HAYAWI…hayawi sasa yamekuwa! Habari ya mjini ni maandalizi kabambe ya
harusi ya staa wa Bongo Fleva na Mbunge wa Viti Maalum (CCM)
anayewakilisha Vijana Mkoa wa Geita, Vicky Pascal Kamata ikidaiwa kuwa
shughuli hiyo itatafuna kiasi cha Sh. milioni 96, Ijumaa lina mkanda
kamili.
Vicky Kamata akiwa na mchumba wake
BWANA HARUSI HUYU HAPA
Habari kutoka kwa chanzo cha ndani zilisema kuwa Vicky anatarajia
kufunga pingu za maisha Mei 24, mwaka huu na mchumba wake wa muda mrefu
ambaye Ijumaa limemnasa aliyejulikana kwa jina la Charles Pai.
Ilidaiwa kwamba mwanaume huyo ni kigogo ndani ya kampuni moja ya huduma za simu hapa nchini.
HARUSI YA REKODI
Kwa mujibu wa mtonyaji wetu
huyo ambaye naye ni miongoni mwa wanakamati, harusi hiyo inatarajiwa
kuweka rekodi ya aina yake Bongo.
“Sijawahi kuona harusi ya kifahari
kama ya Vicky, itafanyika tarehe 24 mwezi huu, ina siku chache tu,
huwezi kuamini mambo yote yamekamilika,” alisema mpashaji wetu.
HOTELI YA NYOTA TANO
Imesemekana kwamba baada ya
ndoa hiyo kufungwa kanisani, shughuli itahamia katika hoteli yenye
hadhi ya nyota tano ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro iliyopo Posta, Dar
ambapo waalikwa watagonga mnuso wa maana na vinywaji vya kumwaga.
Mkali wa Bongo Fleva na mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM, Vicky Kamata akiwa katika pozi.
Habari zilieleza kuwa sherehe hiyo itahudhuriwa na mawaziri, wabunge
wenzake, vigogo mbalimbali serikalini na baadhi ya wasanii wenzake.
Ilidaiwa kuwa bajeti ya shughuli hiyo imefikia kiasi hicho kwani Vicky anataka iwe ya aina yake.
BAJETI MIL. 96
Kwa mujibu wa mwanakamati huyo,
kwa bajeti hiyo ya Sh. milioni 96, Vicky atakuwa amevunja rekodi ya ndoa
za mastaa zilizowahi kufungwa Bongo.
“Nakwambia harusi ya Vicky haina mfano, itafunika harusi za vigogo na
mastaa wengi, itakuwa ya aina yake. Bajeti yake siyo ya kitoto.
“Watu wengi wamemchangia, achilia mbali na kuweka hela yake yeye binafsi na mchumba wake, kitu kama Sh. milioni 40.
KUVUNJA UKIMYA NA UVUMI
“Hakika mheshimiwa
amejipanga kuvunja ukimya na uvumi mwingi juu ya maisha yake ya kisiasa
na jamii inayomzunguka,” alisema mtoa habari wetu na kuongeza:
VIKAO NI DAR, DODOMA
“Huwezi kuamini, vikao
vingi vya harusi sisi wanakamati tunafanyia Dar. Lakini mara nyingine
tunafanyia Dodoma kwa sababu waheshimiwa wengi wanakamati wako huko.
“Hata kwenye vikao watu wanakunywa na kula je, siku yenyewe
itakuwaje? Unaambiwa msafara wa magari ya kifahari tupu na utakuwa kama
wa rais ukiongozwa na farasi.
VICKY ANASEMAJE?
Baada ya kupata habari hizo,
gazeti hili lilimsaka Vicky kwa udi na uvumba ili kujua mchakato mzima
wa harusi umekaaje lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa
huenda ni kwa sababu ya kubanwa na vikao vya Bunge la Bajeti
vinavyoendelea mjini Dodoma huku bwana harusi akishindwa kutoa
ushirikiano.
Credits to Global Publishers
No comments:
Post a Comment