Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.
KAWE ndiyo jimbo lenye vitega uchumi vingi na vikubwa vinavyoliingizia
taifa pato kubwa. Hili ni moja kati ya majimbo kadhaa ya uchaguzi jijini
Dar es Salaam, likiwa na eneo kubwa la fukwe za Bahari ya Hindi
lililoambaa kuanzia katikati ya jiji mpaka maeneo ya Msasani, Kawe,
Kunduchi mpaka Mbweni.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Kama kawaida, Gazeti la Uwazi limeingia katika mitaa mbalimbali ya
kata kumi za jimbo hili tajiri lenye mahoteli mengi ya kitalii, viwanda
vikubwa, ofisi za mashirika na makampuni makubwa, balozi za nchi kadhaa
kubwa ikiwemo Ubalozi wa Marekani na maofisi mengi ya serikali.
Katika ziara hiyo iliyochukua siku kadhaa katika jimbo hili
linaloongozwa na Mhe. Halima James Mdee kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Uwazi limebaini matatizo mengi
yanayowakabili wananchi, kubwa likiwa ni migogoro sugu ya ardhi
inayotishia usalama wa raia na mali zao.
MATATIZO YA WANANCHI
Ukiachilia mbali migogoro
ya ardhi inayolikabili Jimbo la Kawe, ukiwepo ule mkubwa na sugu wa
Kijiji cha Chasimba kilichopo katika Kata za Wazo na Bunju ambapo
wananchi wa eneo hilo wanavutana na mwekezaji wa Kiwanda cha Saruji cha
Twiga (Wazo Hill),
mgogoro mkubwa uliowahi kusababisha vifo vya mabaunsa wa Madale na
mgogoro mwingine wa machimbo ya kokoto ya Mtongani, Kunduchi, Uwazi
limebaini matatizo mengine kadhaa yanayowakabili wananchi wa jimbo hili.
Matatizo hayo ni: Ukosefu wa huduma bora za kijamii zikiwemo maji
safi, hospitali na umeme, ukosefu wa ajira kwa vijana wengi na matukio
ya kihalifu yanayotingisha maeneo mengi hasa katika Fukwe za Bahari ya
Hindi maeneo ya Kawe, Msasani na Kunduchi.
Matatizo mengine ni ukosefu wa miundombinu bora kama barabara na
madaraja, ukosefu wa vyumba vya kutosha vya madarasa, walimu wa kutosha
na vifaa vya kujifunzia na kufundishia yakiwemo madawati,
uporaji wa viwanja vya wazi vilivyotengwa na serikali, ujenzi holela
wa ‘mahekalu’ kwenye maeneo ya fukwe za Bahari ya Hindi, kwenye uoto
asili wa mikoko, ujenzi kwenye mikondo ya maji unaosababisha mafuriko
wakati wa mvua na mgogoro wa makazi na mafao kati ya waliokuwa
wafanyakazi wa Kiwanda cha Tanganyika Packers kilichopo Kata ya Kawe na
serikali.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kuwahoji wananchi wa
maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na kueleza matatizo yanayowakabili,
Uwazi lilimsaka Mbunge Halima Mdee na kutaka kufahamu namna alivyotimiza
ahadi zake alizozitoa wakati wa uchaguzi na jinsi anavyoshughulikia
kero na matatizo yanayowakabili wapiga kura wake.
Jitihada za kumtafuta, ziligonga mwamba baada ya kumweleza mwandishi
kwa njia ya simu kwamba alikuwa Dodoma kwenye Bunge la Bajeti ya
Serikali 2014/15 na badala yake, akaelekeza kuwa majibu ya maswali yote
yatatolewa na katibu wake kwa niaba yake.
Uwazi lilisaga lami hadi Magomeni Usalama kwenye ofisi za mbunge huyo
na kufanikiwa kukutana na makatibu wawili kati ya watatu wa mbunge
huyo, Martha Mtiko na Edward Simbeye ambao walikuwa na maelezo
yafuatayo:
1. MIGOGORO YA ARDHI
Kupitia kwa makatibu wake
hao, mbunge alikiri kuijua migogoro ya ardhi inayowasumbua wapiga kura
wake, ukiwemo wa Kijiji cha Chasimba.
