Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya Ilala Bw. Raymond Mushi akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanzishwa kwa
mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara wa soko la Mchikichini walioathiriwa
na janga la moto kwa lengo la kurejesha hali ya maisha waliyokuwa nayo
hapo awali.
Mmoja wa waanzilishi wa mfuko
wa kuwasaidia waathirika wa moto soko la Mchikichini ambaye pia ni
Meneja wa Vituo vya mizigo vya nchi kavu wa Kampuni ya AZAM Bw. Raymond
Adolph akieleza namna walivyoguswa na tukio la moto lililotokea katika
soko hilo na kuwaomba watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara
wa soko la Mchikichini Bw. Jumanne Kongolo akiongea na waandishi wa
habari kuishukuru serikali na wananchi waliojitokeza kufungua mfuko wa
kuwasaidia waathirika wa moto katika soko hilo.
Baadhi ya wafanyabiashara wa
soko la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto wakifuatilia masuala
mbalimbali ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam wakati wa uzinduzi
wa mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wamejitokeza kuanzisha
mfuko maaluum wa kuwasaidia wafanyabiashara wapatao 5700 wa soko la
Mchikichini walioathiriwa na janga la moto lililotokea usiku wa kuamkia
tarehe 12 mwezi huu eneo la Karume,jijini Dar es salaam.
Akaunti hiyo maalum inayojulikana kwa jina la Mkono wa Pole Chinga
2014 imefunguliwa katika Benki ya CRDB Tawi la Lumumba ili kuwawezesha
wadau mbalimbali wanaoguswa na tukio hilo kutoa mkono wa pole kupitia
akaunti namba 0152270491300.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya
Ilala Bw. Raymond Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es salaam amesema kuwa mfuko huo unalenga kurejesha hali ya maisha
waliyokuwa nayo wafanyabiashara hao hapo awali kabla ya kuungua kwa
vibanda na bidhaa zao.
Amesema akaunti hiyo itasimamiwa kwa pamoja na wawakilishi kutoka
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, wadau waanzilishi na
wafanyabishara walioathirika.
“Tumeanzisha akaunti hii kutokana na wananchi kuguswa na tukio hili
kwa kuonesha nia thabiti ya kutaka kutoa mkono wa pole kwa waathirika wa
janga hili, nachoweza kusema jambo hili tumeliwekea utaratibu na
tutaliendesha kwa uwazi mkubwa kwa kushirikiana na wahusika wa tukio”
amesema Bw. Raymond.
Aidha, amefafanua kuwa serikali kupitia Manispaa ya Ilala ambayo soko
hilo liko chini yake itahakikisha inaboresha hali ya miundombinu katika
soko hilo zikiwemo barabara za kuwezesha magari na vifaa vya uokoaji
kupita wakati wa majanga ya moto huku akiwataka wafanyabiashara hao
kutojenga na kuzuia maeneo ya barabara katika soko hilo.
Mmoja wa waanzilishi wa mfuko huo ambaye pia ni Meneja wa Vituo vya
mizigo vya nchi kavu vya vya Kampuni ya AZAM Raymond Adolph ameeleza
kuwa yeye kama mfanyakazi na wafanyakazi wengine wameguswa na tukio la
moto lililotokea katika soko hilo na kufafanua kuwa kiasi cha fedha
kitakachopatikana kitakabidhiwa kwa walengwa kwa uwazi huku akiwaomba
watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
“Akaunti hii tuliyoifungua itakuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na
kiasi tutakachopata tutakikabidhi kwa wahusika kwa uwazi na tunawaomba
watanzania wajitokeze ili kwa pamoja tuwasaidie ndugu zetu hawa
waliopata matatizo” amesisitiza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara hao ambaye pia
aliathiriwa na moto huo Bw. Jumanne Kongolo ameeleza ameishukuru
serikali na wananchi waliojitokeza kufungua mfuko huo kwa lengo la
kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika na moto huo.
No comments:
Post a Comment