Tuesday, April 28, 2015

Mgodi wa Tanzanite One wamwaga ajira 1,280

 Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akipata maelezo kwa wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma Shabhai na Hussein Gonga


Arusha, Kampuni ya Tanzanite One ambayo sasa inamilikiwa na wazawa, imeongeza ajira kwa vijana kutoka 700 hadi 1,280 ili kukabiliana na tatizo hilo nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya madini ya vito yanayoendelea jijini hapa, wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associate Ltd iliyonunua asilimia 50 ya hisa ndani ya Tanzanite one, Hussein Gonga na Faisal Juma walisema wameanzisha pia mafunzo ya kukata kna usanifu wa madini.
Gonga alisema Sky Associate na Shirika linaloshughulikia Madini Tanzania (Stamico) ambao ndiyo wamiliki wa Tanzanite One, wameongeza maeneo ya uchimbaji madini ili kuhakikisha wanaongeza ajira kwa vijana wengi wanaotafuta ajira za uchimbaji katika migodi ya madini.
Alisema katika mafunzo ya ukataji na usanifu wa madini, vijana hufundishwa jinsi ya kuyaongezea thamani na wanaohitimu hupatiwa mashine.
Awali, Mkurugenzi mwenza wa Tanzanite One, Faisal Juma alisema mipango ya kuongeza ajira na kutoa mafunzo ya usanifu wa madini itasaidia kuboresha sekta ya madini nchini.
Juma alisema Tanzanite One kama kampuni kubwa nchini ya uchimbaji wa madini ya vito, itahakikisha inashirikiana na Serikali na wadau wengine kufanya mapinduzi katika sekta ya madini ili Watanzania wengi waweze kunufaika.
Kamishna wa Madini Tanzania, Paul Masanja akizungumza katika maonyesho hayo, aliwataka wamiliki wa migodi na wachimbaji kushirikiana kuboresha sekta ya madini kwa kuhakikisha hawauzi wa kuyatorosha nje ya nchi madini ghafi.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa madini kuhakikisha wanapata masoko ya madini yao na alipongeza jitihada za kuwapa mafunzo vijana juu ya ukataji wa madini.

No comments:

Post a Comment