Mtoto wa marehemu George Otieno ‘Tyson’, Sonia George Otieno akiuaga mwili wa baba yake kwa huzuni kubwa.
Tukio hilo lililowaumiza wengi lilitokea Jumanne, nyumbani kwa marehemu Tyson, Mbezi – Makonde, jijini Dar es Salaam wakati ndugu pekee wakiaga mwili wa mpendwa huyo.
Sonia alipolifikia jeneza na kumtaza baba yake, alitulia kwa muda kidogo kisha kwa utulivu akasema: “Niamshieni baba yangu, kumbe amelala tu.”
Kauli ya Sonia na umri wake mdogo, akiwa ndiyo kwanza anajiandaa kufanya mitihani yake ya mwisho ya kumaliza elimu ya msingi, vilisababisha huzuni huku baadhi ya watu wakiangua vilio vya nguvu.
Sonia akilia kwa huzuni, pembeni kulia ni mama yake Monalisa na aliyemkumbatia ni bibi yake Natasha.
JUMATANO – LEADERS CLUB
Baadaya ndugu kumuaga Jumanne, juzi Jumatano marehemu Tyson aliagwa rasmi na mashabiki na wadau wote katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar ambapo mamia ya watu walijitokeza.
Mgeni rasmi katika shughuli hiyo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick ambaye aliingia viwanjani hapo akiwa ameongozana na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, Simon Mwakifwamba.
Sadick alisema: “Poleni sana ndugu wasanii. Sisi kama serikali tumeumizwa na kifo cha George Tyson. Tunajivunia kuwa naye katika kipindi chote hapa Tanzania. Ingawa alikuwa Mkenya lakini alisaidia kukuza sanaa hapa nchini kwa nafasi yake.”
WASANII WAMLILIA
Umoja na ushirikiano kwa wasanii wa filamu nchini umeendelea kuonekana ambapo walifurika viwanjani hapo kumuaga mwenzao ambaye atazikwa nyumbani kwao, Kisumu nchini Kenya.
Sonia na Monalisa wakiwa na nyuso za huzuni wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Tyson.
Pamoja na wingi wao, wasanii waliofanya naye kazi tangu awali kabisa katika Kipindi cha Mambo Hayo kilichokuwa kikirushwa na Runinga ya ITV, akiwemo Single Mtambalike ‘Richie’ na Jacob Steven ‘JB’ walipiga picha ya pamoja ya ukumbusho.
Mastaa walishindwa kujizuia wakati wakipita mbele ya jeneza la marehemu, ambapo wengi hata wanaume walitokwa na machozi.
WENGINE WAPOMBEKA
Katika hali ya kushangaza, baadhi ya wasanii walionekana wakiwa kwenye baa iliyopo viwanjani hapo wakiendelea kupiga stori na wengine wakinywa pombe wakati shughuli hiyo muhimu inayohitaji utulivu na nidhamu ikiendelea.
Kamera ya Ijumaa, iliwanasa wasanii wengi wakiwemo Soud Ally, Riyama Ally, Upendo Mushi ‘Pendo’, Miriam Jolwa ‘Jini Kabula’ Hisani Muya ‘Tino’, Idrissa Makupa ‘Kupa’ wakiendelea na stori kama vile hapakuwa na msiba huku miongoni mwao wakikata kilaji.
Mzee Chillo akitoa heshima zake za mwisho kwa mwili wa Tyson.
ROHO WA MAUTI AKEMEWA
Mchungaji wa Kanisa la Huduma ya Inuka Uangaze, Buldozer Mwamposa ambaye aliongoza ibada ya kumuombea marehemu, aliwaombea wasanii wote Tanzania, roho ya mauti inayowaandama iondoke.
Baada ya mahubiri, Mchungaji Mwamposa aliwataka watu wote wasimame ili awaombee wasanii dhidi ya roho ya mauti.
Baada ya maombi hayo alitangaza ushindi akisema: “Damu ya Yesu imewafunika, hakuna kifo chochote cha msanii kitakachotokea. Mungu yupo.”
WASANII WAPONGEZWA
Ushirikiano wa TAFF na Bongo Movie Unity ulipongezwa na wadau wengi waliohudhuria. Walishirikiana kwa umoja bila kubaguana.
Mbali na wasanii wa filamu, mastaa wa sanaa mbalimbali kama Bongo Dansi, Bongo Fleva na wanamitindo walikuwepo kumuaga Tyson.
SAFARI YA UWANJA WA NDEGE
Hatimaye baada ya shughuli hiyo kukamilika, msafara wa kupeleka maiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ulianza tayari kwa safari ya kuelekea Kenya, iliyotarajiwa kufanyika jana Alhamisi.
TYSON KUKAA SIKU 10 ZAIDI
Habari kutoka ndani ya familia ya marehemu, zilieleza kuwa marehemu alitarajiwa kusafirishwa jana hadi Nairobi Kenya kwa ndege, kisha kuhamia kwenye mabasi yatakayowafikisha Kisumu kwa mazishi yatakayofanyika Jumamosi ijayo – achana na kesho (Juni 14, mwaka huu).
Habari kutoka ndani ya familia ya marehemu, zilieleza kuwa marehemu alitarajiwa kusafirishwa jana hadi Nairobi Kenya kwa ndege, kisha kuhamia kwenye mabasi yatakayowafikisha Kisumu kwa mazishi yatakayofanyika Jumamosi ijayo – achana na kesho (Juni 14, mwaka huu).
DK. Cheni naye alimuaga Tyson.
POLENI, PUMZIKA TYSON
Dawati la Ijumaa tunatambua maumivu waliyonayo wafiwa wote na familia kwa jumla. Tunajua namna Monalisa, aliyekuwa mke wa ndoa wa marehemu, Sonia, binti wa marehemu, Natasha, mkwe wa marehemu, wasanii na wadau wengine mnavyoumia. Mungu awafanyie wepesi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Tyson, mahali pema peponi – Amina.
No comments:
Post a Comment