Lilongwe. Wakati Rais wa Malawi, Joyce Banda
akizidi kuelemewa kwenye uchaguzi uliofanyika Jumanne wiki hii, Naibu
Waziri wa Serikali za Mitaa, Godfrey Kamanya amejiua baada ya kubaini
ameshindwa kutetea kiti chake cha ubunge.
Kamanya alijipiga risasi nyumbani kwake mjini Lilongwe saa 9:30 asubuhi baada ya kupewa taarifa hizo kwa ujumbe mfupi wa simu.
Kabla ya kujiua, aliacha ujumbe kwamba amechukua hatua hiyo baada ya kutokea migongano ya kisiasa.
Kamanya aligombea ubunge katika Jimbo la Nzonzi
Kusini kupitia People’s Party (PP) na mwili wake ulikutwa chumbani kwake
na ulipelekewa kuhifadhiwa kwenye Hospitali Kuu ya Kamuzu.
Taarifa nyingine zinaeleza kwamba waziri huyo alijiua kutokana na vitisho kutoka kwa mtu asiyefahamika.
Katika matokeo yasiyo rasmi kutoka kituo cha
kuhesabia kura cha Lilongwe yaliyotolewa Jumatano asubuhi, mgombea huyo
alikuwa ameshika nafasi ya tano kati ya wagombea saba waliowania ubunge
kwenye jimbo hilo.
Katika matokeo hayo ya awali, Kamanya alipata kura
1,738 huku mgombea wa Malawi Congress Party (MCP), Higton Jiya
akiongoza kwa kura 4,625.
Wakati tukio hilo likitokea, mke wa Kamanya
alimpigia simu waziri wa zamani wa usafirishaji, Ulemu Chilapondwa
ambaye alikuwa rafiki ya mumewe na kumweleza kuwa amesikia mlio chumbani
wakati mlango umefungwa.
Kutokana na taarifa hiyo, Chilapondwa alipofika
nyumbani kwa marehemu akiwa na watu wengine wawili walivunja mlango na
kukuta mwanasiasa huyo ameshaaga dunia baada ya kujipiga risasi kifuani.
Tukio hilo limekuja wakati mgombea urais kupitia
chama chake, Rais Joyce Banda akiwa katika nafasi ya pili akiwa na
asilimia 22 ya kura akigongana na Lazarous Chakwera wa Malawi Congress
Party (MCP). Anayeongoza ni mgombea urais kupitia Democratic Progressive
(DPP), Peter Mutharika kwa zaidi ya asimilia 30.
No comments:
Post a Comment