Monday, June 2, 2014

UKWELI WA KIFO CHA MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU

HATIMAYE familia ya denti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, marehemu Sekabenga Pius Mwakimenya (21) kilichotokea hivi karibuni na kugubikwa na utata, imeanika ukweli kuhusiana na tukio hilo.

 Marehemu Sekabenga Pius Mwakimenya enzi za uhai wake.

 Akizungumza na Uwazi, mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, baba mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mwigune alisema, taarifa waliyopewa na daktari aliyemfanyia uchunguzi inamaliza utata na minong’ono yote inayoendelea chuoni.
Alisema, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kifo cha Sekabenga kimetokana na mzunguko wa damu katika mishipa kutokuwa sawa, jambo lililosababisha ajisikie vibaya na hatimaye kufariki dunia.

 Mwili wa marehemu Sekabenga Pius Mwakimenya ukiwa kwenye jeneza.

 “Daktari amesema kwamba mishipa ya damu haikuwa ikifanya kazi vizuri hali iliyomsababishia ajisikie kuchoka kwa sababu damu haikuwa ikifika sehemu zote za mwili wa marehemu,” alisema Mwigune.
Uwazi lilifunga safari hadi chuoni na kuzungumza na baadhi ya wanafunzi ambao walionyesha wasiwasi kuwa huenda marehemu aliamua kujiua kwa sumu kwa maelezo kuwa, siku chache kabla ya kifo chake alionekana mwenye mawazo mengi.

 Sekabenga akiagwa.

“Hakuwa mwenye furaha, ni kama alikuwa na jambo zito linalomsumbua ndiyo maana unasikia wanafunzi wengi hapa chuoni wanahusisha kifo chake na sumu,” alisema denti mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa familia inayonukuu ripoti ya daktari inaziba minong’ono yote kwa kuwa haionyeshi mahali popote kuwa marehemu alijiua kwa sumu.

 Mwili wa Sekabenga ukiingizwa kwenye gari.


Marehemu Sekabenga alikuwa mwaka wa pili chuoni hapo  akichukua Shahada ya Kwanza ya Biashara na Uhasibu, mwili wake  umesafirishwa Jumamosi Mei 31, mwaka huu kwenda mkoani Mbeya kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika jana Jumatatu.
Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.

No comments:

Post a Comment