Tuesday, April 28, 2015

HELKOPTA YA NDESAMBURO YAZUA KIZAAZAA MOSHI.

Helikopta iliyotumiwa na Kada wa CCM Buni Ramolle, ikitua katika Uwanja wa Pasua mjini Moshi, Aprili 18 mwaka huu.


Moshi. Helkopta ya Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, imeleta kizaazaa, baada ya Kada wa CCM, Buni Ramolle ambaye aliikodi kwa ajili ya mikutano yake ya kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, kudai kuwa ni mbovu na ilitaka kumuua.
Kada huyo akaenda mbali na kueleza kuwa kutokana na hitilafu hiyo, ameitaka kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd, iliyomkodishia helkopta hiyo, kumrejeshea fedha zake zote alizoilipa kwa ajili ya kuitumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Ndesamburo ambaye ni mmiliki wa helkopta hiyo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation, alikanusha madai hayo akisema kuwa hayana msingi.
“Anasema helikopta ni mbovu wakati ilimpeleka na kumrudisha? Alihoji Ndesamburo na kusisitiza kuwa “tutawaomba wakaguzi wa ndege waifanyie ukaguzi na ripoti hiyo ndio tutaitumia kumshitaki nayo.”
Kuhusu madai ya Ramolle kuwa amerejeshewa fedha zake alizolipa, Ndesamburo alihoji “Tunamrudishia fedha gani wakati hakulipa? Kuwa na Proforma Invoice ndio kulipia?”
Awali taarifa zilieleza kuwa Ramolle alitoa tuhuma hizo, baada ya viongozi wa CCM, kumbana wakimtaka aeleze kwa nini ameamua kutumia helkopta ya Ndesamburo ambaye ni mpinzani wake kisiasa.
Jana Ramolle alitumia mkutano wake na waandishi wa habari kukanusha kuwa helkopta aliyoitumia Aprili 18 mwaka huu ni ya Ndesamburo. Alidai katika mkutano huo kuwa helkopta hiyo aliikodisha kama mteja kutoka kampuni ya General Aviation Services na hajui kama ni ya Ndesamburo.
Lakini tayari Ndesamburo mwenyewe ameshajitokeza hadharani na kudai kuwa helkopta hiyo ni mali yake na kwamba ameingia mkataba wa kuikodisha kwa kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd.
Huu ni mchezo mchafu
Kwa mujibu wa Ramolle, kinachofanyika sasa ni mbinu za kumchafua ndani ya chama ili asiaminike na aenguliwe kama alivyoenguliwa mwaka 2010.
Ramolle alisema kutokana na Ndesamburo kudai helkopta hiyo ni yake, tayari kampuni ya General Aviation Services wamemrudishia fedha zake alizokuwa amekodishia na ameishtaki kampuni hiyo kwa Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro kutokana na kutompa risiti ya malipo aliyoyafanya. Buni alisema atapambana na waandishi wanaotaka kumchafua kwa kuwa ana mahasimu ndani na nje ya chama na kutaka asiharibiwe kazi yake na siasa.
“Nimechoka kunyanyaswa nimepata madhara makubwa kwa sababu ya siasa nina maadui ndani na nje ya chama nitapambana na yeyote atakayenizushia maneno na mtu asinifuatefuate” alisema.

Chopa siyo maendeleo
Akizungumzia kutumia chopa kwenye mikutano, Ramolle alisema nia ni kuleta ushawishi kwa wananchi ili wahudhurie mikutano na kwamba hekopta si maendeleo.
“Nimechukua (chopa) makusudi ili kuwaonyesha wananchi Chopa si maendeleo, watu wa Moshi wanafikiri chopa ni maendeleo chopa kazi yake ni kuvuta watu na nimeshaiagiza itakuja hii niliyokodisha awali ni mbovu kwanza ingeweza kuniua ile,” alisema.
“Nilitaka watu wajue chopa siyo maendeleo, Ndesamburo alikuwa akiitumia kuwavuta tu. Maendeleo ni uwajibikaji”
Ramolle alisema kwa maslahi ya watu wa Moshi yupo tayari kuchukua uamuzi mgumu iwapo chama kitaengua jina lake . “Nikishinda halafu jina langu likakatwa patachimbika.”

No comments:

Post a Comment