Mgombea urais wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Tanzania, TUCTA Bw. Dismas Lyassa akiongea na waandishi wa habari leo katika hoteli ya Lamada jijini Dar Es Salaam.
metolewa leo tarehe 16 Julai 2014
Na Dismas Lyassa
Mgombea Urais wa TUCTA; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Salaam
Wapendwa ndugu zangu wana habari…Asalam Aleikum…Tumsifu Yesu Kristo… Bwana Yesu Asifiwe…!
Ndugu wanahabari
Lengo hasa la kuwaiteni mahali hapa ni kutoa taarifa kwenu kuwa
ninagombea Urais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania,
uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 4-5, Dodoma.
Vipaumbele vyangu ni;
Ndugu wanahabari
Nina malengo ya kuifufua na kuleta TUCTA yenye uhai na mabadiliko ya kweli kwa kufanya yafuatayo;
Ndugu wanahabari
1. Kupigania na kulinda haki za wafanyakazi;
Katika kipaumbele hili lengo hasa ni kuondoa matatizo sugu ya wafanyakazi yakiwamo-:
i. Kulipwa ujira/mishahara duni isiyoendana na uhalisia wa maisha.
ii. Ucheleweshaji wa upatikanaji wa ujira/mishahara
iii. Ucheleweshaji fedha za kujikimu kwa waajiriwa wapya/ kiwango kidogo cha fedha za kujikimu
iv. Uhaba au kutokuwepo kabisa makazi kwa wafanyakazi wapya
v. Rushwa na kuajiri kwa misingi ya kujuana kwa mfano katika
Halmashauri ya Siha, wilaya ambayo imegawanywa kutoka Hai, kuna pori
kubwa la West Kilimanjaro mlimani kabisa, hakuna maendeleo…ni suala la
kawaida kuona watu wakiongea kilugha ofisini kama lugha ya Taifa
vi. Wakubwa yaani mabosi kujifanya Mungu kwa kuwaendesha wafanyakazi kwa kadri wanavyotaka wao, sivyo inavyosema sheria.
vii. Uwepo wa mpangilio usio sawa wa ujira/mishahara.
viii. Kutopewa posho au kupewa kidogo au kutopewa kwa wakati
ix. Fedha za uhamisho na likizo; kwa mfano kuna walimu ambao wameanza
kazi 2004 NIT Shule ya msingi Dar es Salaam wamelipwa fedha za likizo
mara moja mwaka 2012, mfano halisi ni mwalimu Ruth Natumwa, huyo ni kati
ya walimu hao. Matatizo ya walimu kimsingi ni janga la taifa, yapo
Taifa zima, kwa mfano katika shule ya Sekondari Kizota, Dodoma kuna
walimu wengi wana madai yao dhidi ya Serikali, waliajiriwa mwaka jana
Machi, wakaanza kupata mshahara mwenzi wa tisa…walilipwa mshahara wa
mwezi wa tisa tu na kuendelea, ile mingine wanaendelea kudai.
x.
Mazingira magumu ya kazi mijini na vijijini (tunapozungumzia mazingira
magumu inahusisha kutokuwepo vitendea kazi au kuwa vichache, miundo
mbinu duni nk).
xi. Waajiri kutochangia mifuko ya jamii
xii.
Fedha za makato ya wafanyakazi kupitia mifuko ya jamii zimekuwa
zikikopeshwa watu wengine wasio wanachama wakiwamo wanasiasa huku
wafanyakazi wenyewe wakiendelea kuwa na maisha duni
xiii. Kufanya kazi kama kibarua kwa miaka mingi jambo ambalo ni tofauti za sheria za kazi
xiv. Huduma za kifedha kuwa mbali na maeneo ya kazi, hali
inayosababisha wafanyakazi kutumia fedha nyingi kufuatilia mishahara kwa
vile ni mbali na eneo wanalofanyia kazi.
xv. Kutokuwa na mfumo unaoeleweka wa upandishaji vyeo na ujira/malipo kwa wafanyakazi/vibarua
xvi. Waajiri hasa binafsi kufukuza wafanyakazi hovyo/no job security…kufanya kazi bila mikataba
xvii. Kupambana na tatizo la kodi kubwa kwa mishahara (PAYE)
xviii. Tatizo la mabosi kutoa upendeleo wa wazi kwa baadhi ya wafanyazi
kwa sababu zisizo za kitaalamu; wakati mwingine ni kwa sababu ya ngono;
kuwataka kimapenzi wafanyakazi ili waendelee kuwepo kazini au
kupandishwa vyeo…tatizo hili linaonekana kuwa sugu, wanawake wengi
maofisini hawako huru sana, wamekuwa wakitakwa kimapenzi mno na mabosi
wao, wengi wanashindwa kujizuia, tunataka kuona kunakuwa na sheria kali
dhidi ya mabosi wa aina hii kama ilivyo katika nchi nyingine.
