ZAIDI
ya nyumba 700 zilizopo kando ya barabara ya Arusha-Moshi, zitabomolewa
kupisha ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha hadi mpaka wa Holili, kwa
upande wa Tanzania na Taveta hadi Voi nchini Kenya.
Akizungumza
kwenye uzinduzi wa barabara hiyo jana, Meneja wa Wakala wa
Barabara(Tanroads) Mkoa wa Arusha, Deusdedit Kakoko, alisema mradi huo
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), utaanza
kutekelezwa kabla ya Desemba mwaka huu.
Alisema
tayari wenye nyumba ambazo zitabomolewa, wameshataarifiwa juu ya suala
hilo. Aliwataka wananchi ambao wameshalipwa fidia zao, kuondoa majengo
yao, kabla ya kubomolewa na wakala huo.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliwataka wananchi wa Arusha kutoa
ushirikiano wa kutosha kwenye ujenzi wa barabara hiyo, kutokana na
umuhimu wake kiuchumi.
“Mradi
huu una umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya mkoa wa Arusha, hivyo
wananchi wanatakiwa kuunga mkono ili uweze kukamilika kwa wakati,”
alisema Mulongo.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, alisema ujenzi
huo unahusisha upanuzi wa barabara ili iwe na njia nne kutoka eneo la
Sakina hadi Usa River.
Mfugale
alisema mradi huo, utatekelezwa kwa awamu mbili, ikiwemo Sakina-Tengeru
(km 14.2) na barabara ya pembeni mwa jiji la Arusha (km 42).
Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa kipande cha Tengeru-Usa River (km 8.1) na kisha marekebisho ya barabara hiyo hadi Holili.
Mfugale
alisema ujenzi wa barabara hiyo na nyingine ni sehemu ya Mpango wa
Uendelezaji wa Mtandao wa barabara za Afrika, ambao nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) waliuandaa.
Mhandisi
Mwandamizi wa masuala ya Uchukuzi kutoka AfDB, Patrick Musa, alisema
barabara ya Arusha-Holili/Taveta-Voi, itakuza biashara mingoni mwa nchi
wanachama wa EAC.
No comments:
Post a Comment