Thursday, June 19, 2014

UBUNGO MATAA KUFUNGWA KUPISHA UJENZI WA BARABARA

Muonekano wa daraja Kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar.

KAMPUNI ya ujenzi ya Strabag  inayojenga barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) imetangaza mabadiliko ya muda katika eneo la Ubungo jijini Dar es salaam kuanzia kesho na kesho kutwa usiku kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Bwana Yahya Mkumba, alisema  kazi hiyo itahusu ujenzi katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam
Nujoma na Nelson Mandela katika eneo la Ubungo.
Alisema ujenzi huo utakaoanza leo utasababisha kufungwa kwa baadhi ya njia katika barabara hizo kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi keshokutwa Jumamosi.
Akielezea zaidi alisema katika awamu ya kwanza ujenzi huo utahusisha eneo la upande wa kulia la makutano la barabara ya Sam Nujoma na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na Tabata kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma watakapofika taa za Ubungo,” alisema.
Alifafanua kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama zitakazowaelekeza kupita katika barabara za mradi zinazojengwa hadi barabara ya Shekilango ambapo wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa kutumia barabara ya Igesa.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea Sinza kupitia barabara ya Igesa hayataweza kuelekea eneo la Ubungo yatakapofika katika makutano ya barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua kuwa magari yanayotumia barabara ya Morogoro kutokea maeneo ya Mbezi na Kimara yatalazimika kuchepuka kulia na kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka yatakapofika eneo la Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Bw. Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la upande wa kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela litafungwa siku ya Jumamosi kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi siku ya Jumapili.
Katika awamu hii, alisema, watumia magari yatakayokuwa yanatokea eneo la Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika kuchepuka kushoto kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea barabara ya Nelson Mandela na kutaka kuelekea mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika kuchepuka kushoto na kwenda kugeukia eneo la Kibo ili kuikamata barabara ya Morogoro.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema Bwana Mkumba na kuongeza kuwa pamoja tunajenga na hivyo usumbufu utakuwa ni wa muda mfupi.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa usafiri.
Ubungo Tabata Diversion

No comments:

Post a Comment