Ndugu wanahabari
Tatizo la ajira kuporwa na wageni
Ingawa sheria/sera za ajira zinaeleza wazi kwamba hairuhusiwi wageni
kuingia nchini zaidi ya watano kwa kazi ziziso na ujuzi, baadhi ya
makampuni yamekuwa yakiingiza wageni kwa kazi ambazo Watanzania wengi
wanaweza kuzifanya.
Ndugu wanahabari
Nitahakikisha wazawa
wanapewa fursa ya kufanya kazi nchini; hii ni pamoja na kuomba CV za
wageni ili tuone kama ni kweli hakuna Watanzania wenye sifa za kufanya
hiyo kazi hiyo.
-: Kumekuwa na taarifa za uwepo wageni
katika makampuni kadhaa yakiwamo mahoteli, migodi, viwanda vya sarufi nk
ambao baadhi wanalipwa malipo makubwa tofauti na wazawa japo hawana
elimu au ujuzi wa kuwazidi wazawa. Nitakuwa na kamati maalumu ya
kufuatilia waajiriwa wote Tanzania hasa wageni ili kujua kama wanazo
sifa za kufanya kazi au wanapora nafasi za Watanzania.
Ndugu wanahabari
Nitapigania kuhakikisha tabia ya waajiri kulazimisha waajiriwa lazima wawe na uzoefu mkubwa inapungua au kukoma kabisa
Kigezo cha kupata ajira kiwe ni uwezo wa mtu wakati huo baada ya
kufanyiwa usaili, siyo lazima awe na uzoefu wa miaka mitatu au mitano
kama ambavyo waajiri wengi wanalazimisha; tunahitaji kuona Serikali
inasimamia hili. Kama hali ni hii, wahitimu wanawezaje kupata ajira? Ni
suala ambalo nitakuwa mkali nalo mno kwa sababu lina athari kubwa kwa
jamii ya Tanzania, limekuwa ni sababu ya rushwa ikiwamo ya ngono…walioko
vyuoni wengi hawana uhakika wa ajira, kwa sababu ya tabia hii. Ni
lazima tubadilike, watu waajiriwe kulingana na uwezo wao wa kazi, siyo
uzoefu.
Ndugu wanahabari
Wanafunzi shule ya Msingi/Sekondari nk wapatiwe elimu ya kujiajiri.
Kwa nafasi nitakayokuwanayo nitaishawishi Serikali iingize elimu ya
ufundi/utengenezaji bidhaa na ujasiriamali kama mojawapo ya masomo ya
ziada kama njia ya kupambana na tatizo la ajira ambalo linaonekana kukua
nchini. Kama ambavyo kumekuwa na masomo ya dini katika shule zenu, tuwe
pia na masomo ya ujasiriamali. Nitaangalia namna ya kuzishawishi
taasisi zingine za ndani na nje kuhakikisha hili linafanyika; lengo ni
kuhakikisha hata mhitimu wa msingi au sekondari nk awe ana uwezo wa
kufanya ujuzi anaotaka kama kujenga, kushona, kufuma, kufuga,
kutengeneza batiki, vikoi, sabuni, mishumaa nk.
Ndugu wanahabari
Nitaanzisha idara mbili mpya na kuboresha zilizoko;
i. Idara ya walemavu
Hii itahusika kuangalia hali ya maisha ya wafanyakazi walemavu nchini
ikiwamo kuwasaidia kupata baiskeli na huduma zingine muhimu.Nitatumia
uzoefu wangu kwa kushirikiana na rafiki zangu wa nje kuhakikisha hili
linafanikiwa. Tutaangalia namna ya kushirikiana na mashirika mbalimbali
yakiwamo Free Wheelchair Foundation www.wheelchairfoundation.org.
Ndugu wanahabari
Kutakuwa ni mikakati mbalimbali kuhusu wafanyakazi walemavu na wale
wanaopata ulemavu wakiwa kazini, kwa mfano Mwenyekiti wa Wasioona mkoani
Tanga amekuwa ni mtu ambaye ameumia kazini, lakini aliishia kulipwa
Sh150,000 na bandari ambako alikuwa anafanya kazi kama kibarua. Kitendo
kitakuwa na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu hali za wafanyakazi
walemavu, kuangalia kama wanavyotoka vyuoni wanapewa ajira au wanaishia
kunyanyapaliwa? Utafiti unaonyesha kuna wanafunzi wengi wanaohitimu
masomo wakiwa na ulemavu, hata hivyo hawaonekani kwenye maofisi
wakifanya kazi. Wanakwenda wapi? Litakuwa ni jukumu la hicho kitengo.
Ndugu wanahabari,
Idara ya pili ni
Idara ya fursa/Career Development Department na Mafunzo
Nimetembea katika nchi tofauti Duniani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Mauritius, India, Thailand, Sweden na Marekani…nimeona fursa
kadhaa ambazo zimenishawishi kuanzisha idara maalum ya kusaidia
wafanyakazi kufahamu fursa zinazoendelea Duniani na hapa nchini. Fursa
hizo zitakuwa zinapatikana katika tovuti za TUCTA na ofisi za vyama vya
wafanyakazi mikoani. Baadhi ya fursa ni namna gani mtu anaweza kusoma
nje ya nchi bila kulipa ada kwa kozi za muda mrefu na mfupi, fursa ya
mashirika ambayo yanatoa misaada kwenye sekta mbalimbali.
-Kwa mfano kuna mashirika kama www.nuffic.nl au vyuo ambavyo mtu anaweza kusoma bure bila kulipa chembe ya ada kama www.berea.edu
ya Marekani na fursa nyingine nyingi. Nimegundua Watanzania wengi
hawanufaiki sana na fursa hizi. Ziko pia taasisi nyingine zinatoa.
Ndugu wanahabari
Idara hii itakuwa na majukumu ya kutoa elimu kwa wafanyakazi kuzifahamu
sheria za kazi, hali kadhalika itakuwa inawasiliana na waajiri ili
zaidi ya barua ya ajira au mkataba wanaompa mwajiriwa, ampe pia na
chapisho letu ambalo mwajiriwa anapaswa kupewa siku ya kuajiriwa kwake
ili ajue kwa uhakika sheria za kazi zinasemaje; haki ya mwajiriwa kwa
mwajiri au ipi na haki ya mwajiri kwa mwajiriwa ni ipi; tutashawishi
hili liwe ni suala la lazima. Tutakuwa na vituo maalum vya msaada wa
kisheria mikoani kote au kwenye kanda. Tutakuwa na vipindi kwenye
televisheni angalau kila mwezi mara kuelezea masuala ya sheria za kazi.
Tutaitumia tovuti ya TUCTA kuwa ya kisasa zaidi.
Ndugu wanahabari
Kulifufua gazeti la Mfanyakazi ndani ya siku 90 ili liwe sauti thabiti ya wafanyakazi
Haijalishi kama TUCTA itakuwa na fedha au la, nitahakikisha ndani ya
siku 126 litakuwa mitaani likiandika habari mbalimbali hasa likitumika
kama sauti ya wafanyakazi na yote ambayo yataonekana ni ya maana kwa
ustawi wa taifa. Nina uzoefu zaidi ya miaka 20 katika sekya ya habari
kama Mhariri, na hata sasa ni Mhariri wa Biashara gazeti la Mwananchi,
nitahakikisha tunatafuta fedha ndani na nje ya TUCTA ikiwamo kuwatumia
wafanyabiashara kwa kubadilishana msaada kwa matangazo kwa muda, ili
hatimaye liweze kuwa mitaani. Ni aibu kubwa kuona nchi ina wafanyakazi
wengi, lakini gazeti kama hili la wafanyakazi haliko mitaani.
