Monday, April 27, 2015

MASTAA WANAOONGOZA KUTUKANA\KUTUKANWA MTANDAONI

Tamrina Posh "Amanda" katika pozi

Imekuwa ikielezwa kuwa wasanii ni kioo cha jamii. Kwa maana hiyo wanatakiwa kufanya mambo ambayo yanaweza kuigwa na wale wanaowatazama. Hata hivyo, maisha wanayoishi baadhi ya wasanii hayaakisi msemo huo.
Wengi wamekuwa wakikumbwa na skendo mbalimbali zinazowafanya wasiwe na vigezo vya kuitwa kioo cha jamii.
Miongoni mwa mambo yanayowafanya wakati mwingine wadharaulike ni kutoa maneno machafu, ‘live’ au kupitia kwenye mitandao ya kijamii.

Katika makala haya nitawazungumzia mastaa wanaoongoza kwa kutukana mitandaoni lakini pia wale ambao wanaongoza kwa kutukanwa katika siku za hivi karibuni.

 Wastara Juma

Wastara…

Huyu Wastara amekuwa akiheshimika kwenye jamii kwa muda mrefu na alikuwa ni miongoni mwa mastaa wa kike ambao wangesimama na kuamua jambo wangesikilizwa kutokana na jinsi alivyokuwa amejiweka na kuwaaminisha watu.
Lakini katika siku za hivi karibuni alichafuka kwa kuingia katika orodha ya mastaa wanaotukana mtandaoni baada ya kumvaa mmoja wa mashabiki wake aliyemsemea mbovu na kumtukana matusi mazito
 “Iweje anakubali kushushwa na mtu mmoja ambaye alikaa na kuamua kumvuruga, anasahau kama kuna kundi la watu linamheshimu?”  Aliandika mmoja wa mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram baada ya kuona matusi hayo.

 Amanda Posh
Wafuatiliaji wa mambo na hasa wale ambao wapo Facebook watakumbuka jinsi staa huyu wa filamu alivyomshambulia jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la Joel.
Haikuwa ustaarabu kabisa kwa staa huyo kufanya hivyo kwani jambo lililomkasirisha angeweza kulipuuza na angebaki na heshima yake huku yule aliyemtukana akionekana mjinga.
Lakini ukiacha hilo, Amanda amekuwa akisifika kwa kutoa maneno machafu pale anapochokozwa, tabia inayomfanya afiti kwenye makala haya.


Isabela Mpanda
Katika mastaa micharuko, huyu yumo! Hajivuni, hajisikii lakini ukimchokoza lazima akushikishe adabu kwa matusi.
Posti zake zenye lugha chafu kwenye mtandao wa Instagram zipo nyingi lakini pia kwa wale wenye kumbukumbu watakumbuka kuwa staa huyu aliwahi kumtukana mwanamitindo Belina Mgeni na mpaka sasa hawaongei.
Hao ni baadhi ya mastaa ambao katika siku za hivi karibuni wameshika chati kwenye suala la kutukana mtandaoni.
Kwa upande wa wale ambao wanashika nafasi za juu kwa kutukanwa, wapo wengi lakini leo tutawazungumzia wahanga watatu.

 Kajala Masanja: 
Tangu aingie kwenye bifu na Wema Sepetu, kuna kundi ambalo linajiita Team Wema limekuwa likimshambulia kwa kumtukana na kumshutumu kwa mambo ambayo mengine hayana ukweli.
Hata hivyo, Kajala anaonekana kuwa mstaarabu kidogo kwani licha ya kutukanwa mtandaoni, yeye amekuwa mkimya akijua kujibizana na watu hao ambao wala hawana majina ni sawa na kuzidi kujichafulia.
Elizabeth Michael ‘Lulu’: Huyu naye ni mhanga wa matusi mtandaoni. Kuna kundi la watu ambao linaonekana kuwa na chuki dhidi yake, huenda kutokana na mafanikio aliyonayo akiwa kwenye umri mdogo.
 Lakini sasa, licha ya matusi anayoyaoga mtandaoni, amekuwa mvumilivu wa kuyaacha yapite. Watu wake wa karibu wanaeleza kuwa, licha ya kutukana sana mwenyewe wala hajui kwamba anatukanwa kwani si mtu wa kufuatilia nani kasema nini kibaya juu yake
Wema Sepetu:
Kama ilivyo kwa Kajala, huyu naye anashambuliwa sana na Team Kajala. Hawa ni watu ambao wamejitenga kuhakikisha wanamkosesha amani staa huyu.
 Amekuwa akitukanwa kwa mengi lakini kwa kuwa anajua ustaa ni kama jalala, huwa hajali na anachukulia poa.
 Ni mara chache sana amekuwa akinyanyua mdomo wake kuwajibu wale ambao wamekuwa wakimsema vibaya sambamba na kumtukana.
Kwa uchache hao ndiyo mastaa ambao hivi karibuni wametia fora kwa
 kutukana na kutukanwa mtandaoni.
Tahadhari
Mastaa ambao ni wepesi kutukana mtandaoni  wajue kwamba endapo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete atasaini ile sheria ya makosa ya mtandaoni ya mwaka 2015, watajikuta wanaenda jela hivi hivi.

GLOBAL PUBLISHERS








No comments:

Post a Comment