DAH! Inasikitisha sana jamani. Faustina Selali, 38,
mkazi wa Mgeta, Mvomero mkoani hapa, yupo kwenye mateso makali
akijiuguza kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa mumewe wa ndoa
aliyemtaja kwa jina la Lugasiani John Miasiku, kisa kikiwa ni mumewe
huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Faustina Selali, akiwa katika maumivu makali baada ya kushambuliwa na mumewe.
Mwanamke huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote mbele ya kamera ya
Uwazi.
KISA CHENYEWE
Akizungumza kwa tabu, Faustina
alisema tukio hilo lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia
machungu moyoni mwake, lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne
usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye ndoa
kwa muda wa miaka 20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi
kirefu nilihisi ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati
naendelea kumchunguza, mume wangu akaniambia anataka kuoa mke wa pili,”
alisema Faustina kwa uchungu na kuongeza:
“Nikamhoji mume wangu, dini yetu hairuhusu jambo hilo na zaidi ya
yote anachotafuta kwa huyo mke wa pili ni kitu gani wakati tayari mimi
nimeshamzalia watoto watano na bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu
la maana, akaendelea kushikilia msimamo wake. Mwisho nikaona
nisimlazimishe sana, nikamwambia kama hivyo ndivyo basi tugawane mali
ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani sitakuwa tayari kuishi maisha
ya uke wenza. Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”
Akionyesha sehemu ya jeraha.
HARUFU YA KIFO
“Ugomvi huo ulitokea Jumanne,
kesho yake yaani Jumatano (siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba
nilimtengea ugali kama kawaida. Alikula vizuri tu... tukapanda kitandani
kulala, kama unavyojua tena wanandoa muda wao wa kuzungumza kwa utulivu
ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia kama bado ana msimamo wake uleule, anipe sehemu yangu
niondoke zangu. Hapo nikawa nimechokoza moto. Ilikuwa ghafla tu, aliamka
kitandani na kuchukua nyundo kisha akaileta kichwani na kunipiga nayo,
baadaye akanipiga mdomoni na kuning’oa meno mawili ya mbele kwa kutumia
ile nyundo.
“Hakuishia hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono yote,
palepale damu zikaruka kama kachinja ng’ombe. Nilihisi maumivu makali
sana, sikuwahi kupata maumivu makali kama yale. Kusema ukweli
nilichanganyikiwa kabisa na kile kipigo.”
ATUMIA UJANJA KUJIOKOA
“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma,
alikuwa akisema dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo
mwanamke wake bila usumbufu. Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili;
nikajiangusha chini na kujifanya nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.
“Alipoona hivyo kweli akaniacha. Akavaa nguo zake na kukimbia.
Mwanangu mdogo Nesto akanisaidia kunikongoja hadi kwa jirani yetu Mzee
Chota ambaye naye aliita majirani haraka, ilikuwa ni saa sita usiku,
wakanikimbiza hadi Zahanati ya Mlali lakini nikapewa rufaa ya kuletwa
hapa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia ukatili huo,
ndugu wanaofika hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe bado
hajakamatwa na amekuwa akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
Uwazi lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la kuhojiana na
mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi wetu,
Miasiku alitimua mbio akidhani alifuatwa na askari.
No comments:
Post a Comment