“Ni kweli kuna mgogoro mkubwa katika kijiji hicho, mwekezaji alienda
mahakamani na kuwashitaki wananchi kwa madai kuwa wamevamia eneo lake,
hukumu ikapita kwamba wananchi walipwe fidia na kuhamishwa lakini
mheshimiwa mbunge ameendelea kuwapigania wananchi kwa nguvu zote kwani
Kijiji cha Chasimba kipo pale kisheria na kilisajiliwa mwaka 1975.
“Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka anafahamu kila kitu na yeye amekuwa akichangia kwa kiasi
kikubwa kuuchochea mgogoro huo kwa kutoa maamuzi yenye kutia shaka,
likiwemo suala la wakazi wa eneo hilo kulipwa fidia zao ambapo mchakato
mzima umeendeshwa kwa ujanjaujanja na kuibua hasira kali kwa wananchi,”
alisema Mtiko kwa niaba ya Mdee.
Akizungumzia mgogoro mwingine wa mipaka kati ya wachimba kokoto,
wakazi wa Mtongani (Kunduchi) na kambi ya jeshi, katibu mwingine wa
mbunge, Simbeye alisema Mdee amejitahidi kulishughulikia suala hilo
mpaka jeshi likaamua kurekebisha mipaka yake.
“Mpaka sasa mgogoro ule ambao ulisababisha maafa makubwa umemalizika
kwa jitihada za mbunge na wananchi na wanajeshi wanaishi kwa amani
isipokuwa kuna mgogoro mwingine ndani ya eneo hilohilo unakaribia
kulipuka kwani manispaa inadai eneo hilo ni lake kisheria na wakati
huohuo linawaachia wananchi wanaendelea kujenga, hilo nalo mheshimiwa
analishughulikia,” alisema Simbeye.
2. VITENDO VYA KIHALIFU UFUKWENI
Ofisi ya mbunge
ilikiri kulifahamu tatizo hilo na kueleza kwamba mbunge amejitahidi kwa
kadiri ya uwezo wake kulishughulikia lakini anakwamishwa na utendaji
mbovu wa jeshi la polisi kwani licha ya wananchi na mbunge kutoa taarifa
mara kwa mara juu ya makundi yanayoendesha uhalifu huo hasa nyakati za
jioni, wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua za haraka.
3. HUDUMA ZA KIJAMII
“Mbunge amejitahidi sana
kuboresha huduma za kijamii, ukiachilia mbali fedha za bajeti
zinazotengwa na zile za mfuko wa jimbo, mheshimiwa pia amefikia hatua
mpaka ya kutoa fedha zake za mfukoni ili kuboresha huduma za kijamii
ikiwemo kununua madawati na vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa
ajili ya shule mbalimbali.
“Ameshajenga zahanati kadhaa kwenye maeneo ya Salasala, Mbezi Juu,
Kunduchi, Wazo na Mbopo na kusimamia ukarabati wa nyingine nyingi
jimboni. Pia amefanikisha kupatikana kwa maji ya bomba katika maeneo ya
IPTL (Wazo), Kawe Ukwamani, Mbweni, Makongo na kuna miradi inayoendelea
maeneo ya Mabwepande, Mbuyuni na kwingineko,” alisema Mtiko.
“Pia mbunge amefanikisha kuunganishwa kwa umeme kwenye maeneo ya
Mivumoni, Bunju, Salasala, Wazo Mji Mpya, Nakasangwe, Manyema na maeneo
mengine,” aliongezea Simbeye.
4. TANGANYIKA PACKERS
Makatibu hao wa Mhe. Mdee
waliliambia Uwazi kwamba mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha
waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda cha Tanganyika Packers waliosimamishwa
kazi kuanzia April 30, 1992 kwa likizo isiyo na malipo baada ya kiwanda
kufilisika, wanalipwa mafao yao.
Hata hivyo anakumbana na kikwazo kikubwa kutoka kwa serikali ambayo
inabomoa nyumba za wanyonge na kuwaacha vigogo kadhaa wa serikali
waliojenga ufukweni na kwenye mikondo ya maji wakipeta.” Watumishi wengi
wa serikali, wanamkwamisha, makusudi ili ionekane chama cha upinzani
hakiwezi kazi,” alisema Simbeye.
No comments:
Post a Comment