Dar es Salaam. Mume wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili, (jina tunalihifadhi kwa sasa), anatuhumiwa kumbaka shemeji yake mdogo (17).
Taarifa za tukio hilo ziliripotiwa juzi saa 12
jioni katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule), zikimtuhumu
mwanamume huyo kwamba alimbaka binti huyo mara tatu na kumsababishia
maumivu makali.
Binti huyo alifika katika kituo hicho cha polisi
akiwa na ndugu zake wawili ambao walilalamika kwamba kulikuwa na
jitihada kubwa kutoka upande wa mtuhumiwa wa kuzima kesi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili nje ya kituo hicho,
binti huyo alisema shemejiye alimbaka mara ya kwanza, Ijumaa iliyopita
na Jumapili alipombaka mara mbili ndani ya gari.
Alisema mara ya kwanza alikaa kimya baada ya
mtuhumiwa kumtishia kwamba angemdhuru kama angetoa taarifa ya tukio hilo
alilofanyiwa wakiwa sebuleni nyumbani kwako Tabata Kimanga, lakini
aliamua kutoa taarifa kwa ndugu zake baada ya kubakwa mara ya pili.
Polisi katika kituo hicho walithibitisha kupokea
taarifa za tukio hilo lakini walishindwa kwenda kumkamata mtuhumiwa kwa
maelezo kwamba hawakuwa na askari wa kutosha na kuahidi kwamba
angekamatwa jana. Hata hivyo, hadi jana mtuhumiwa huyo alikuwa
hajakamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi
kutwa nzima ya jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na kila simu
yake ilipopigwa (kati ya saa nane mchana na saa mbili usiku), ilipokewa
na msaidizi wake akisema bosi wake ana kazi nyingine.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hakuwa amepokea taarifa yoyote ya aina hiyo.
Mwimbaji anena
Alipoulizwa jana, mwimbaji huyo alisema kwa sasa
hawezi kuzungumzia kwa undani tuhuma zinazomkabili mumewe na kwamba
alikuwa anajisikia vibaya kutokana na tukio hilo kuhusisha watu wake wa
karibu.
“Of course (bila shaka), hili sio tukio zuri. Kwa
sasa sina uwezo wa kuzungumza kwa sababu hili suala lipo Polisi. I am
confused (nimechanganyikiwa), ukizingatia kwamba linasemekana kutokea
wakati sikuwepo nyumbani, naomba tuzungumze baada ya akili kutulia,”
alisema.
Kadhalika, jana saa 6:20 mchana, gazeti hili
lilifanikiwa kuzungumza na mtuhumiwa ambaye baada ya kupewa maelezo
kuhusu tuhuma zinazomkabili alisema: “Samahani sana ujue sikusikii
kabisa,” kisha alikata simu.
Gazeti hili lilimpigia tena simu lakini ilikatwa na baada ya
hapo kila alipopigiwa haikupokewa. Baadaye saa 6:35 mchana, mtu
aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa alipiga simu chumba cha
habari akitaka kuonana na mhariri wa gazeti hili, kwa maelezo kwamba
alipewa namba husika na kaka yake.
“Samahani, mimi (anataja ina) niko hapa nje Ofisi
za Mwananchi, nilifika hapa kutaka kuonana na mhariri maana nasikia
mwandishi wenu alikuwepo polisi tangu jana kwenye tatizo lililompata
kaka yangu, sasa wakati nasubiri kuonana na mhariri kaka amenipigia simu
akisema namba hii imempigia, kwa hiyo naomba tuonane ili tuzungumze
tuone jinsi ya kumsaidia,” alisema.
Baada ya kuonana na mwandishi wa habari wa gazeti
hili, alisema suala hilo lilikuwa likijadiliwa katika ngazi ya familia,
hivyo wasingependa liandikwe kwenye vyombo vya habari.
Vipimo vya hospitali
Juzi, baada ya tukio hilo kuripotiwa, mtoto huyo
alipelekwa katika Hospitali ya Amana ambako alifunguliwa faili la
matibabu na kupewa namba ya usajili 667. Aliingia chumba cha matibabu
namba 21 kumuona daktari kwa ajili ya vipimo zaidi.
Matokeo ya vipimo yalionyesha kuwa binti huyo
alikuwa amefanya ngono kwa nguvu. Katika fomu hiyo ya uchunguzi, daktari
aliandika ‘High vagina swab’.
Baada ya vipimo, familia ilirudi katika Kituo cha
Polisi kupeleka matokeo ya vipimo vya daktari, hivyo kufungua faili la
kesi lililopewa namba RB TBT/RB/319/2014 na namba TBT/IR/1865/2014. Jana
binti huyo alikwenda tena Amana ambako alifanyiwa vipimo vilivyobaki
vya VVU na mimba. Vipimo vya awali vya VVU vilionyesha kuwa hakuwa
ameathirika na hakupata ujauzito.
Mtoto alipo
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana jioni,
zilisema mtoto aliyebakwa alichukuliwa na familia ya Mchungaji Josephat
Gwajima.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta
Mchungaji Gwajima bila mafanikio, lakini lilimpata mkewe, Grace ambaye
hakuwa tayari kuthibitisha kuwapo au kutokuwapo kwa mtoto huyo nyumbani
kwake.
“Naomba nisiwe msemaji katika jambo hilo, yupo
msemaji mwenyewe ambaye naamini mnamfahamu naye ni Mchungaji Gwajima,
kwa hiyo mtafuteni, yeye atasema kama mtoto yupo hapa au hayupo na kama
yupo sababu zake ni zipi,” alisema Grace.
Alipoombwa atoe mawasiliano ya simu ya mchungaji
huyo, Grace alisema: “Kwa kweli kama unaweza, kesho nenda pale Kanisani
Kawe utapewa utaratibu wa kuonana naye.”
No comments:
Post a Comment