Dar es Salaam. Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume
wa mwimbaji nguli wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha amejitokeza
hadharani na kusema kwamba atakwenda polisi mwenyewe kujibu tuhuma dhidi
yake za kumbaka shemeji yake mwenye umri wa miaka 17.
Faili la tuhuma dhidi ya Mbasha lilifunguliwa
Jumatatu iliyopita katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule) wakati
shemejiye huyo (jina tunalihifadhi), alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka
mara tatu kwa siku mbili tofauti. Kesi hiyo ilipewa namba
TBT/RB/3191/2014 na TBT/IR/1865/2014.
Tangu siku hiyo, polisi imekuwa ikieleza kuwa
inamsaka Mbasha bila ya mafanikio lakini mwishoni mwa wiki mtuhumiwa
huyo aliongea na gazeti hili na kuelezea upande wake wa tukio hilo na
kwamba yuko tayari kujisalimisha ili ukweli ubainike.
“Tuhuma dhidi yangu ni za kutengeneza,” alisema
Mbasha na kufafanua kuwa yote hayo yanatokana na mgogoro wa kifamilia
baina yake na Flora na familia yake ambao alisema umedumu kwa siku
kadhaa.
“Mimi sijabaka na sijawahi kubaka; sijatenda
dhambi yoyote; sijafanya kitu chochote na kibaya haya mambo yote ni ya
kusingiziwa tu. Mungu wangu ni shahidi. Na kwa kuwa sijafanya hiyo
dhambi kama wanavyodai, basi Mungu wangu atanitetea,” alisema Mbasha
ambaye anaonekana zaidi kwenye video ya wimbo wa Maisha ya Ndoa
alioshirikiana na mkewe Flora.
“Si wamesema wananitafuta, nitakwenda mwenyewe
polisi. Nitawasikiliza na nitatoa maelezo yangu. Kama wakinipeleka
mahakamani basi ukweli utajulikana... ipo siku kila kitu kitakuwa wazi.”
Kabla ya kufunguliwa kwa faili la tuhuma hizo,
msichana huyo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Ilala (Amana)
ambako alifunguliwa faili la matibabu namba 667. Matokeo ya vipimo
ambavyo vilifanywa na daktari kung’amua kama binti huyo aliingiliwa
vinaonyesha kuwa kulikuwa na mbegu utokaji wa mbegu usio wa kawaida
(HVD).
Kadhalika binti huyo alifanyiwa vipimo kuona kama
ameambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU), pia kupata ujauzito, lakini
matokeo ya awali yalionyesha kuwa yupo salama.
Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu usiku,
binti huyo aliliambia gazeti hili kwamba mara ya kwanza alibakwa mchana
Mei 23 na kwamba mtuhumiwa alirudia kitendo hicho Jumapili Mei 25 usiku
ndani ya gari katika eneo la Tabata, ambako anadai alifanyiwa kitendo
hicho mara mbili.
Hata hivyo, Mbasha alihoji: “Hivi kweli hata kama
mimi ni mbakaji, kweli nimbake mtoto wa kumlea mwenyewe mara tatu, yaani
Ijumaa halafu nirudie tena Jumapili? Hata kama ni kusingiziwa basi
tuhuma hizi zimezidi.”
“Huyu binti nimekaa naye miaka mingi na sijawahi
kumfanyia hivyo. Hapo nyumbani kwangu wamekaa mabinti wengi, wakiwamo
shemeji zangu wadogo zake na Flora na sikuwahi hata kuwagusa, leo hii
kwa nini wananifanyia hivi?”
Mgogoro wa familia
Mbasha alidai kwamba chanzo cha kusingiziwa kwake ni mgogoro
baina yake na mkewe Flora, ambao umesababisha mgawanyiko mkubwa ambao
umefanya achukiwe na familia nzima ya mkewe.
“Yako mambo mengi tu ambayo yanahusu familia, kwa
hiyo ilifika mahali mimi na Flora tukawa hatuishi kwa amani na hata hili
jambo limetokea wakati tukiwa na mgogoro huo. Hivyo Flora na ndugu zake
waliamua kumlisha binti huyo maneno ili mimi nifungwe,” alisema Mbasha.
Hata hivyo, Flora hakutaka kuingia kwa undani
katika suala hilo, akisisitiza kuwa Mbasha bado ni mumewe na kwamba
yaliyotokea awali alishamsamehe, lakini akamtaka ajitokeze kutoa maelezo
polisi.
“Mimi nilishamwambia kwamba hata kama alifanya au
hakufanya, nilishamsamehe kutoka ndani ya moyo wangu maana yeye ni mume
wangu wa ndoa na Mungu wangu ni shahidi, lakini kuna suala la kisheria
polisi ambalo mimi siwezi kuliingilia,” alisema Flora ambaye alitamba na
wimbo wa injili wa “Tanzania” ambao ulimfanya aalikwe katika shughuli
mbalimba za kitaifa.
