Wednesday, May 14, 2014

Usiombee kuugua dengue, kipimo Sh50,000

Waombolezaji wakibeba jeneza lenye mwili wa Daktari Gilbert Buberwa wa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuagwa. Daktari huyo, aliyefariki kwa kuugua homa ya dengue, anatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam. Picha na Rafael Lubava 


Dar/Dodoma. Wakati taharuki iliyosababishwa na mlipuko wa homa ya dengue ikiendelea kutikisa kila kona ya jiji, imebainika kwamba gharama za vipimo katika hospitali mbalimbali zinafikia Sh50,000, ikiwa ni tofauti kubwa na Sh1,000 kwa kipimo cha malaria.
Ugonjwa huo unazidi kusambaa jijini Dar es salaam na baadhi ya mikoa, kiasi cha mamlaka kuagiza mabasi yote yaendayo mikoani yafanyiwe usafi wa kunyunyizia dawa za kuua wadudu kudhibiti usienee zaidi mikoani. Pia wananchi wameshauriwa kuvaa nguo ndefu ili kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa huo mchana tofauti na mbu wa malaria.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilipita katika baadhi ya hospitali kubwa binafsi na za Serikali jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa gharama ya kupima homa hiyo ni kubwa zaidi katika hospitali na vituo binafsi vya afya, lakini wagonjwa wanaokwenda katika hospitali za Serikali hulazimika kulipa kati ya Sh25,000 na Sh30,000. Pamoja na homa hiyo kufananishwa na malaria kwa dalili na kuenezwa na mbu, gharama za vipimo vyake ni tofauti kwani mgonjwa wa malaria hutozwa kati ya Sh1,000 na 2,000.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni kwamba baada ya mgonjwa kupata majibu na kubainika anaumwa homa ya dengue, gharama za tiba huwa ndogo kati ya Sh200 na 500 za kununulia dozi ya dawa za kutuliza maumivu aina ya panadol.
Wanaopima waongezeka
Mchunguzi wa magonjwa katika maabara ya kimataifa ya Lancet, Kanda ya Tanzania, Mohamed Abdulai alisema idadi kubwa ya watu wanakwenda katika maabara hiyo kupima homa ya dengue tangu ugojwa huo uenee kwa kasi kati ya Machi na Aprili mwaka huu.
Alisema kwa siku wagonjwa zaidi ya 40 hupima dengue na katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja, wagonjwa 53 waligundulika kuwa na homa hiyo.
Abdulai alisema gharama za kipimo cha dengue katika kituo hicho ni Sh50,000.
Katika Hospitali ya Aga Khan, Mkurugenzi wa Tiba, Dk Jaffer Dharsee alisema kipimo cha homa ya dengue ni kati ya Sh35,000 hadi Sh40,000 kutokana na mchakato wa upimaji wake.
“Ni lazima tunapompima mtu dengue pia tumpime na maradhi mengine kwanza kama homa ya matumbo, malaria na maradhi mengine ambayo tunahisi anayo na ndiyo gharama inakuwa kubwa,” alisema Dk Dharsee.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dk Kaushik Ramaiya alisema katika hospitali hiyo kipimo cha homa ya dengue ni Sh30,000. “Tunatumia vipimo vitatu, kile kitakachoangalia iwapo chembe hai nyeupe za damu zimepungua, malaria na kiwango cha sumu kinachotokana na virusi vya dengue,” alisema.
Dk Ramaiya alisema tangu vyombo vya habari vianze kuripoti ugonjwa huu, watu wamejawa hofu na hufika hospitali kwa wingi wakitaka kupima maradhi hayo ili kujua kama wapo salama.

 Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela alisema baada ya vipimo vilivyotoka maabara kuu ya Serikali kumalizika, gharama ya vipimo hivyo zimefikia Sh25,000.
“Hospitali imetumia fedha zake kununua vipimo 10 ambavyo viligharimu Sh250,000, hata hivyo kwa sasa vimekwisha hivyo mgonjwa hana budi kuchangia,” alisema. Hata hivyo, alisema inapotokea mgonjwa mwenye hali mbaya na hana uwezo, humpima bure.
Daktari kiongozi wa Hospitali ya Mwananyamla, Mrisho Lupinda alisema awali wagonjwa wa dengue walipimwa bure na taasisi ya Afya ya Ifakara, lakini uongozi wa hospitali yake unatarajia kununua vipimo kwa Sh480,000 na baada ya kupatikana, uongozi utapanga gharama za upimaji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Amani Malima alisema wana uhaba wa vipimo ingawa kwa sasa wanatumia vichache vilivyopo kusaidia wagonjwa wa dharura.
Katibu CCM augua
Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Mufindi, Daud Yassin ameugua ugonjwa wa dengue akiwa jijini Dar es Salaam kwa shughuli binafsi.Yassin alisema aligundulika kuwa na ugonjwa huo alipokwenda Hospitali ya Dk Mvungi iliyopo Kinondoni jana ambako alilipia Sh60,000 kwa ajili ya kipimo.
“Wiki iliyopita nilikuwa nasumbuliwa na malaria, nikatumia dozi nikamaliza, lakini sikuwa na nafuu. Homa iliongezeka na kichwa kikazidi kuuma, usiku wa kumkia leo (jana) hali ilikuwa mbaya sana,” alisema. Yassin, ambaye ni mratibu wa mashindano ya Kombe la Muungano Mufindi, alisema kutokana na kuzidiwa alimpigia simu rafiki yake mmoja wa Iringa ambaye ni daktari na baada ya kumwelezea dalili hizo, alimshauri aende hospitali kwa sababu alikuwa na dalili zote za dengue.
“Nilipokwenda Hospitali ya Dk Mvungi, nilipumzishwa pale, nikafanyiwa ‘full blood picture’ na kugundulika kuwa na dengue, ni ugonjwa unaotesa sana,” alisema Yassin.
Serikali yaongeza vipimo
Akitoa taarifa bungeni jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe alisema hadi sasa Serikali imetumia Sh132 milioni na kutenga Sh500 milioni katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Dk Kebwe alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha vitendanishi vyote vinakuwepo na tayari imeagiza vipimo 750 vya nyongeza, kwa kuwa vipimo vilivyo sasa ambavyo ni 350 vinaweza kutumika kwa miezi miwili.

Dk Kebwe alisema Serikali imeanza utaratibu wa kupuliza dawa ya kuua wadudu wakiwamo mbu kwenye mabasi na maeneo yote yenye watu wanaoingia na kutoka Dar es Salaam, ili kuepuka ugonjwa wa dengue kusambaa nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutoa kauli ya mawaziri bungeni kuhusu ugonjwa huo, Dk Kebwe alisema hatua hiyo inafanywa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na wizara yake.
“Mkoa wa Dar es Salaam, umeanza zoezi la kupulizia viatilifu vya kuua mbu katika mabasi yanayoingia na kutoka Dar es Salaam,” alisema Dk Kebwe, kauli ambayo iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki.
Awali, Dk Kebwe alisema wananchi wanatakiwa kuvaa nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye dawa na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba ili kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema mbu huyo anayeishi katika mazingira ya binadamu huuma mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususan majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Temeke wamuaga Dk Buberwa
Jana wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke waliuaga mwili wa Dk Gilbert Buberwa aliyefariki dunia Jumapili kutokana na homa ya dengue.
Sadiki, aliyeongoza wafanyakazi hao, alisema: “Tumepoteza nguvu kazi muhimu katika sekta ya afya, tena kwenye Kitengo cha Magonjwa ya Akili. Alikuwa kijana mdogo na alitegemewa sana.”
Mwili wa Dk Buberwa ulihifadhiwa hospitalini hapo tangu alipofariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amepelekwa kwa dharura baada ya hali yake kuwa mbaya.
Baada ya wafanyakazi kuuaga mwili huo kwa majonzi na vilio, ulipelekwa nyumbani kwa marehemu, Tabata Kinyerezi kusubiri taratibu nyingine za mazishi leo jioni.

Credits to Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment