Friday, June 27, 2014

YULE MSUDANI ALIYETAKA KUUAWA SABABU YA KUOLEWA NA MKRISTO AELEZA MAKUBWA

Dunia haina huruma! Meriam Ibrahim, raia wa Sudan aliyetakiwa kuhukumiwa adhabu ya kifo kufuatia kuolewa na mwanaume Mkristo, Daniel Wani, raia wa  Marekani, amezidi kuteseka baada ya kuachiwa huru kisha kudaiwa kukamatwa tena hivyo kumuongezea mateso juu ya mateso.

 Meriam Ibrahim, raia wa Sudan akiwa na mume wake (Daniel Wani ) ambaye ni mkristo. 

Mwanamke huyo aliachiwa huru Jumatatu iliyopita, Juni 23, mwaka huu baada mashirika mbalimbali ya kupigania haki za binadamu ikiwemo ubalozi wa Marekani kuingilia kati suala lake.
Awali, sheria za nchini humo, zilimtia hatiani mwanamke huyo kwa kosa la kubadili dini wakati alipoolewa na Daniel mwaka 2011 katika Kanisa Katoliki.
Mahakama ilidai ilimtambua mwanamke huyo kama Muislam tangu alipozaliwa hivyo kubadili dini kwa kuolewa na mwanaume ampendaye ni kosa kisheria na kahukumiwa adhabu hiyo ya kifo.
Meriam ambaye ni mama wa watoto wawili, kabla ya kuachiwa huru, alikuwa akishikiliwa mahabusu kwa takriban miezi tisa, aliteseka gerezani na kilichokuwa kikimuumiza zaidi ni hukumu ya kifo.

 Meriam Ibrahim na mume wake wakiwa kwenye picha ya pamoja na familiya yake.

 Mumewe ameelezea kuwa, kulikuwa na mvutano kwenye Uwanja wa Ndege wa Khartoum ambapo alikuwa ameongozana na mkewe pamoja na watoto wao wawili kuelekea Marekani, kabla wanausalama zaidi ya 40 kujitokeza na kumkamata upya Meriam hivyo kumuongezea mateso juu ya mateso.
Katika kipindi ambacho alikuwa gerezani, Meriam alifungwa pamoja na mwanaye wa kwanza huku wa pili akijifungua akiwa humohumo gerezani.
Vyanzo mbalimbali vya habari nchini humo vimeeleza kuwa, baada ya kuachiwa huru, alikamatwa tena kwa kile kinachodaiwa kuwa wamefanya udanganyifu katika hati za kusafiria.
Tangu Meriam alipokamatwa kwa mara ya kwanza, Septemba 27, mwaka jana, mumewe alikwenda katika ubalozi wa Marekani nchini humo kulalamikia tatizo la mkewe lakini alijibiwa kuwa wapo bize.

No comments:

Post a Comment