ARUSHA
Mkurugenzi wa Kampuni ya Excite Media inayomiliki mtandao maarufu wa Udaku Pepe jana alifanyiwa unyanyasaji na polisi wa Arusha wakati akiwa kazini.
Ilivyokuwa
Ilikuwa majira ya saa moja na nusu asubuhi wakati mdaku huyo akiwa katika harakati za kutafuta habari za asubuhi kwa ajili ya blogu hii pendwa ndipo alipokutana na tukio la askari wa usalama barabarani kumpiga na kumuumiza dereva wa daladala iliyokuwa ikifanya safari zake toka USA river na Arusha mjini. Baada ya kufanya kitendo hicho askari huyo alikimbilia kujificha katika gari aina ya Noah ili kukwepa wananchi waliokuwa na ghadhabu na walioonekana walikuwa na nia ya kujichukulia sheria mikononi.Mdaku mkuu aliamua kufuatilia kwa karibu ili kufahamu undani wa habari hiyo ndipo wananchi waliokuwa katika eneo hilo walipomtonya kwamba kulikuwa na kutoelewana kati ya dereva wa daladala na gari aina ya Noah iliyokuwa ikiendeshwa na mwanamama ambaye hakujulikana mara moja. Wakati mzozo huo ukiendelea ndipo askari huyo alifika ili kusuluhisha tifu hilo ndipo walipopisha lugha na dereva wa daladala na askari huyo kumpiga na kitu kilichomtoboa kijana huyo na kutokwa damu katika jereha hilo.
Hata hivyo baada ya wananchi kuchachamaa na kutaka kujichukulia sheria mikononi, askari huyo alipiga simu makao makuu ya trafiki Arusha ambapo askari walifika kuja kumsaidia mwenzao. Katika hali hiyo mmoja wa askari alimuona mdaku akipiga picha kwa kutumia simu yake ya mkononi na kumnyang'anya kisha kumkamata kwa nguvu na kumuweka chini ya ulinzi. Baada ya tukio hilo askari hao walimchukua mdaku mkuu mpaka kituo kikuu cha polisi Arusha na mkuu wa msafara huo aliamuru mdaku mkuu aswekwe lupango bila maelezo.
Kwa amri hiyo ya mkuu wa msafara huo, mdaku mkuu aliwekwa lupango kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni ndipo alipoachiwa bila masharti na kurudishiwa vitu vyake vyote ikiwamo simu yake ya mkononi ambayo baadae aliamriwa kufuta picha zote alizopiga.
Akiwa mikononi mwa polisi.
Akiwa mikononi mwa polisi baadhi ya askari walikuwa wakimtisha kwa kumuambia kwamba leo atakiona cha moto maana mmezoa kupiga askari picha wakiwa wamelewa na kuwasababishia matatizo kazini ikiwamo kufukuzwa kazi.Mtandao huu unalaani na kupinga vikali juhudi zozote za baadhi ya askari wa jeshi la polisi kuwanyanyasa waandishi wa habari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
No comments:
Post a Comment