Ndugu wanahabari
Kuimarisha uhusiano wa vyama vya ndani na vyama vya nje
Nitahakikisha nafanya mawasiliano na mashirika mengine yakiwamo
International Trade Union Confederation, Secretary General Sharan
Barrow na mashirika mengine ili kuona namna gani vyama vya wafanyakazi
vya nchini vinanufaika na ushirikiano huo kwa kubadilishana uzoefu na
kadhalika mara kwa mara kadri inavyowezekana.
Ndugu wanahabari
Nitatutumia uzoefu wangu wa shughuli za kuwasiliana na vyuo vya nje na
uzoefu wangu wa kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya nje kama
muwakilishi wao hapa nchini, na kutembea nchi mbalimbali, kuviunganisha
vyama vya ndani vya wafanyakazi, kuwa na ukaribu zaidi na vile vya nje,
na pia kujenga uwezekano wa viongozi nchini kwenda nje kupitia
ushirikiano huo.
Ndugu wanahabari
Hili linawezekana kwa
njia mbili, kwanza kama washirika wetu kwa vile tutakuwa tuna
mawasiliano ya karibu na aina ya chama ambacho mtu anatoka, kwa mfano
kama COTWU, TTU, TALGWU, TUICO, TAMICO, TEWUTA, DOWUTA, TPAWU, RAAWU,
TUGHE, CHODAWU, TRAWU. Nahitaji kuona ofisi za vyama vya wafanyakazi
nchini zinakuwa za kuvutia kwa kuzipatia vitendea kazi, kuna mashirika
nayafahamu, tunaweza kuyatumia kuwasiliana nayo yakatusaidia kama vile
Computer Aid International la Uingereza ambalo hutoa misaada ya computer
za aina mbalimbali kwa nchi maskini kama Tanzania (www.computeraid.org).
Nje ya hiyo nitakuwa na vikao na viongozi wa chama kimoja badala ya
kingine kuangalia namna gani tunaweza kuboresha shughuli za utendaji za
ndani na nje hasa kuimarisha rasilimali watu na vifaa. Lengo kubwa la
kuomba niwe Rais wa TUCTA ni kuangalia namna gani tunaweza kushirikiana
na wafanyakazi na viongozi wa vyama katika kuimarisha wafanyakazi, kwani
malalamiko ni mengi. Tutaendeleza mali za TUCTA zikiwamo Chuo cha
Wafanyakazi Mbeya na maeneo mengine.
Ndugu wanahabari
NAMNA GANI HAYA YATAWEZEKANA?
Mkakati wa kuondoa kero zote zilizoelezwa juu utafanikiwa kwa
majadiliano yenye ukomo (deadline) na Serikali/waajiri, au kufanya
chochote ambacho katiba inaruhusu. Sheria ziko wazi, nitahamasisha
zifuatwe na zifahamike. Shida kubwa ninayoiona kwa sasa, wafanyakazi
wengi hawajui haki zao pia msaada wa vyama katika kuwasaidia wafanyakazi
ni mdogo.
Ndugu wanahabari
Hata hivyo mkakati hasa ni
kuangalia TUCTA kwa kushirikiana na vyama shiriki vinafanya nini kuondoa
changamoto ambazo sisi wenyewe tunaweza kuziondoa. Uongozi siyo
kulalamika, bali kuthubutu kuchukua hatua zinazoweza kuondoa shida
zilizoko. Tayari nimeanza kuwasiliana na vyama mbalimbali vya
wafanyakazi katika mataifa ya nje ili kuangalia namna gani
tunashirikiana kwa maana ya kubadilishana uzoefu nk.
Ndugu wanahabari
Ofisi nyingi za vyama vya wafanyakazi zimechakaa, naangalia uwezekano
wa kushirikiana nao katika hili kwa njia ya kutafuta wafadhili wa nje au
kubuni miradi itakayosaidia kuondoa hali hiyo; nataka pia maisha ya
viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kwa ujumla yabadilike
kwa kutumia jitihada hizo nilizozieleza juu, nafahamu vizuri namna ya
kusaka wafadhili, kwani ni shughuli ambayo nimekuwa nikifanya kwa muda
mrefu kupitia taasisi yangu ya Global Source Watch, niliyoianzisha toka
mwaka 2001 ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuwaunganisha watu na vyuo
zaidi ya 78 vya nje kama Marekani, Canada, Greece, India, Malaysia nk.
