Kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza
mkoani Tanga, Ally Mkufya (60), anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi
shingoni.
Mkufya ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya
Wilaya hiyo, alijipiga risasi jana alfajiri akiwa chumba alichokuwa
akiishi kwenye baa yake ya Tete Pub Extra ambayo pia ina sehemu ya
nyumba ya kulala wageni, iliyopo pembeni ya barabara ya kwenda Tanga
mjini.
Kigogo huyo wa CCM ambaye pia ni mfanyabiashara anayemiliki baa kadhaa,
anadaiwa kukatisha maisha yake kwa kujipiga risasi shingoni wakati huo
akiwa amejifungia chumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, akizungumzia kifo
hicho alisema uchunguzi unafanyika ili kujua chanzo cha kujiua kwa
kujipiga risasi ingawa baadhi ya watu wanasema kifo hicho kimetokana na
sababu za kifamilia zilizomfanya ahame nyumbani kwake na kuishi baa kwa
muda mrefu.
Viongozi wa chama wilayani humo akiwamo Mwenyekiti Peter Jambele, Katibu
Mwenezi , Makame Seif na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Muheza, Josephin
Mbezi, walielezea kusikitishwa na kifo hicho walichosema ni kibaya.
Awali akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mlinzi wa baa hiyo, Idd
Abdallah, alisema alipoingia kazini juzi jioni hakukutana na mwajiri
wake licha ya kwamba alikuwa na kawaida ya kukaa nje hadi usiku baa
inapofungwa.
Alieleza kuwa aliingiwa na hofu na kuwauliza wahudumu, lakini alijibiwa
kuwa bosi wao amejipumzisha chumbani kwake kwa kuwa anajisikia homa na
kwamba hali iliendelea hivyo hadi muda wa kufunga baa ulipofika na
wahudumu kuondoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa ilipofika asubuhi wahudumu walifungua baa na
kufanya usafi, lakini cha kushangaza Mkufya alikuwa hajaamka jambo
ambalo halikuwa kawaida yake kulala hadi wakati huo.
Hofu hiyo iliwafanya kugonga mlango, lakini haukufunguliwa hivyo kulazimika kuwapigia simu ndugu zake ili waje kwenye baa hiyo.
Abdallah alisema walipofika chumbani kwake walivunja mlango na kumkuta
amekufa kwa kupigwa risasi shingoni na bunduki aina ya Short ikiwa
pembeni yake huku damu zikiwa zimetapakaa chumba kizima.
Alisema walipiga simu polisi na askari walifika kuuchukua mwili wa
marehemu hadi hospitali Teule wilayani Muheza ambako umehifadhiwa.
KAULI YA MKEWE
NIPASHE ilifika nyumbani kwa marehemu jana na kumkuta mkewe, Anna
Mkufya, akiwa katika majonzi makubwa. Hata hivyo, hakuwa tayari
kuzungumza lolote juu ya tukio hilo.
Marehemu ameacha watoto watano na anatarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Semgao wilayani Muheza.
SOURCE:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment