Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Aikaeli Mbowe akiwa na James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba katika harakati za UKAWA hivi karibuni.
KAMBI
rasmi ya upinzani bungeni imeunda upya baraza lake kivuli la mawaziri
kwa kuingiza wabunge wa vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi isipokuwa TLP na
DP. Kiongozi wa kambi hiyo bungeni, Freeman Mbowe alitaja orodha ya
mawaziri vivuli jana mjini Dodoma kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Katika baraza hilo ambalo Mbowe alisema ni taswira ya Ukawa-bungeni,
litakuwa na mawaziri vivuli 28 na manaibu 12 na kufanya jumla ya
mawaziri hao kuwa 40 dhidi ya 51 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Baraza
hilo linaundwa na wabunge 25 wa Chadema chenye wabunge 49.
CUF chenye wabunge 35 kimepata nafasi 11 kwenye baraza hilo na
NCCR-Mageuzi chenye wabunge watano, wabunge wanne ndiyo wameingizwa
kwenye baraza hilo kivuli.
“Tunaonesha kwa vitendo azma ya kushirikiana. Tunaonesha kupitia Ukawa ndani ya Bunge,” alisema Mbowe.
Akizungumzia kutowahusisha Augustine Mrema wa TLP na John Cheyo wa
UDP, Mbowe alisema kwa upande wa Cheyo, upo wakati watahitaji busara
zake watamshirikisha.
Lakini kwa upande wa Mrema alisema hana dhamira ya kuwa mshirika wao.
Alipoulizwa kuhusu kitendo cha Chadema kubeza serikali ya umoja wa
kitaifa Zanzibar na kutaja CUF kuwa imefunga ndoa na CCM, Mbowe alisema,
“ni kweli CUF na Chadema tulitofautiana. Mungu kasaidia Katiba
imetuunganisha na sote tuna malengo sawa.”
Kuhusu mpango wa vyama hivyo kuendelea na ushirikiano na hatimaye
kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mkuu ujao, Mbowe alisema,
“Sisi ni binadamu. Kuna hoja ya kutamani jambo na kuna hoja ya
uhalisia.”
Walioteuliwa Wizara na wabunge walioteuliwa kuziongoza ni Ofisi ya
Rais yenye mawaziri vivuli watatu ambao wote wanatoka Chadema.
Mawaziri hao na wizara zao kwenye mabano ni Profesa Kulikoyela Kahigi
(Utawala Bora), Vincent Nyerere (Menejimenti na Utumishi wa Umma) na
Esther Matiko aliyepewa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu).
Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira) itakuwa chini ya Mchungaji Israel Natse
(Chadema) ambaye atasaidiana na Asaa Othman Hamad (CUF).
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) amepewa Pauline Gekul
(Chadema), Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) itaongozwa na
Rajabu Mohamed Mbarouk (CUF) na Tamisemi ni David Silinde (Chadema).
Mbowe alitaja mawaziri vivuli wengine ni Meshack Opulukwa (Chadema)
ataongoza Wizara ya Kilimo na Ushirika, John Mnyika ataongoza Nishati na
Madini akisaidiana na Raya Ibrahim (Chadema).
Alimtangaza Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia kuwa Waziri wa
Fedha na Uchumi, akichukua nafasi ya Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini. Naibu wa Mbatia atakuwa Christina Lissu. Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaongozwa na Ezekiah Wenje (Chadema) na
Haroub Mohamed (CUF).
Tundu Lissu (Chadema) ni Waziri Kivuli wa Katiba, Sheria na Muungano
akisaidiana na Rashid Abdallah (CUF). Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi)
amepangiwa Wizara ya Ujenzi.
Kwa upande wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, amepewa Mbunge wa Viti
Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) na Wizara ya Uchukuzi imekuwa chini ya
Moses Machali (NCCR-Mageuzi). Wengine ni Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema) anayeongoza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa
kusaidiana na Khatib Said Haji (CUF).
Halima Mdee (Chadema) anaendelea kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi. Aidha katika orodha hiyo ya Ukawa, Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inaongozwa na Rose Kamili (Chadema) pamoja
na Mkiwa Kimwanga (CUF). Maliasili na Utalii inaongozwa na Mbunge wa
Iringa Mjini, Peter Msigwa wakati Ushirikiano wa Afrika Mashariki
inaongozwa na Joseph Selasini (Chadema) pamoja na Rukia Ahmed Kassim
(CUF).
Mbowe pia alimtaja, Masoud Abdallah Salim (CUF) kuwa waziri kivuli wa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Wizara ya Elimu ameendelea
kuwa Suzan Lyimo (Chadema) akisaidiana na Joshua Nassari.
Mbunge wa
Biharamulo Gervas Mbassa (Chadema) amekuwa Waziri ya Afya na Ustawi wa
Jamii akisaidiana na Conchesta Rwamlaza (Chadema). David Kafulila
(NCCR-Mageuzi) amepewa wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Habib Mnyaa (CUF) anaongoza Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia akisaidiana na Lucy Owenya (Chadema). Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto inaongozwa na Baruan Salum (CUF) atakayesaidiana
na Subreena Sungura (Chadema).
Wizara ya Kazi na Ajira inaongozwa na Cesilia Pareso (Chadema).
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akiendelea kuongoza Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo.
No comments:
Post a Comment