Sunday, June 8, 2014

Mvutano mkali Bunge, Mahakama

Mwanasheria mkuu wa serikali Frederick Werema

Dodoma. Kitendo cha Mahakama kufungua milango kwa mawaziri na wabunge kufunguliwa mashtaka kutokana na kauli watakazozitoa bungeni ambazo ni kinyume cha Katiba na Sheria, kimeonekana kuwachanganya viongozi hao ambao wamesema kuwa wanalindwa na sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Wamesema licha ya kuwa kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria, Bunge kutunga na Serikali kusimamia sheria, nchi nyingi duniani wabunge wake wana kinga na hawashtakiwi kwa kauli watakazozitoa bungeni.
Kauli za wabunge hao zimekuja ikiwa imepita siku moja tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa msimamo huo wakati ikitoa uamuzi wa pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa ikimkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG, George Masaju.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake juzi ilikubaliana na baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali kesi hiyo, lakini ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa kwa kauli au jambo walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za binadamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, Naibu Spika Job Ndugai alisema, “Mahakama ikisema, imesema licha ya kuwa Katiba inaeleza wazi kuwa Bunge lipo huru.”
Alisema kuwa suala hilo linaweza kuwekwa sawa katika Katiba Mpya ambayo mjadala wake utaendelea Agosti mwaka huu.
“Nchi nyingi duniani wabunge wana kinga kwa kauli zao watakazozitoa bungeni. Kama hapa kwetu tumeamua hivyo ni sawa tu, ila mashtaka yatakuwa mengi kwelikweli,” alisema Ndugai.
Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla (CCM) alisema, “Sidhani kama tafsiri hii ni sahihi sana kwa sababu wabunge wanalindwa na Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.”
Kigwangalla alisema sheria hiyo ipo wazi kwamba mbunge akizungumza lugha isiyofaa mtu ambaye anataka kuchukulia hatua anatakiwa kuiandika barua Ofisi ya Bunge.
“Barua hiyo itakwenda kwa Spika wa Bunge na kama akiridhika atalipeleka suala hilo katika Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ambayo inaweza kumwita mlalamikaji ili kumsikiliza,” alisema Kigwangalla.
Alifafanua kuwa sheria hiyo haijawahi kufanyiwa marekebisho na kama mahakama imetoa tafsiri hiyo maana yake ni kwamba kesi za wabunge zitarundikana mahakamani.
“Wabunge kazi yetu ni kuzungumza na kama ni kushtakiwa basi tungekuwa tumeshtakiwa siku nyingi. Kwa tafsiri hii ya mahakama sijui itakuwaje, ngoja tuone hatua zipi zitafuata,” alisema Kigwangalla.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) alisema kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na kama imeamua hivyo hakuna wa kupinga.
“Kama Bunge halitaridhika lina mamlaka ya kutunga sheria kukazia uhuru wake, lakini kifupi ni kwamba huwezi kubishana na mahakama,” alisema.
Hata hivyo, Kafulila alisema kuwa uhuru wa mbunge unamfanya kuwa huru wakati akitoa mawazo yake, “Lengo la sheria ile ni kuwafanya wabunge kujadili hoja bila woga wala hofu yoyote na huo ndiyo mfumo wa nchi nyingi duniani, hata zile za Jumuiya ya Madola.”
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema, “Nadhani Mahakama imeshindwa kuitafsiri sheria hii kwa sababu lengo lake siyo kumfanya mbunge kuzungumza chochote bali kumpa uhuru na kujadili kitu bila woga wowote.”
Alisema tafsiri hiyo ya Mahakama italifanya Bunge kukosa meno na wabunge watashindwa kujadili jambo kwa kutoa mifano halisi inayoleta msisimko na wakati mwingine kuibua mambo yaliyojificha.
“Nchi za Jumuiya ya Madola na nyingine nyingi duniani zinatumia mfumo huu wa mbunge kuwa na kinga. Hiyo ni tafsiri ya mahakama ila sisi tunajua kuwa tuna kinga na kama Bunge likikosa kinga afya yake itakuwa mbovu,” alisema Lugola.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kapteni Mstaafu John Chiligati, alisema hajauona huo uamuzi wa Mahakama.
Hata hivyo, alisema Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria kuu imetoa uhuru kamili wa mbunge kutoa mawazo yake akiwa bungeni na kwamba mawazo anayotoa mbunge akiwa bungeni hayawezi kuhojiwa na chombo chochote nje ya Bunge.
Alisema ibara ya 100 ya Katiba imetoa uhuru wa majadiliano ya mbunge ndani ya Bunge na kwa kadiri ilivyotafsiriwa katika sheria ya Haki, Madaraka na Kinga siyo rahisi kwa mbunge kukamatwa akiwa bungeni kwa maneno anayotoa kwani kinga aliyonayo ni ya kikatiba.
“Mbunge anaweza kukamatwa na kushtakiwa akiwa bungeni kwa kosa au makosa ya jinai tena kwa idhini ya Spika, yaani mkamataji atatakiwa kuwa na idhini ya Spika ili kumkamata mbunge akiwa bungeni akifanya kosa la jinai,”alisema Chiligati.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso, alisema ingawa Katiba ya nchi imetoa uhuru wa kuzungumza bungeni lakini hakuna uhuru usio na
“Kinga waliyopewa wabunge ni katika utekelezaji wa majukumu yao. Hakuna uhuru ambao hauna mipaka, ni lazima wananchi waelewe hilo,” alisema Cecilia ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Hata hivyo, alisema kanuni za Bunge zimetoa mwanya kwa mtu ambaye hajaridhika na maneno ama matamshi ya mbunge kuwa anaweza kuwasilisha malalamiko yake na yakasikilizwa na Bunge.
Serikali imekuwa ikivutana mara kadhaa na mhimili mwingine wa mahakama katika baadhi ya masuala ambayo yanagusa Katiba.
Katika kesi hiyo, LHRC na TLS walikuwa wakidai kuwa Pinda alivunja Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Hivyo, walikuwa wakiiomba mahakama, pamoja na mambo mengine, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda aifute hadharani.

Mtikila

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila mwaka 1993 alifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, akiiomba mahakama itamke kuwa kifungu kilichopo katika katiba kinachozuia mgombea binafsi ni kinyume cha haki za binadamu.
Katika hukumu yake Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Kahwa Lukangira (kwa sasa ni marehemu), alikubaliana na Mtikila wagombea binafsi waruhusiwe kushiriki kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi.
Hata hivyo, Serikali ilipeleka muswada bungeni wa kuzuia mgombea binafsi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment