Mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita huko Thailand, Amina Ngaluma.
MWILI wa mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita
nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’ unatarajiwa kuwasili Dar es
Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid Sumuni tayari taratibu muhimu
kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani zimefanyika na wana amini mambo
yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke wangu utaondoka Thailand
Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es Salaam siku
inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili
kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa
marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko
yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika lini, kwa sababu bado mwili
haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana na sehemu alikokuwa
anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule tumeshamaliza taratibu
zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,” alisema Sumuni
kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuwa karibu na familia yao
wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba wanapotaka kutoa habari
kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa familia ili kupata
taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki
dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa
akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African
Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za
Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge
yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya
shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini
na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga
nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo
Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night,
Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni
Mgumba, Maisha Kitendawili, Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu
wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa
Dunia’. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin.
No comments:
Post a Comment