Ndugu wanahabari
Nafahamu kuna vyama vina miradi ya maendeleo, vinawasaidiaje wanachama
wao? Nahitaji niwe Rais ili nishirikiane na vyama vya wafanyakazi na
wafanyakazi kwa ujumla kuleta tija kwa Watanzania. Tusiwe watu wa
kunyoosheana vidole…kila mtu awe chanzo cha mabadiliko anayotaka kuyaona
Tanzania! Naamini kila mtu akifanya kazi zake vizuri…Tanzania itakuwa
na maendeleo kwa kasi. Wafanyakazi wanahitaji mambo mengi zaidi ya
kuhamasishwa migomo, lakini kama tutaamua kugoma, tunapaswa kugoma kwa
kumaanisha, hatupaswi kuogopa kutekeleza yaliyo haki yetu.
Ndugu wanahabari
Kwa nafasi nitakayokuwa nayo nitaanzisha semina, makongamano, mijadara
itakayokuwa ya wazi na kutoa elimu ya kutosha juu ya haki za wafanyakazi
na wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi. Hii itasaidia kupunguza migogoro
na wafanyakazi watatambua haki zao.
Ndugu wanahabari
Tunatakiwa kuwa sauti ya wafanyakazi hapa Tanzania, TUCTA imelala,
tunataka kuikimbiza mchakamchaka,, kuna mambo mengi yanatokea dhidi ya
wafanyakazi hapa nchini lakini TUCTA haitoi hata matamko au kutetea
wafanyakazi,
Ndugu wanahabari
Natambua changamoto za wafanyakazi, tunataka kuwa na
TUCTA Mpya
Nguvu Mpya
Uongozi Mpya
Sauti Mpya
Umoja Mpya
Maendeleo Mapya
Kwa pamoja tunaweza.
Mungu awabariki!
Dismas Lyassa
Mgombea nafasi ya Urais-TUCTA
simu 0754 49 89 72
********************
HOTUBA FUPI KUTOKA KWA JEBRA KAMBOLE, Wakili wa Dismas Lyassa
anayefanya Kampuni ya Uwakili ya Law Guards Advocates ya Jijini
Dar-es-salaam kwa Waandishi wa Habari.
Ndugu waandishi wa Habari wa vyombo vyote vya Habari,
Ndugu watanzania wengine mliopo hapa,
Shukrani
Tunashukuru sana kwa kuitikia wito wetu, Mungu awabariki sana, Tunamshukuru mwenyezi mungu kwa kutupa afya na sia njema,
Ndugu waandishi wa Habari
Kuna mambo muhimu manne tunataka kuwaeleza watanzania wote, hasa wafanyakazi na viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi
Moja, Ndugu anatimu iliyojipanga makini kuhakikisha TUCTA inarejea na
kuwa na Nguvu zaidi, Ni kijana makini mwenye malengo ya kuleta maendeleo
ya haraka na kufufua uhai wa TUCTA.
Ndugu Waandishi wa Habari
Napenda kuchukua fursa hii kutoa onyo kwa wanaopanga kutoa rushwa
kwenye huu uchaguzi wa TUCTA kuwa tuko makini na hili tumejipanga,
tutachukua hatua za haraka za kisheria dhidi yao, ikiwa ni pamoja na
kuwaripoti kwenye vyombo husika, Rushwa si kipaumbele utapinga kwa nguvu
zetu zote.
Ndugu Waandishi wa Habari
Ndugu Dismas Lyasa
pia atasaidia kuanzisha kituo au kushirikiana na mashirika mengine kutoa
masaada wa kisheria kwa wafanyakazi wanaofukuzwa makazini kinyume cha
sheria. Wafanyakazi wengi wakikumbwa na matatizo wafanyakazi wenzao
wanawatenga, vyama vyao vinawatenga, Dismas atahakikisha kuwa TUCTA ni
kimbilio lao.
Ndugu Waandishi wa Habari
Ndugu Dismas Lyasa
atasaidia kutoa mafunzo ya kisheria kwa wafanyakazi ili waweze kutambua
haki zao za msingi, kwa kuendesha semina, makongamano na mijadara
itakayotoa elimu na kuibua mijadala kwa wafanyakazi.
CHAGUA DISMAS LYASA KWA TUCTA MPYA, Mabadiliko ni sasa, Asanteni.
No comments:
Post a Comment