Dar es Salaam. Aliyekuwa Meneja wa Biashara ya
Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius
Gashaza alijinyonga kwa tai. Taarifa iliyotolewa jana Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kipolisi Temeke, Engelbert Kiondo imesema.
Baada ya taarifa hiyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeunda jopo kuchunguza sababu za kifo hicho.
Meneja huyo alikutwa amekufa katika Gesti ya
Mwanga Lodge iliyopo Yombo na kifo chake kinaelezwa kutokea katika
mazingira ya kutatanisha. Alijinyonga muda mfupi baada ya kuwasili Dar
es Salaam akitokea Dodoma ambako alihudhuria mkutano kwenye Kamati ya
Bunge ya Bajeti.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema jana kuwa jopo hilo litaongozwa na Mkuu wa
Upelelezi kanda hiyo, Jaffary Mohamed atakayeshirikiana na wataalamu wa
Maabara Kuu ya Polisi, daktari bingwa wa Polisi na serikalini.
Kova alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi ili
kuondoa utata ulioanza kujitokeza kuhusiana na kifo chake baada ya
taarifa kuzagaa kwamba kilitokana na kutoelewana na viongozi wenzake
katika masuala ya kikazi.
Alisema uchunguzi huo ukikamilika, jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Kinachofanyika ni kupata maelezo ya kina kuhusu
mwenendo wa shughuli za marehemu na hali iliyomsibu kabla ya kifo chake
kwani hakuacha ujumbe wowote wa maandishi au wa mdomo,” alisema Kova.
Alisema maelezo mbalimbali ya mashahidi yanaendelea kuchukuliwa ili kufahamu kama kuna kosa la kijinai, kiutawala au yote.
Kamanda wa Mkoa wa Temeke
Kamanda Kiondo alisema: “Uchunguzi ninaoufahamu
hadi sasa ni kuwa Gashaza alijinyonga kwa kutumia tai yake, akiwa bafuni
katika hoteli ya Mwanga. Alitumia stuli kupanda juu, stuli ilianguka na
tai ilikatika ndipo mauti yakamfika,” alisema.
Alisema mwili wake ulionekana kuvimba kutokana na kujinyonga na inaonekana mshipa wa hewa ulizibwa na kusababisha kifo chake.
Kamanda Kiondo alisema kutokana na kuthibitika kuwa Gashaza amejinyonga, uchunguzi utakaofanyika ni kujua chanzo cha kujinyonga.
Alitishiwa maisha
Ndugu wa marehemu aliyefahamika kwa jina moja la
Silipwango alisema Gashaza alirudi akiwa na wasiwasi mwingi na kusema
kuwa alikuwa akitishiwa maisha ingawa hakueleza kwa undani na nani na ni
kwa nini.
“Ilibidi tuongozane wote, mimi, Gashaza na mkewe
hadi katika hoteli aliyotaka kulala. Tukiwa pale tulifanya hata na
maombi yaliyoongozwa na mke wake ili kumkabidhi mikononi mwa Mungu,
ndipo tukamuacha,” alisema.
Alisema kutokana na hali waliyokuwa wamemuacha
nayo usiku, hawakulala vyema na asubuhi na mapema alikwenda katika
nyumba hiyo ya wageni ndipo alipogundua kuwa Gashaza amejiua.
Mamia wamuaga
Mamia ya wakazi wa Vituka, ndugu, jamaa na
wafanyakazi wa Ewura jana walifurika nyumbani kwa marehemu kutoa heshima
zao za mwisho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Felix Ngamlagosi
alimtaja marehemu kuwa: “Kiungo muhimu sana kwa Ewura, alikuwa si tu
mchapakazi, bali mwadilifu na mtiifu aliyeunganisha wafanyakazi wenzake,
aliyewatia moyo na kutenda kazi kwa umakini mkubwa.”
Ngamlagosi alisema Gashaza aliibadili taswira ya
Ewura kutokana na uadilifu wake, hasa kwa utendaji wake wa kutukuka
alipokuwa Mkaguzi Mkuu wa Mafuta.
No comments:
Post a Comment