Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga (Chadema),
amewaumbua wabunge wenzake kuwa wanapeana na kuchukua rushwa ndani ya
Bunge.
Suzan aliyasema hayo juzi jioni wakati akichangia
katika mkutano wa Chama cha Wabunge walio katika Mapambano dhidi ya
Rushwa (APNAC). Suzan alisema vitendo hivyo vya rushwa vilionekana
wakati wabunge hao walipokuwa wakiwachagua wabunge wa Bunge la Afrika
Mashariki.
“Rushwa ilikuwa ni wazi wazi ukienda chooni unapewa laki mbili (Sh200,000) unaondoka,”alisema Suzan.
Alisema wao kama viongozi ambao wanatunga sheria
na wanatakiwa kuisimamia serikali wanapaswa kuwa waadilifu. Hata hivyo,
Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga (CCM), alisema hakuna ukweli
kuhusu jambo hilo la baadhi ya wabunge kuchukua rushwa hadi chooni.
Hata hivyo, Mbunge wa Tunduru, Mtutura Mtutura
(CCM), alimuunga mkono Suzan na kusema suala hilo ni la kweli na kwamba
kama Sanga hakuliona walikuwa wanamkimbia.
“Alichokizungumza Suzan ni cha kweli. Kaka yangu (Sanga) walikuwa wanakukimbia. Ni kweli hilo lilifanyika,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa APNAC, Vita Kawawa,
alisema si vyema wabunge wenye taarifa kuhusiana na masuala ya rushwa
wakatoa taarifa katika ofisi za Spika na kamati ya maadili ili liweze
kufanyiwa kazi mara moja.
“Ni vyema mkatupa taarifa kitu ambacho kinaashiria rushwa sisi tupo, ofisi ya spika ipo na kamati yetu ya maadili,”alisema.
Alisema rushwa ni mdudu ambao unatakiwa kukataliwa
na kila mtu. Alisema rushwa imesababisha maisha ya wananchi
kutobadilika ingawa uchumi wa nchi unakuwa.
No comments:
Post a Comment