Sunday, June 1, 2014

VODACOM KUTENGENEZA AJIRA ZAIDI YA 400 KUPITIA MADUKA YAO‏

Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Rejareja wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Upendo Richard (kushoto) akimkabidhi Meneja wa duka jipya la huduma kwa wateja la Vodacom Sinza Afrika Sana, Swaum Manengelo funguo ya duka hilo kuashiria ufunguzi rasmi wa duka hilo kuanza kutoa huduma kwa wateja. Akishuhudia tukio hilo katikati ni Meneja Uhusiano wa Nje wa kampuni hiyo, Salum Mwalim. Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

 Meneja wa duka jipya la huduma kwa wateja la Vodacom lililopo Sinza Afrika Sana jijini Dar es Salaam, Swaum Manengelo akifungua mlango kuashiria ufunguzi rasmi wa duka hilo. Wakishuhudia tukio hilo ni Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Rejareja Upendo Richard (kushoto) na Meneja Uhusiano wa Nje wa kampuni hiyo Salum Mwalim (kulia).

Mkuu wa Idara Mauzo ya rejareja wa Vodacom Tanzania, Upendo Richard akikagua huduma na bidhaa mbalimbali ndani ya duka jipya la huduma kwa wateja lililopo Sina Afrika Sana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuzinduliwa rasmi hivi karibuni. Hilo ni duka la 18 la huduma kwa wateja Wilayani Kinondoni na la 79 nchi nzima.

 
- Ni kupitia maduka mbalimbali ya Vodacom yaliyokwisha kufunguliwa hadi sasa
Dar es Salaam, Kampuni ya mawasiliano nchini ya Vodacom imendelea na azma yake ya kuhakikisha inawafaidisha wateja wake kupitia huduma zake huku wakitengeneza nafasi za ajira kupitia maduka yake yanayoendelea kufunguliwa nchi nzima.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Rejareja, Upendo Richard wakati akizindua duka jipya la Vodacom maeneo ya Sinza Afrika Sana ambalo linakuwa ni la 18 kwa wilaya ya Kinondoni pekee na la 79 Tanzania nzima.
“Dhamira kubwa ya kusambaza maduka haya ni kusogeza na kuboresha huduma kwa wateja wetu popote walipo lakini pia tunawatengeneza watanzania nafasi za ajira. Ajira hizi kwa namna moja au nyinigine ni suluhu la upungufu wake nchini na pia hupunguza mzigo kwa serikali katika jitihada za kuhakikisha watu wanajiajiri wenyewe.” Alisema Bi. Richard
Ameendelea kuwa kwa kila duka la Vodacom linalofunguliwa, watu watano mpaka saba huajiri kwa nafasi kama vile za; meneja wa duka, uhasibu, wauzaji simu, watoaji ushauri kwa wateja  pamoja na wakala wa M-Pesa. Amesema kuwa duka hili likiwa ni la 79 kufunguliwa nchi nzima, takwimu zinaonyesha kuwa kuna takribani idadi ya wafanyakazi zaidi ya 400 wanafanya kazi katika maduka yote ya Vodacom yaliyosambaa nchi nzima.
“Wateja wote wa Vodacom sasa wasipate tabu za kwenda maeneo ya mbali kutafuta huduma za kimawasiliano badala yake watumie duka hili lililopo hapa Sinza Afrika Sana.” Alisema Bi. Richard na kuongezea, “Huduma zinazotolewa hapa ni sawa na maduka mengine ili kuweza kutimiza haja zao na kuepukana na usumbufu wa kwenda maeneo kama Mlimani City, Quality Center. Mkifanya hivyo mtasababisha msongamano wa watu hali ambayo inapelekea na foleni ambazo zinasababisha kuchelewa kupata huduma.”
Nae mteja wa kwanza kutumia duka hilo mara baada ya kufunguliwa rasmi, Alfred Joseph, ambaye ni mkazi wa Sinza Afrika Sana  ameishukuru Vodacom kwa jitihada zao za kusogeza huduma kwa wateja na kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.
“Kabla ya kufunguliwa kwa duka hili, tulizoea kwenda Mlimani City kufuata huduma ambapo ilikua ni changamoto kubwa sana. Kwa mfano kwetu sisi wafanyakazi, muda mwingine unakuwa umetoka kazini umechoka halafu unahitaji huduma kwa uharaka lakini unashindwa kuzifikia mpaka uanze safari ya kwenda Mlimani City. Kwa kweli ulikua ni usumbufu mkubwa sana, tunashukuru kwa kuliona hilo na kulifanyia kazi na sidhani kama nitasumbuka tena kwenda huko.” Alisema mkazi huyo
Akitoa machache wakati wa uzinduzi Meneja wa duka hilo, Swaum Manengelo amebainisha shukrani zake za dhati kwa Vodacom kwa ushirikiano waliouonesha mpaka duka hilo linakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wateja.
“Naweza kusema ndoto ya wakazi wa Sinza Afrika Sana kuwa na huduma za Vodacom karibu yao zimetimia, ufunguzi wa duka hili ni ushahidi tosha. Ningependa kuwakaribisha wateja wote wa kutoka maeneo haya na ya jirani kutembelea dukani hapa na kuhudumiwa.” Alisema Bi. Manengelo, na kumalizia, “Ningependa kuwatoa hofu wateja wetu wasihofie ubora wa huduma na bidhaa zinazopatikana hapa kwani wengi hudhani labda huduma zinazotolewa Mlimani City au Quality Centre ni bora zaidi, hilo si kweli na nathubutu waje kujaribu leo.”

No comments:

Post a Comment