Coutinho akiwa katika pozi.
KIUNGO mshambuliaji wa Kibrazili, Andrey Coutinho,
aliyetua jana (Ijumaa), kutoka nchini humo kuja kukipiga kwenye timu ya
Yanga, jana alitua na mkosi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, baada ya gari lililoenda
kumchukua kufungwa nyororo na wasimamizi wa maegesho ya magari uwanjani
hapo.
Katika sakata hilo mchezaji huyo baada ya kutua uwanjani, alipokelewa
na viongozi na mashabiki wa timu hiyo wakiwemo Meneja wa timu hiyo,
Afidh Saleh, Msemaji, Baraka Kizuguto, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
timu hiyo, Mohammed Binda na viongozi wengine na mashabiki wa timu na
kuongozwa moja kwa moja kwenye gari aina ya Toyota Alteza aliloandaliwa
kumpeleka kwenye klabu ya timu hiyo.
Muda mfupi kabla ya mchezaji huyo kuingia kwenye gari hilo, kundi
lililokwenda kumpokea mchezaji huyo liligundua kuwa gari hilo limefungwa
nyororo na wasimamizi wa maegesho ya uwanja huo hivyo kushindwa
kuondoka.
Kitendo hicho kilisababisha mchezaji huyo kupigwa na butwaa lakini
akaamua kuingia ndani ya gari hilo na kujipumzisha wakati viongozi wa
Yanga wakihaha kuwasaka waliolifunga gari hilo.
Akizungumza na Championi wakati sakata hilo
likiendelea msemaji wa timu hiyo (Kizuguto), alisema anashangaa
wasimamizi wa maegesho hayo kulifunga nyororo gari lao wakati sehemu
waliyopaki waliekezwa na afisa mmoja wa polisi mwenye nyota moja.
“Mimi nawashangaa hawa jamaa, sisi tusingeweza kupaki hapa bila
kuelekezwa, kuna afisa mmoja wa polisi mwenye nyota moja ndiye
aliyetuelekeza tupaki hapa tena ndiye yule aliyeongoza mapokezi ya
Maximo jana (Alhamisi), mbona hata gari lililomchukua Maximo nalo
lilipaki hapahapa?” Aliuliza Kizuguto huku akilalamika.
Wakati Kizuguto akisema hayo kundi la mashabiki wa Yanga waliofika
kwenye mapokezi, lilikuwa likipiga mayowe na kusema aliyelifunga gari
hilo ni lazima atakuwa ni mtu wa timu ya Simba na alifanya hivyo
makusudi maalum kwani baada ya kulifunga gari mtu huyo alipotea ambapo
juhudi za kumsaka zilichukua zaidi ya dakika ishirini.
Baada ya sakata hilo kutaka kuleta sura ya vurumai kutoka kwa
mashabiki waliokuja kumpokea mchezaji huyo baadhi ya maofisa wa uwanja
huo walikubaliana kulifungulia gari hilo ambapo faini yake ya kuegesha
sehemu hiyo ingegharimu shilingi elfu ishirini.
No comments:
Post a Comment