“Tatizo linakuwa kubwa kwa sababu yeye mwenyewe
haonekani na taarifa ni kwamba amekimbia,” alidai Flora. “Sasa kama
kweli hajafanya kitendo hicho, kwa nini anajificha? Ajitokeze... aende
polisi na huko ndiko akatoe maelezo yake. Kuzungumza na vyombo vya
habari haisaidii kabisa.”
Mwimbaji huyo, ambaye ni mjukuuu wa muhibiri
maarufu wa Injili, Askofu Moses Kulola alisema yeye hana uwezo wa
kuingilia kesi hiyo kwani hakuhusika kwa namna yoyote ile kupeleka suala
hilo polisi kwa sababu hakuwapo wakati likitokea na kwamba linasimamiwa
na familia.
“Inawezekana anatamani nikafute kesi polisi, mimi
sina uwezo huo kwa sababu ni suala la kisheria na tuhuma zenyewe ni za
kijinai. Pili familia yenye mtoto ndiyo inafuatilia kesi hiyo, lakini
hilo halifuti msamaha wangu kwake,” alisisitiza.
Kauli ya Flora kwamba ameshamsamehe mumewe
inafanana na ya Mbasha ambaye pia alisema kwamba kama kuna jambo ambalo
mkewe alimkosea, hana tatizo na kwamba alishamsamehe.
“Flora ni mke wangu, mke wa ujana wangu,
ninampenda asilimia 100 na yeye analifahamu hilo, lakini sijui ni kitu
gani kimemkuta? Sijui ni nini kimeingilia ndoa yetu?” alisema Mbasha.
Alisema ameshampigia simu mkewe mara nne akitaka
waonane ili wazungumze, lakini hakuonyesha utayari, kauli ambayo Flora
aliikanusha akisema: “Hajanitafuta maana tangu Jumatatu hapatikani
kwenye simu.”
Mwenendo wa upelelezi
Wakati hayo yakiendelea, maendeleon ya kesi hiyo
yanasuasua baada ya faili kutokupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni kutoka
Tabata kwa ajili ya hatua zaidi.
Baadhi ya wanafamilia wa mtoto anayedaiwa kubakwa walisema
jalada hilo lingefikishwa Buguruni Jumatano jioni, lakini kutokana na
ofisa anayeshughulikia kesi hiyo kuwa na udhuru, ilishindikana.
Mjomba wa Flora ambaye amepewa jukumu la kusimamia
kesi hiyo, alisema wamekuwa wakifuatilia Kituo cha Polisi cha Tabata
tangu tukio hilo liliporipotiwa, lakini wakaelezwa kuwa kesi hiyo
itahamishiwa Buguruni.
“Tuliambiwa lile faili lazima lihamie kituo cha
Buguruni. Nilifika hapa nikaonana na kamanda wa polisi wa wilaya ambaye
ametupokea vizuri na kuonyesha moyo wa kutusaidia,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Ilala, Marietha Minangi
alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa kesi hiyo na kwamba hafahamu
taarifa kuwa faili hilo linacheleweshwa kuhamishiwa Buguruni.
“Tunaendelea kuchunguza, ila siyajui hayo masuala ya faili yanayotoka
kinywani mwako. Lakini nimepata taarifa kuwa bado wanachunguza,” alisema
Minangi.
Mwanzoni mwa wiki jana, Kamanda Minangi alisema
kuwa maofisa wake walikuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa na kwamba
walienda mpaka nyumbani kwake, lakini hawakumkuta.
“Nimefuatilia ni kweli hiyo kesi imefunguliwa na
maofisa wangu wameniambia walienda nyumbani kwake na hawakumkuta mtu.
Waliniambia walikaa pale kwa takribani dakika 20 na ile nyumba ina fence
(uzio) na geti waligonga kengele, lakini hakuna mtu aliyekuja kufungua.
“Na baadaye waliwauliza majirani, nao wakasema
hawafahamu mtu huyo alipo. Inaonekana ametoweka, lakini sisi kama
wasimamizi wa sheria tunaendelea kumtafuta mpaka tutakapomkamata,”
alisema Minangi.
Ustawi wa Jamii
Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu na Idara ya
Ustawi wa Jamii ya Manispaa ya Ilala kujua usalama na matibabu ya binti
huyo. Ofisa ustawi wa jamii anayeshughulikia ulinzi na usalama kwa mtoto
wa manispaa hiyo, Fransica Makoye alisema kuwa wanalishughulikia suala
hilo kama mengine katika kutafuta haki na usalama wa mtoto na wala
hawahusishi na umaarufu wa wahusika.
“Sisi tunafuatilia kama alipata tiba sahihi mara
baada ya tukio la kubakwa na kufahamu mahali ambako anakaa kwa ajili ya
usalama wa huyo mtoto. Tumeiona PF3 haionyeshi kama alipata matibabu,
lakini tutawajulisha zaidi kinachojiri kwa kuwa tutaenda Hospitali ya
Amana kwa maelezo zaidi,” alisema Makoye.
No comments:
Post a Comment