Friday, May 30, 2014

KAMBI YA UPINZANI BUNGENI WAMNING'INIZA ZITTO KABWE...

Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi akiwasilisha bungeni maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma, jana.

Dodoma.Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jana ilimlipua mbunge kutoka kambi yao, Zitto Kabwe ikimhusisha na ufisadi wa Sh119 milioni kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Hii ni mara ya kwanza kwa kambi ya upinzani kumhusiaha mbunge ‘mwenzao’ na tuhuma za ufisadi tofauti na kawaida yao ya ‘kuwashughulikia’ ubadhirifu katika Serikali.
Zitto, mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema na ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), anadaiwa kuchota fedha hizo kupitia kampuni ya Leka Dutigite ambayo ina hisa nyingi katika kampuni nyingine ya Gombe Advisors Limited ambayo Zitto ni mkurugenzi wake.
Akiwasilisha maoni ya upinzani bungeni jana kuhusu makadirio na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka 2014/15, waziri kivuli wa wizara hiyo, Joseph Mbilinyi alisema Zitto hakutakiwa kuchota fedha hizo kwa kuwa anabanwa na sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Alisema Zitto, ambaye katika miezi ya karibuni aliingia kwenye mgogoro na uongozi wa chama chake, ni mwenyekiti wa PAC, kamati ambayo jukumu lake ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika wizara na mashirika ya umma, yakiwamo Tanapa na NSSF, hivyo kulikuwa na mgongano wa kimasilahi katika suala hilo.
Tuhuma za Zitto
Katika hotuba yake, Mbilinyi alisema taarifa za kibenki ambazo kambi hiyo imezipata zinaonyesha kuwa Desemba 10, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilihamisha Sh12 milioni kwenda katika akaunti ya kampuni ya Leka Dutigite.
“Siku moja baadaye fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo. Januari 14 na Februari 7, 2013 akaunti ya Leka Dutigite iliingiziwa Sh28.6 milioni,” alisema Mbilinyi.
Sugu alisema fedha hizo ziliingizwa na mtu aitwaye Mchange na kwamba ilipofika Februari 7 zote zilikuwa zimetolewa.
Alisema Februari 28 mwaka jana, akaunti ya Leka Dutigite iliingiziwa Sh32.3 milioni kutoka NSSF na kwamba siku hiyo hiyo fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadaye shirika hilo lilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite.
“Ziliingizwa Sh46.6 milioni ambazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili. Katika kipindi cha miezi mitatu, kati ya Desemba 10, 2012 na Machi 4, 2013 kampuni hiyo (ya Zitto) ililipwa Sh119.9 milioni kwa utaratibu huohuo wa ingiza-toa fasta,” alisema Mbilinyi.
Alisema kati ya fedha hizo Sh12.2 milioni zililipwa na Tanapa na Sh79 milioni zililipwa na NSSF.

 Mbilinyi alizihusisha Sh12.2 milioni za Hifadhi ya Taifa ya Saadan na maandalizi ya filamu fupi ya kuhamamisha shughuli za utalii wa hifadhi kwa kuwatumia wasanii kutoka mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa wana nakala ya mkataba huo.
Alisema ofisi ya kampuni ya Gombe Advisors zipo jengo moja na zilipo ofisi za Kampuni ya Leka Dutigite na kusisitiza kuwa nyaraka walizo nazo zinaonyesha kuwa Zitto na Raphael Ongangi ndiyo wakurugenzi, huku Zitto akitajwa kuwa mchumi katika kampuni hiyo.
“Zitto siyo mchumi kama ambavyo zinaeleza nyakara za usajili wa kampuni hiyo. Ni mbunge na kiongozi na kwa mujibu wa sheria viongozi wanatakiwa kuwa waadilifu, wenye huruma, utulivu na umakini,” alisema Mbilinyi.
Aliongeza: “Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Zitto hajawahi kutangaza masilahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe Advisors na Leka Dutigite.”
Alisema Zitto kwa kampuni hizo mbili amefanya biashara na mashirika yanayosimamiwa na kamati yake na kulipwa fedha za umma.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma,” alisema.
Alifafanua kuwa Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma, yakiwamo yanayohusu utangazaji wa masilahi.
Zitto ajibu mapigo
Hata hivyo, Zitto mwenyewe alipohojiwa jana, alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) akisema amesikitishwa na kitendo cha kuingizwa katika siasa za majitaka katika kipindi hiki akimuuguza mama yake.
“Kampuni ya Leka Dutigile inamilikiwa na wasanii na Gombe Advisors ni kampuni isiyofanya faida na haina masilahi yoyote ya kiabiashara,” alisema.
“Wasanii wa Kigoma wamefanya kazi na Tanapa na NSSF kazi ambazo zipo na zinajulikana,” alisema Zitto aliyekuwa naibu kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kabla ya kuondolewa.
“Kwa namna yoyote, hii ni ishara ya kukosa ubinadamu maana waliyoyasema wanajua sina faida yeyote ya kifedha, leo wala kesho na Leka Dugitile na Gombe Advisors,” alisisitiza Zitto.

Akizungumza kwa uchungu Zitto alisema “kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi tena mjumbe wa kamati kuu ya chama chao, pole ninayopewa ndiyo hiyo…Hakuna namna ya kukosa ubinadamu zaidi ya hivi”.
Zitto alisema ni vyema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi haraka na yeye atawajibika iwapo ataonekana kwa namna yoyote ile ana masilahi ya kifedha katika kampuni hizo.
Tanapa yafafanua
Naye Meneja Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete alikiri kufahamu jambo hilo na kusema: “Leka Dutigite ilifika Hifadhi ya Saadan na kuitangaza kupitia kazi za sanaa... sikumbuki ni lini lakini walifanya kazi na DvD zake zipo.
“Ifahamike si Leka Dutigite pekee, tunafanya kazi na wasanii mbalimbali kutangaza vivutio, mbuga na hifadhi zetu,” alisema Shelutete.
NSSF nayo yalonga
Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF, Eunice Chiume alisema pesa walizozitoa kwa kundi hilo zilikuwa malipo ya kutengenezea wimbo maalumu wa shirika hilo na nyingine ni za udhamini wa onyesho lililofanyika mwaka jana mkoani Tanga.
“Kweli mara ya kwanza tuliwalipa Sh25 milioni wasanii wa kundi hilo ili watutengenezee wimbo na Sh56 milioni zilikuwa za udhamini wa onyesho lao, lakini kwa masharti ya kututangaza jambo ambalo lilikuwa na mafanikio kwetu kwani tumefanikiwa kupata wateja wapya 30,000 kutoka sekta isiyo rasmi,” alisema Chiume.
Alisisitiza kuwa wametumia kiwango hicho cha pesa ili kujitangaza kwa kuwa hata mashirika ya kijamii yanapaswa kufanya hivyo ili kuvutia wateja wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment