Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama
cha Wananchi (CUF) limemchagua Mbunge wake wa Viti Maalumu, Magdalena
Sakaya kuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho upande wa Tanzania Bara
kushika nafasi iliyoachwa wazi na Julius Mtatiro.
Pia limemchagua Waziri wa Biashara wa Zanzibar,
Nassor Ahmed Mazrui kuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho upande wa
Zanzibar nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Hamad Masoud.
Mtatiro hakuingia katika kinyang’anyiro cha
kuwania nafasi hiyo kutokana na kutokuchukua fomu kugombea ujumbe wa
Baraza Kuu ambayo ndiyo sifa inayotakiwa kuingia katika sekretarieti ya
chama hicho.
Akizungumza jana kwa simu, Naibu Mkurugenzi wa
Habari wa CUF, Abdul Kambaya alisema awali, Sakaya alikuwa akishindana
na Mbunge wa Viti maalumu,
Kuluthum Mchuchuli kabla ya mpinzani wake kujitoa
akisema ana imani kubwa na Sakaya ambaye aliibuka na ushindi wa kura 51
kati ya 52 zilizopigwa. Moja iliharibika.
Upande wa Zanzibar, Mazrui alimshinda Mbunge wa Viti Maalumu, Zahra Ahmed Ali baada ya kupata kura 51 na Zahra akiambulia moja.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mtatiro alisema ana
imani kubwa na Sakaya kutokana na uwezo mkubwa wa siasa alionao akisema
ameking’arisha chama hicho ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu
alichoshika wadhifa huo amekuwa mkomavu katika siasa baada ya kuchota
hekima za viongozi wazoefu wa kitaifa.
“Kupumzika majukumu haya makubwa ni faraja kwangu
na kutanipa muda wa kutosha wa kukamilisha shahada ya tatu ya sheria,”
alisema Mtatiro.
Alisema ataendelea kutumia uzoefu alioupata kukieneza chama hicho ili kuhakikisha kinaweka mizizi Tanzania Bara.
“CUF ni kila kitu kwangu bado najiona nina deni
kubwa katika chama changu, leo, kesho na keshokutwa nitakuwa nafikiria
nini nikifanyie chama changu na siyo chama kinifanyie nini mimi,”
alisema.
No comments:
Post a Comment