uingereza
Februari 12, mwaka jana inasema haikuwa sahihi tozo hiyo, lakini bado
kiwango hicho kinaendelea kulipiwa.”
Salma alisema pamoja na vitisho ambavyo bado
ameendelea kukutana navyo mpaka sasa kutoka kwa baadhi ya wabunge wa
lililokuwa Bunge la Katiba, bado msimamo wake utaendelea kuwa palepale.
Aidha, alisema vita iliyopo kwa sasa imehamia
kwenye harakati za Baraza la Katiba la Zanzibar ambalo linaendesha elimu
kwa Wazanzibari kuhusu Katiba Inayopendekezwa. “Mimi ni mjumbe wa
Baraza hilo na kwa sasa hawapendi kuona tukielimisha ukweli wa Katiba
hiyo na badala yake wanataka kueleza mazuri tu. Hilo tumesema
haliwezekani.”
Miswada ya sheria
Miswada ya sheria
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (THBUB), Tom Nyanduga aliyekabidhi tuzo hizo, amewataka
wadau wote wa haki za binadamu nchini kufungua kesi mahakamani kupinga
miswada hiyo itakayosainiwa na Rais wakati wowote kuanzia sasa.
Nyanduga aliwataka kutoendelea kulalamika tu na
badala yake wachukue hatua hiyo ili kujihakikishia haki imetenda kwani
Mahakama ndiyo sehemu itakayopima uhalali wa sheria hizo kama
zinawapokonya uhuru na haki zao kikatiba. Miswada hiyo ni ule wa Sheria
ya Takwimu ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015.
Kauli hiyo inajibu madai ya Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), kupitia viongozi wake, ambao juzi walisema ikiwa Rais
Jakaya Kikwete atasaini miswada hiyo kuwa sheria, watakwenda mahakamani
kupinga hatua hiyo licha ya Ikulu kueleza msimamo ikisisitiza kusainiwa
miswada hiyo.
Akizungumza jana wakati wa kusherehekea Siku ya
Watetezi wa Haki za Binadamu nchini, jijini hapa, Nyanduga alisema:
“Wasilalamike tu kuna utaratibu ambao wanaweza kufikisha madai yao
mahakamani bila kujali kama rais atasaini au la kwani yeye (Rais) anayo
mamlaka yake kikatiba,ila wakienda mahakamani haki itatendeka kama kuna
ukandamizaji umefanyika,” alisema Nyanduga.
Mbali na utoaji wa tuzo hizo, umoja huo pia
ulizindua ripoti ya taarifa ya hali ya upiganiaji wa haki za binadamu
kwa mwaka 2014, ambayo inaonyesha kuwa kesi tano zilifikishwa
mahakamani, kesi 20 zilizoripotiwa na waandishi mbalimbali wa habari
nchni, wakidai kufanyiwa vitisho huku ikielezea maombi ya uboreshaji wa
sheria 29 kandamizi katika uhuru na haki za wananchi kupata taarifa.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alikuwa miongoni mwa wadau wa umoja huo
ambaye alisema kundi la wanaokandamiza haki isitendeke nchini linazidi
kujitokeza, huku likijenga hofu kwa watetezi wa haki.
“Kundi hilo halipendi kukosolewa na hata likiona
kuna utetezi sehemu fulani, basi yule anayetetea atakuwa kwenye wakati
mgumu. Mfano kuna vipingamizi vya kuzuiwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa
mikoa ili tusitoe elimu juu ya Katiba inayopendekezwa katika baadhi ya
wilaya nchini. Hatuwezi kukubaliana na hali hiyo lazima tuone haki
ikitendeka kwa wote,” alisema Dk Hellen.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment